The House of Favourite Newspapers

Kijana Mwenye Ulemavu Amlilia DC Jokate

DUNIANI kuna mateso! Ndiyo maneno unayoweza kutamka ukimuona kijana Aloyce Thomas (37) mkazi wa Bagamoyo, Nia Njema aliyepo katika kipindi kigumu kutokana na kupata ulemavu wa miguu kwa kuungua alipoangukia jikoni ambapo amemlilia Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amsaidie.

Akizungumza na Amani, kijana Aloyce alisema alipatwa na janga hilo mwaka 1982, akiwa nyumbani kwao Himo mkoani Kilimanjaro ambapo mama yake alikuwa akipika jikoni, kwa bahati mbaya alitoka kidogo na yeye akiwa mdogo kabisa alijigeuza kitandani kwa bahati akaangukia kwenye moto.

“Nilikuwa mdogo sana sikumbuki maumivu yake sana lakini baada ya kuangukia kwenye moto, mama alipokuja alipiga kelele sana na hapohapo walikuja watu wakanichukua na kunikimbiza Hospitali ya Mawenzi, ambapo walichonifanyia cha kwanza waliwaambia wazazi wangu kuwa natakiwa nikatwe miguu yote ndiyo itakuwa salama yangu,” alisema Aloyce.

Aliendelea kusema kwa uchungu kuwa baada ya kurudi nyumbani akawa bado hajapona ndipo alipopelekwa Hospitali ya KCMC na ambako madaktari walishangaa kwa nini alikatwa miguu yote kwa kuwa kulikuwa na uwezekano wa kutibu bila ya kuikata.

Kijana huyo aliendelea kusema kuwa wazazi wake walihangaika wakamchongea miguu ya bandia lakini baada ya muda wazazi wake walifariki kwa nyakati tofauti, hivyo akanza kuteseka katika kutafuta huduma ya mguu mwingine wa bandia.

“Nilipata taabu sana baada ya wazazi wangu kufariki, kwa kweli nilianza kupata shida ambapo kwa bahati nzuri nilikuwa napata msaada kutoka KCMC, kupitia huduma ya wanafunzi lakini sasa hivi hiyo huduma hamna na ukiangalia miguu yake ya bandia imeoza.

“Yaani naumia sana kwa sababu miguu imeharibika yote mpaka sasa inanitoa vidonda vikubwa, natakiwa niibadilishe lakini sina uwezo huo nimetoka Moshi, kuja kumtafuta Mh. Jokate najua anasaidia sana wagonjwa lakini mpaka sasa sijaweza kumuona.

Aidha alisema gharama ya miguu ni milioni mbili na laki nne ambayo hajaipata mpaka sasa kwa sababu ya kukosa uwezo wa kifedha ndiyo maana alifunga safari kutoka Moshi mpaka Dar kwa ajili ya kumtafuta Jokate amsaidie maana anateseka sana na tangu amalize chuo hajapata kazi. Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo hili na ana chochote cha kumsaidia awasiliane na kijana huyu kwa namba; 0655 192 067.

Stori: Imelda Mtema, Amani

Comments are closed.