The House of Favourite Newspapers

Wawili wafa kifo cha kutatanisha

0

Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
SHINYANGA: Watu wawili wamefariki dunia kitatanishi wiki iliyopita baada ya kugusa waya wa kuanikia nguo katika nyumba waliyopanga ambayo haina huduma ya umeme.

Hata hivyo, baadhi ya majirani walisema huenda watu hao walifariki dunia kutokana na hitilafu ya umeme iliyosababishwa na waya kwa ajili ya runinga (cable) uliopita juu ya nyumba hiyo kuelekea nyumba ya jirani.

Waliofariki dunia wametambulika kuwa ni Paskaline Nikomedi (26) aliyekuwa anafua nguo na kuzianika kwenye waya huo na Marco Martine (29) aliyefika eneo la tukio kumsaidia jirani yake huyo.
Mmiliki wa nyumba hiyo, mzee Zabron Mazoya alisema tukio hilo siyo la kawaida kwani nyumba yake haina umeme na kushangaa kuona namna hitilafu hiyo ya umeme ilivyotokea.

Aliongeza kuwa, waya uliosababisha vifo wamekuwa wakiutumia kwa muda mrefu kuanikia nguo hivyo inawezekana ni mambo ya kishirikina.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bondeni, Mohamed Saguti alipoulizwa alisema: “Zimamoto wamefika hapa,wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania nao wamefika lakini wameshindwa kuelewa chanzo cha tukio hili, wamesema watarudi tena kwa vile katika eneo hili wamekata umeme.”

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Injinia Felix Olang amesema bado wanaendelea kufanya uchunguzi juu tukio hilo kwani linachanganya kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na chanzo chochote cha umeme. (Picha kwa hisani ya Malunde 1 Blog.)

Leave A Reply