The House of Favourite Newspapers

KIBOKO ALIYEZUA TAHARUKI MORO, WANANCHI WAGAWANA NYAMA YAKE

KIBOKO aliyezua taharuki kwa saa kadhaa karibu na  makazi ya watu maeneo ya Kihonda-Mbuyuni karibu na Kanisa la Mangwea nje kidogo ya mji wa Morogoro, ameuawa leo kwa kupigwa risasi  na maofisa wa Idara ya Maliasili na nyama yake kugawiwa kwa wananchi waliokuwa eneo hilo.

Kabla ya kuvamia maeneo hayo, kiboko huyo alitoka kwenye Mto Ngerengere alimokuwa akiishi.

Akizungumza na mtandao wa www.globalpublishers.co.tz, Ofisa Wanyamapori Mwandamizi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Privatu Kasisi, amesema wameamua kumuua mnyama huyo kukwepesha madhara ambayo angeweza kusababisha kwani tayari alikuwa amekasirika kutokana na kuzongwa na umati wa watu ambapo angeweza kujeruhi ama kuua mtu.

“Tayari alikuwa amekasirika sana, angeweza kusababisha madhara makubwa mno, hii ni kwa sababu ya kuzongwa na umati mkubwa wa watu, angekuwa hajakasirika tungetumia mbinu zetu za maliasili na tungemrudisha kwenye hifadhi, lakini kwa alipokuwa amefikia, ilikuwa ni bora kumuua,” alisema Privatu.

Baada ya kumuua, maofisa hao walichukua kichwa chake kama nyara ya serikali na uthibitisho wa kwamba ameuawa.

Mamlaka hiyo ilitaka kuwauzia wananchi nyama hiyo lakini Diwani wa Kata ya Kihonda Maghorofani, Ole Gabriel Temba,  aliwaomba wawagawie bure kwani walifanya jitihada kubwa za kumzuia asilete madhara na kufikisha taarifa kwenye mamlaka hiyo.

Maofisa hao waliamua kugawa kilo moja kwa kila mwananchi aliyekuwepo.

 

Aidha, Privatu amesema mnyama huyo anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 na uzito kilo zaidi ya 2,500.

Aliongeza kwamba mnyama huyo aliamua kukimbia kutoka Mto Ngerengere kutokana kupungua kwa kina chake cha maji ili aende kwengine kujihifadhi.

PICHA NA DASTUN SHEKIDELE | GLOBAL TV ONLINE, MOROGORO

Comments are closed.