The House of Favourite Newspapers

Kiba Akikubali tu Kupatana na Mondi, Amekwisha!

ACHANA na habari za Idris Sultan, weka pembeni ishu ya yule aliyetiwa nguvuni kwa kutishia kuua na bastola, bifu la Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ bado linaendelea kufukuta kwenye ulimwengu wa habari za burudani.

 

Gumzo hilo limeshereheshwa na maneno aliyoyatoa Kiba baada ya kuombwa ahudhurie Tamasha la Wasafi, Kiba akasema; “Unikome!”

Taarifa zinaeleza kwamba mara baada ya sakata hilo kuwa hoti mitandaoni, Kiba anatarajia kuachia ngoma mpya inayokwenda kwa jina la Unikome.

 

Hapa ndipo kwenye msingi wa hoja yangu. Yawezekana kabisa Kiba hakuwa na wazo la ngoma ya Unikome, lakini baada ya neno hilo kupata kiki kwenye mitandao ya kijamii, akaiona fursa ya kuachia ngoma hiyo ambayo bila shaka akiitoa kweli katika kipindi hiki itapata mapokezi mazuri.

 

Hiyo ndiyo faida namba moja ya bifu la Kiba na Diamond au Mondi. Lakini faida nyingine ambayo naiona kwa Kiba, bifu hili kwake ni neema kwani tayari watu walikuwa wameanza kumsahau kama yupo.

Badala ya wafalme mahasimu wa Bongo Fleva kuwa Kiba na Mondi, mahasimu walianza kuwa Mondi na mwanaye wa kumlea kimuziki, Harmonize.

 

Vyombo vya habari tayari vilishachukua hatamu kwamba, mpinzani wa Mondi ni Harmonize ambaye ametoka kwenye lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB) na kwenda kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide.

Huko bwa’mdogo ana studio yake ya muziki. Ana timu ya watenda kazi kama ilivyokuwa tu Wasafi. Ana mameneja wake, ana watu wa kum-brandi ili aonekane kwenye mwonekano wa kistaa.

 

Usisahau, alishafaulu kizingiti cha WCB kuzuia kucheza nyimbo zake hadi atakapolipa shilingi milioni 500 ambazo mkataba ulikuwa unambana pindi atakapoamua kusepa zake.

Akalipa, swali likawa ni je, ataweza kusimamia shoo kivyake? Ataziweza fitina za wapinzani pindi atakapotoa ngoma yake mpya?

 

Huku na huku Harmonize au Harmo akaachia Uno. Bonge moja la ngoma ambalo sasa ndiyo habari ya mjini. Hiyo ikadhihirisha kwamba, amekua na anao uwezo wa kushindana na jeshi la upande wa pili ambalo lina askari kama wote wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 kwenye Bongo Fleva.

 

Kauli aliyoitoa Kiba kwamba kuna mambo Mondi anamfanyia ambayo yeye akiyaanika yatamchafua kama si kumwaibisha, inadhihirisha kwamba kuna vitu Mondi pengine anavifanya ili kumharibia Kiba.

 

Kweli ushindani kwa Kiba na Mondi ulikuwa umeyeyuka ghafla, ule ushindani ‘mwenye kiti chake’ amerudi aliokuja nao Kiba baada ya kupotea kwa muda mrefu ulishasahaulika.

Kudhihirisha kwamba mpinzani si Kiba tena, upande wa pili walikuwa bize kumtengeneza Rayvanny ili sasa awe mbadala wa Harmo pale Wasafi.

 

Ulimwengu wa burudani ulishampa kisogo Kiba, aina ya maisha yake ya kimuziki ni yeye mwenyewe anaijua maana kama ni maadui wa Mondi wapo na walikuwa wanatosha kabisa kumuangusha, lakini wapi bwana.

Wamejaribu kumbeba Kiba ili kuhakikisha wanamuangusha Mondi, lakini hawakufua dafu, Wasafi ndiyo wamelikamata gemu.

 

Yaani iko hivi, ukimtoa Mondi, alikuwa anakuja Harmo halafu ndiyo sasa unamfikiria Kiba. Mbaya zaidi, kuna wengine walianza kuona ushindani upo kwa Wasafi wenyewe kwa wenyewe.

Yaani akitoka Mondi anafuata Harmo ambaye ametoka kisha wanafuata wasanii kutoka WCB, Rayvanny, Mbosso, Lavalava na wengineo.

 

Hivyo basi, ukiliangalia hili bifu kwa jicho la tatu utagundua linamnufaisha zaidi Kiba kuliko Mondi kwani pindi anapokinukisha kama hivi, basi watu wanaanza kumzunguzia Kiba.

Hata ukifuatilia kwa makini, Kiba ndiye amekuwa mzito mno kukubali yaishe na kumaliza tofauti zao licha ya Mondi kujishusha mara kwa mara.

 

Kiba anajua, akikubali tu kupatana na Mondi, basi biashara yake itakuwa imekwisha. Hakutakuwa tena na mtaji wa bifu kama ambao amekuwa akiutumia mara kwa mara!

ERICK EVARIST

Comments are closed.