The House of Favourite Newspapers

Kigogo Dar alidai Uwazi Sh. Mil. 500

0

Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Daudi Yakubu Adam ‘Kanyau’ (pichani) ameliandikia barua ya kisheria gazeti hili akilidai fidia ya Shilingi 500,000,000 kwa madai ya kukashifiwa.

Barua hiyo ya Januari 27, mwaka huu iliyoandikwa na Kampuni ya Brocard Attorneys ya jijini Dar, amedai kukashifiwa kutokana na habari iliyotoka katika gazeti hili la Januari 19, mwaka huu chini ya kichwa cha habari ‘Rais Magufuli kiboko, Kigogo Dar akamatwa kwa unga,’ akidai kuwa habari hiyo ni ya uongo na udhalilishaji kwake, familia na kwa marafiki zake.

Kanyau amesema hajawahi kukamatwa na kuhojiwa kuhusiana na mambo ya ‘unga’. “Kituo cha polisi ambako mteja wetu huwa anakwenda haendi kuhusiana na madawa ya kulevya wala utakatishaji wa fedha,” imesema sehemu ya barua hiyo.

Imeongeza: “Mteja wetu hajawahi kushtakiwa katika mahakama yoyote kuhusiana na madawa ya kulevya au utakatishaji wa fedha.”

Barua hiyo imelitaka gazeti hili kumlipa Kanyau fidia ya shilingi 500,000,000 ndani ya siku saba tangu kuandikwa kwa barua hiyo na kulitaka kukanusha ukurasa wa kwanza kwa ukubwa.

Mhariri wa Gazeti hili, Elvan Stambuli alipoulizwa kuhusiana na barua hiyo alisema: “ Kwanza niwaondoe hofu wasomaji wa gazeti hili niwaambie kuwa tunapoandika habari huwa hatukurupuki. Habari ile ni ya uhakika kwa asilimia 100, lakini Kanyau kwenda kwa wanasheria ni haki yake, hatuwezi kumzuia.” Usikose kusoma muendelezo wa habari hii kwenye gazeti dada na hili, Risasi Jumatano kesho.

Leave A Reply