The House of Favourite Newspapers

Khadija Kopa Hili la Biashara Atakuwa Amechelewa Mno!

0

NI vigumu kuuzungumzia Muziki wa Taarab nchini bila kumtaja  Malkia Khadija Omar Kopa, hata kama ni binti tu mbele ya Fatma Binti Baraka ambaye tulimfahamu zaidi kama Bi. Kidude.
Mchango wake katika ustawi wa muziki huo nchini na Afrika Mashariki na Kati ni wa kutukuka, kwani katika miaka ile ya mwishoni mwa tisini na mwanzoni mwa 2000, yeye na hasimu wake mkubwa, Nasma Hamis ‘Kidogo’ walikuwa ndiyo wameushika.

Khadija akiwa Tanzania One Theatre (TOT) na Nasma katika kundi lililoongozwa na Norbet Chenga la Muungano Cultural Troupe, walikuwa ‘wabishi’ kwelikweli, kwani huyu alipotoa kibao kimoja ambacho kilipokelewa vyema na mashabiki, mwenzake naye alikijibu na hivyo kuwafanya kuwa washindani waliovutana kwa tungo hadi pale Nasma alipotangulia mbele za haki hapo Juni, 2009.

Licha ya kuwepo kwa vikundi vingi vya taarabu vilivyokuwa maarufu enzi hizo kama vile Egyptian, Babloom, Zanzibar Modern, Dar Modern na nyingine nyingi, bado Muziki wa Taarab uliendelea kuwa chini ya himaya ya waimbaji hao wawili waliojaaliwa miili mikubwa.
Kwa maana hiyo, heshima ambayo anastahili kuwa nayo Khadija Kopa ni kubwa, kwa sababu hadi sasa yeye bado ni mwanamuziki mkubwa.

Hata hivyo, wiki chache zilizopita mkongwe huyu alitoa kauli inayonishawishi kuchangia naye mjadala, maana imenifanya nifikiri mara mbilimbili juu yake. Bi mkubwa alisema muda si mrefu ujao, anataka aache kuimba ili aanze kufanya biashara, kwani anahisi umri unamtupa mkono hivyo uwezo wake jukwaani hautakuwa katika ubora wake.
Suala la kuacha kuimba kutokana na umri huwa haliepukiki, hata kama uwezo utakuwepo, lakini mwili utakuwa umechoka, hautaki kuendana na manjonjo, matokeo yake ni lazima ukubali yaishe.

Lakini alichonishawishi zaidi, ni kauli yake ya kuanza biashara, kwani ameitoa akiwa amechelewa mno, kwa sababu kama ni ujasiriamali, alipaswa kuufanya kipindi kile akiwa na wateja wengi kila kona ya nchi.
Na hili huenda ni kosa wanalofanya vijana wengi hasa wanamichezo, wasanii na watu wa kada zinazotegemea vipaji, kwani mara nyingi hujikuta wakianza kuchukua maamuzi mazuri wakati nafasi yao kwa jamii inapokuwa imepungua au kutoweka kabisa.

Khadija Kopa alikuwa katika nafasi nzuri sana ya kuanza ujasiriamali katika miaka ile alipokuwa kwenye chati ya juu kimuziki, kwani wale mashabiki wangekuwa wateja wakubwa wa bidhaa ambayo angeamua kujihusisha nayo. Siku zote mashabiki huwa ‘crazy’ kwa mtu wao, wako tayari kumsapoti kwa namna yoyote anayoamua kufanya.
Hili pia ni somo kwa makundi mengine niliyoyataja hapo juu. Kama ni mtu mwenye ndoto za kufanya kitu kingine nje ya sanaa au fani unayojihusisha nayo, inayokupatia mashabiki, wakati mzuri ni pale jina lako linapokuwa juu.
Uzoefu wa mashabiki wa nyumbani unaonesha kwamba huwa ni watu wanaokwenda kwa wakati, huwa siyo wenye kuweka sana kumbukumbu na kuenzi. Ni wepesi kuanza kumcheka na kumsimanga mtu waliyekuwa wakimshabikia miaka michache iliyopita.

Muda mzuri wa kuwafanya kuwa upande wako ni kipindi kile unapo-shine, lakini enzi hizo zikipita ni vigumu shabiki wa Mbagala kufunga safari hadi Mwenge kwa ajili ya kumpa sapoti msanii wake aliyeisha makali.
Kama wasanii watafanya hivi mapema, hata wakati wao kisanaa unapokuwa umekwisha, tayari wanakuwa wameshapata uzoefu wa kazi walizoamua kufanya na huenda wameshatengeneza wateja ambao hawafuati jina lake, bali ubora wa bidhaa anayozalisha.

Leave A Reply