The House of Favourite Newspapers

Kifo cha Mlinzi wa Mfanyabiashara Songwe Chaibua Mazito

0
Mama wa marehemu Bi. Betha Kaonga. 

KIFO cha kijana Baraka Haonga ambaye alikuwa mlinzi wa Mfanyabiasha Baraka Mwakalinga ‘Bajo’ mkazi wa Mbozi mkoani Songwe, kimezua sintofahamu hali iliyoilazimu familia kuingilia kati.

Mlinzi huyo ambaye amefariki ghafla wiki iliyopita akiwa usingizini nyumbani kwao Ichenjezya, kimezua maswali mengi kwa wakazi wa wilaya ya Mbozi hali iliyosababisha baadhi yao kudai kuwa kimetokana na imani za kishirikina.

MAMA AFUNGUKA

Kufuatia utata huo, Mwandishi wetu alizungumza na Mama mzazi wa marehemu anayejulikana kwa jina la Betha Kaonga ambaye ameeleza ukweli wa kifo cha mwanae Baraka.

Mama huyo amedai kuwa kwa kipindi cha miaka mitano mwanae amekuwa na matatizo ya ugonjwa wa kudondoka (kifafa) na walihangaika kumtafutia tiba  na kumfanyia maombi lakini hawakuweza kufanikiwa.

Waombolezaji wakiwa na jeneza lenye mwili wa marehemu.

“Mwanangu ndani ya miaka mitano iliopita alipatwa na tatizo la kifafa na tumehangaika sana na mwanangu lakini bila mafanikio na huyu bosi wake Bajo ameshatupatia sana usafiri tumsaidie mtoto wangu huku na kule,”  alisema mama mzazi wa marehemu.

Mama huyo aliendelea kufafanua kuwa anashangazwa sana na maneno yanayoendelea hivi sasa juu ya kifo cha mwanae kwa kuhusisha na ushirikina jambo ambalo wao kama familia linawaumiza na amewataka wakazi wa Mbozi kuacha imani potofu kwenye jambo kama hilo.

MWAJIRI HUYU HAPA

Aidha, kwa upande wake mfanyabiashara huyo, Bajo alieleza kusikitishwa na kifo cha mlinzi huyo na kumwelezea kama mmoja wa wafanyakazi wake waliokuwa wachapakazi na waaminifu.

Mfanyabiashara Baraka Mwakalinga ‘Bajo’

“Kwa kweli nimehuzunika sana kumpoteza Baraka, alikuwa kijana mtulivu na mwenye vipaji lukuki ikiwamo uimbaji.

“Nakumbuka kuna kipindi alizidiwa nikamshauri apumzike lakini mama yake mzazi alikuwa kuniomba kuwa aendelee tu hivyohivyo na kazi kwa kuwa kijana huyu ndio alikuwa tegemeo pale kwenye familia yao,” alisema.

Baraka Haonga enzi za uhai wake.

“Kwa kweli nilishirikiana na familia kutafuta matibabu yake, laki ni ndio hivyo tena Mungu amemchukua, ninachowaomba wakazi wa Mbozi waache kuwa na mawazo potofu kwa sababu magonjwa ya aina hii yapo na vifo vya aina hii vipo, kama alivyoeleza mama yake mzazi,” alisema.

HABARI/PICHA: RAHIM NZUNDA GPL SONGWE

Leave A Reply