The House of Favourite Newspapers

Wamerudi tena

0

Hans Mloli,Dar es Salaam
VITA ya mechi za wikiendi iliyopita imeshasahaulika na leo Jumatano timu 10 zitadondoka dimbani kuwania pointi tatu muhimu lakini gumzo kubwa ni kwa vigogo wa Ligi Kuu Bara, ambapo Yanga itakuwa Dar kwenye Uwanja wa Taifa ikivaana na Toto Africans wakati Simba yenyewe ikiikabili Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Yanga itaingia uwanjani ikiwa na jeraha la kuondoka na pointi moja katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC baada ya kutoka sare ya bao 1-1 hivyo itataka kurekebisha makosa yake na kuondoka na pointi tatu ikiendelea kuusaka ubingwa.
Katika michezo ya awali, Yanga ilifanikiwa kushinda yote mitano kabla ya kusimamishwa na Azam, ingawa bado ipo kileleni kwa pointi 16 ilizofungana na Azam, wakifuatiwa na Simba na Mtibwa Sugar zenye pointi 15 kila mmoja. Yanga na Azam zimeachana kwa tofauti ya mabao.

Lakini Toto yenyewe inayoonekana kusuasua kwenye michezo yake saba ya awali baada ya kutoa sare mechi nne, kushinda mbili na kufungwa moja, itahitaji kujiweka sawa leo kwa ushindi kabla jua halijazama na hivyo kuzidisha utamu wa mchezo huo.

Pamoja na hayo, Yanga imeamua kutumia mbinu za ziada kwa ajili kujihakikishia ushindi leo baada ya kumtuma shushushu kwenye mchezo wa mwisho wa Toto waliosuluhu na Ndanda FC, ambaye tayari ameshakabidhi ripoti ya juu ya alichokiona kwa Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm.

Ingawa Pluijm hakuwa tayari kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, lakini Championi Jumatano lililokuwepo kwenye mazoezi ya Yanga juzi Jumatatu na jana Jumanne kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar lilishuhudia baadhi ya mbinu na mikakati mipya tofauti na siku za nyuma ikisukwa uwanjani hapo kwa ajili ya mchezo huo.

“Haya ni mazoezi kwa ajili ya kurekebisha makosa tuliyoyaona kwenye mechi iliyopita, kuna baadhi ya mambo ya kiufundi tunayafanyia kazi kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Toto.

“Siifahamu wala sijawahi kuiona Toto lakini nikuhakikishie hiyo si shida yetu kubwa, ishu hapa ni kushinda na kupata pointi tatu ndiyo tutakachokifanya kesho (leo),” alisema Pluijm.

Kwa upande wa Simba iliyo chini ya Muingereza, Dylan Kerr, imeendelea na mwendo wa ushindi baada ya Jumamosi iliyopita kuipiga Mbeya City bao 1-0, hivyo leo itaingia kifua mbele dhidi ya Prisons iliyojeruhiwa baada ya kupigwa mabao 3-0 na Stand United.

Hata hivyo, Simba inayotarajia kukamilika kila idara leo baada ya kuwepo kwa uhakika wa kurejea kwa baadhi ya wachezaji wake waliokuwa nje wakisumbuliwa na majeraha, ilishaapa tangu awali kuwa haitaacha kitu Mbeya na itahakikisha inaondoka na pointi sita kwa kuikandamiza Prisons pia.

“Nimeambiwa Prisons ni timu ngumu kwa Simba lakini sina wasiwasi wowote, timu yangu ipo fiti na tayari tumeshazoea mazingira ya Mbeya. Lengo ni ushindi tu bila ya kujali chochote, shida hapa ni kuvuna pointi zote sita licha ya mimi binafsi kutowafahamu vizuri Prisons,” alisema Kerr.

Huku kocha wa Prisons, Salum Mayanga, akisema kama wakishindwa kushinda hakika watatafuta hata sare kitu ambacho hawatashindwa.

Kama Simba watashinda na Yanga watapoteza mchezo huo, basi vijana hao wa Msimbazi watakaa kileleni,

Michezo mingine inayotarajiwa kupigwa leo ni pamoja na Stand United dhidi ya Majimaji FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, na Coastal Union itakuwa kibaruani dhidi ya Kagera Sugar huko Mkwakwani, Tanga.

Leave A Reply