The House of Favourite Newspapers

Kijana Ajiua kwa Sumu ya Panya Kisa Kudaiwa Sh. 45,000 ya Vinywaji

0

 

Bukindu Bukindu (22), mkazi wa Kijiji cha Ihega, Kata ya Bukoli wilayani Geita amefariki kwa kunywa sumu ya panya siku ya Krismasi, akihofia kudaiwa Sh 45,000 aliyoagizwa kununua vinywaji.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Ally Kitumbu amethibitisha tukio hilo na kueleza uchunguzi unaendelea kupata kiini halisi cha tukio hilo.

Shija Antony, ni mama wa marehemu ambapo kwa masikitiko makubwa, ameelezea mazingira yaliyosababisha mwanaye achukue uamuzi huo wa kujiua kwa kunywa sumu.

Ameeleza kuwa mwanaye alipewa fedha kiasi cha shilingi 45,000 na muuza duka mmoja, aliyemtuma kwenda kumnunulia vinywaji kwenye duka la jumla.

Amesema baada ya kufika duka la jumla alilipia na kukabidhiwa vinywaji na alipotaka kuondoka alizuiwa na kuamriwa kurejesha vinywaji na alipoeleza ameshalipia wahusika hawakumuelewa.

Anazidi kueleza kwamba aliporudi kwa bosi aliyemtuma na kumuelezea hali halisi, alimtaka waongozane mpaka kwenye duka hilo la jumla ambapo wauzaji walidai kwamba kijana huyo alikuwa akitaka kuchukua vinywaji bila kulipia.

Licha ya kujitahidi kujitetea, hakuna aliyemwelewa kijana huyo na bosi akamwambia anataka arudishiwe fedha zake na kijana huyo.

Baada ya mabishano hayo, kijana huyo alirudi nyumbani kwao ambapo alichukua maji na kuingia ndani kisha akafunga mlango ambapo muda mfupi baadaye alianza kutapika na ndipo ilipogundulika kwamba alikuwa amekunywa sumu ya panya.

Jitihada za kumpeleka zahanati kijana huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu, zilifanyika ambapo alipewa huduma ya kwanza lakini baadaye akafariki dunia.

Leave A Reply