The House of Favourite Newspapers

Tembo Kufungwa Mikanda ya GPS ya Sh. Mil. 800

 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangallah jana amezindua mpango kuwafunga mikanda ya mawasiliano ya kijiographia (GPS) Tembo  katika hifadhi ya wanyamapori ya  Maswa mkoani Simiyu utakaogharimu zaidi ya Sh. milioni 800.

Alizindua mpango huo katika eneo la makao makuu ya taasisi ya WMA ambayo imewekeza kampuni ya Mwiba Holding,  moja ya makampuni yaliyo chini ya Taasisi ya Friedkin Conservation Fund (FCF) aliposema vifaa hivyo vya GPS vitawezesha tembo kufuatiliwa mienendo yao na kudhibiti  matukio ya wanyama hao kuvamia mashamba na kuwalinda dhidi ya ujangili.

Katika mpango huo pia kutakuwa na uzio wa teknolojia ya kielektroniki ambao utawezesha kuonekana tembo ambao wanatoka maeneo ya hifadhi kabla ya kufanya madhara huku akiipongeza taasisi ya Friedkin Conservation Fund (FCF) kwa kufadhili mradi huo na kueleza wizara yake ilifanya utafiti na kubaini taasisi hiyo ni miongoni mwa taasisi zinazoendekeza uhifadhi  na kuwapongeza watafiti kutoka taasisi ya utafiti wa wanyamapori (TAWIRI) kwa kuendesha zoezi hilo.

Mkurugenzi wa FCF, Nicholas Negri, alisema mradi huo utasaidia uhifadhi nchini na kuvutia watalii zaidi.   Alisema FCF itaendelea kushirikiana na serikali katika kuendeleza uhifadhi kwani pia tayari wamefadhili mradi wa kuwafunga vifaa vya mawasiliano faru ili kuwalinda na ujangili.

Mtafiti Mkuu wa TAWIRI, Dk. Edward Kohi. amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola 300,000 ambazo ni zaidi ya sh 800 milioni. Amesema katika eneo la hifadhi ya Maswa tembo 18 watafungwa vifaa vya GPS na katika maeneo mengine tayari tembo 95 wamefungwa GPS.

 

Mtafiti wa TAWIRI,  Dk.  Emmanuel Masenga amesema hadi sasa tembo 95 wamefungwa mikanda ya GPS maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema mpango huo wa kuwafunga tembo GPS utasaidia kuondoa migogoro baina ya wa hifadhi na jamii. Alisema wananchi wamekuwa wakipiga simu mara kadhaa kuomba msaada pale tembo wanapovamia mashamba yao.

 

“Sasa tembo kufungwa GPS ni faraja kwetu lakini pia tunampongeza mwekezaji wetu Mwiba Holdings kwa mradi huo,” alisema.

Comments are closed.