The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-19

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale yule mama rafiki wa mama mkubwa aliposhtuka alipopewa taarifa za kifo cha mama Dorcas, kufuatia kukumbushwa kifo cha mama yake, Dorcas akaanza kulia. Je, kilifuatia nini? Endelea…

Yule mgeni alipata huzuni na kumuuliza mama mkubwa kama alichokisema kilikuwa kweli, akamwambia hakuwa na sababu ya kumuongopea kwenye suala la kifo, alijongea kwa mama mkubwa na kumkumbatia akaanza kulia na kumpa pole.

Alipomaliza kumpa pole alihamia kwangu, licha ya kwamba nilikuwa binti mkubwa alinipakata na kunipa pole, kwa dakika kadhaa nyumba ya mama mkubwa iligubikwa na vilio lakini baadaye tulinyamaza.

Baada ya kunyamaza, yule mama alimuuliza mama mkubwa sababu za kifo cha mama, alimfahamisha kwamba kilitokana na ajali.

Taarifa hiyo ilimhuzunisha sana yule mama akatupa pole na kusema kama angepata taarifa za msiba wa mama tungeungana naye kwenda Mpanda.

Baada ya kutufariji kwa muda, yule mama alifungua mkoba wake na kutoa pochi ndogo ambayo aliifungua na kutoa shilingi 20,000, elfu kumi alinipatia na kumi nyingine alimpatia mama mkubwa kama pole.

Hakuishia hapo, alifungua begi lingine akatoa kitenge kimoja akampatia mama mkubwa, mimi alinipatia gauni zuri sana ambalo alisema alikuwa ameliandaa kama zawadi yangu.

Baada ya kumshukuru, alitoa kitenge kingine akanipatia na kusema alikuwa kamletea mama lakini kwa kuwa hakuwepo kitakuwa changu.

Nikiwa nimeshika zawadi hizo, nilijikuta natiririkwa na machozi jambo lililowafanya mama mkubwa na rafiki yake kupata kibarua cha kunisihi ninyamaze.

Nilipotulia, yule mama aliniambia maneno ya faraja kwamba nisilie sana badala yake niwe namuombea mama huko aliko apumzike kwa amani kwani licha ya sisi kumpenda lakini Mungu alimpenda sana akaamua kumchukua.

Nilimshukuru kwa maneno hayo ya faraja, mama mkubwa aliandaa chakula, tulipokula yule mama alituaga kwamba anakwenda kufuatialia mizigo yake angerejea kulala pale nyumbani.

Jioni alirejea akiwa kanunua mahitaji mbalimbali ya nyumbani, katika maongezi yaliyojiri usiku, alimuomba mama mkubwa kama hatajali aondoke nami kwenda nyumbani kwake Shinyanga.

“Nipe muda wa kufikiria jambo hilo kwani siyo la kulifanya haraka,” Dorcas anasema mama mkubwa alimwambia rafiki yake.

Kufuatia kuambiwa hivyo, yule mama mwenye upendo alimwuliza kufikiria nini wakati naye alikuwa sawa na mama yake na alihitaji kunifariji kwa kufiwa na mama?

Mama mkubwa alimfahamisha kwamba alikuwa sahihi lakini akumbuke nilikuwa mtoto wa watu hivyo kuniruhusu tu kwenda Shinyanga bila hata ndugu yeyote wa mama kufahamu isingekuwa vizuri.

Mama mkubwa alipotoa kauli hiyo, yule mama alimwelewa na kusema awasiliane na ndugu wa mama atakaporejea tena Mbeya angeondoka nami.

Kwa upande wangu, nilifurahi sana kuhamia Shinyanga bila kujua kama huko ndiko ungekuwa mwanzo wa mateso yaliyobadilisha kabisa maisha yangu.

Usiku huo tulizungumza mambo mengi ambapo yule mama wa Shinyanga alitusimulia jinsi anavyoishi vizuri na familia yake na kwamba siku ambayo ningefika kwake angejisikia faraja sana.

Kulipokucha, niliwaaga mama zangu hao nikaenda shuleni na niliporejea alasiri mama mkubwa alinifahamisha kwamba rafiki yake aliondoka kuelekea Tabora.

Mama aliniambia kuwa, yule mama alikuwa na upendo sana ambapo nilimuunga mkono kisha aliniuliza kama nilikuwa tayari kwenda kuishi naye Shinyanga.

Kwa kuwa bado sikukomaa sana akili, nilimwambia nilikuwa tayari akacheka na kunieleza akiwasiliana na mjomba wangu akimruhusu ningeenda Shinyanga.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply