The House of Favourite Newspapers

Kigogo NIDA Afutiwa Mashtaka

0

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP) amewafutia mashitaka 10 ya utakatishaji fedha washtakiwa watatu kati ya watano akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu.

 

Mbali na Maimu washitakiwa wengine waliofutiwa mashitaka hayo ni aliyekuwa Ofisa Usafirishaji Nida, George Ntalima na Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 

Awali washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka 55 likiwamo utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.

 

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya amedai jana Oktoba 22 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa shauri hilo limekuja kwaajili ya kutajwa lakini wanakusudia kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka.

 

Amedai kesi hiyo iko katika hatua za usikilizwaji lakini Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) amekusudia kufanya marekebisho madogo chini ya kifungu cha 234(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA).

 

“Jumla ya mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ni 55, baada ya marekebisho haya yatakuwa mashtaka 45, kwa mshtakiwa wa kwanza Dickson Maimu, mshtakiwa wa tatu, George Ntalima na wa nne Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo ambao wameondolewa mashtaka ya utakatishaji fedha,” amedai Wakili Komanya.

 

Wakili Komanya amedai endapo hakutakuwa na pingamizi, wangeomba kuwasilisha hati mpya, hata hivyo hati hiyo haikupokelewa kutokana na Hakimu Mkazi Mkuu Rashid Chaungu anayesikiliza kesi kutokuwepo.

 

“Hata mkiwasilisha hati mpya, kesi hii haiko haiko mbele yangu, nawashauri muiwasilishe mbele ya Hakimu husika tarehe itakayopangwa, na kuhusu dhamana nawashauri kuwasilisha maombi Mahakama Kuu,” alieleza Hakimu Shaidi.

 

Baada ya maelezo hayo kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka itakapotajwa ambapo upande wa mashtaka utawasilisha hati mpya.

 

Katika kesi hiyo, tayari upande wa mashitaka umeshafunga ushahidi kwa kuwaita jumla ya mashahidi 26 pamoja na kuwasilisha vielelezo 45. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Meneja Biashara wa (Nida), Aveln Momburi na Mkurugenzi wa Sheria, Sajina Raymond.

Leave A Reply