The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-23

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale yule mama wa Shinyanga alipomuhusia Dorcas aliyekuwa amevunja ungo namna ya kujiepusha na masuala ya wanaume ambao alimweleza wangemuharibia maisha yake kisha akampa mfano wa wasichana walioharibikiwa na maisha baada ya kupata mimba wakiwa shuleni. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Licha ya kupewa tahadhari hiyo na mama, kwa kuwa nilikuwa napitia kipindi cha ukubwa nilikuwa napata hisia za mapenzi lakini nilikuwa nikijizuia kwa kuwa bize na kazi za nyumbani.

Kadiri siku zilivyokuwa zikisonga, kuna baadhi ya walimu wa kiume wakawa wakinisifia na yupo mmoja akaanzisha tabia ya kuniita ofisini na kunipa zawadi ya madaftari na kusema alifanya hivyo kwa sababu nilikuwa nafanya vizuri katika masomo yangu.

Mwalimu huyo ambaye niligundua nia yake, kuna wakati alikuwa akinipa fedha ambazo nilizikataa, kwa ujumla nami nilijijua nilikuwa mrembo haswa kwani hata wasichana wenzangu pia walinisifia.

Niliendelea na masomo huku nikikwepa vishawishi vya wanaume hadi tulipofunga shule likizo ya pasaka, kwa kuwa ilikuwa fupi kaka Evance hakuja Shinyanga.

Baada ya sikukuu hiyo, tulifungua shule ambapo niliendelea na masomo hadi ulipofika mwezi wa tano mwishoni tulifunga kwa ajili ya likizo ya mwezi mmoja na wiki moja.
Wakati huo, kaka Evance naye alikuja likizo ya miezi mitatu kama sijakosea, aliponiona aliniambia kwamba nilikuwa nimekuwa mdada, nikamwambia ndiyo akaishia kucheka.

Kaka alifurahi sana alipoona matokeo ya mitihani niliyofanya ambapo alinisifia, nilimshukuru kwani kwa sehemu msaada wake ndiyo uliosababisha pia nifanye vizuri.

Kama ilivyokuwa likizo ya awali, hakuacha kunifundisha na kuwa karibu nami ambapo alinieleza nikikutana na jambo lolote gumu katika masomo nimwambie ili anisaidie.
Baada ya kukaa nyumbani wiki mbili, alifanikiwa kupata kibarua kwenye mradi mmoja wa Wazungu uliokuwa ukishughulika na masuala ya mazingira.

Kufuatia kupata kibarua hicho akawa anatoka nyumbani asubuhi na kurejea jioni, mama alifurahi sana na kuniambia nifuate nyao za kaka yangu kwani kusoma lilikuwa jambo zuri ndiyo maana hata kabla hajamaliza chuo aliweza kupata kazi.

Nilimwambia mama nitajitahidi kuwa kama kaka Evance, mama alifurahi sana kusikia hivyo, nakumbuka kaka alipopata mshahara wake wa kwanza, sehemu ya fedha alizolipwa alimpatia mama, akanininua viatu mimi na mdogo wake Emmy ambaye hakumpenda sana sababu alikuwa hapendi shule.

Niliendelea na masomo na kaka aliendelea na kazi hadi muda wake wa kurudi chuoni ulipowadia aliaga alikokuwa akifanyia kazi na siku mbili baadaye alikwenda Dar es Salaam kuendelea na masomo.

Ilipofika Oktoba mwishoni tulifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba na kwa jinsi nilivyokuwa nimejiandaa nilikuwa najua matokeo yatakapotoka nitakuwa miongoni mwa wanafunzi watakaofaulu.

Kaka alipokuja nyumbani wakati wa Sikukuu ya Chrismasi na Mwaka Mpya aliniuliza kama nitafaulu, nilimwambia ilikuwa lazima, akafurahi sana.

Kama nilivyokuwa nategemea, matokeo yalipotoa nilikuwa nimefaulu, kila mmoja alifurahi sana na kunipongeza, nilimshukuru sana kaka Evance kwa msaada wake ulioniwezesha kufaulu.

Ilipofika Januari nilianza masomo ya sekondari katika shule iliyopo palepale mjini, kaka aliniambia japo alikuwa mbali atajitahidi kunitafutia vitabu na kunitumia.

Wakati nikiwa kidato cha kwanza katika shule hiyo ya kutwa, bado niliendelea kusumbuliwa na wanaume kutokana na uzuri wangu kwani nikiwa kama binti niliyekua nilikuwa najipenda sana.

Pamoja na kusumbuliwa na wanaume wakiwemo wenye fedha zao, sikuzuzuka nikaendelea na msimamo wangu jambo ambalo lilimfurahisha sana mama.
Marafiki zangu ambao hawakuwa watulivu walikuwa wakinicheka kufuatia kutokuwa na mpenzi kama walivyokuwa wao lakini hawakuweza kubadili msimamo wangu.

Kutokana na msimamo huo, akina mama wengi walinitolea mfano kwa watoto wao kwamba waniige jinsi nilivyokuwa, kwa ujumla nilikuwa najisikia vizuri sana kusifiwa.
Kama kawaida, tulipofika katikati tulifunga shule kwa likizo ambapo kaka Evance alikuja Shinyanga kwa mapumziko marefu, aliponiona alifurahi sana.

Kama ilivyokuwa awali akawa yupo karibu nami katika kunifundisha na wakati mwingine alikuwa akinisubiri tule pamoja, alikuwa akionesha kunijali kwa kila kitu.

Tofauti na wakati nilipokuwa nasoma shule ya msingi ambapo alikuwa akinifundisha masomo nisiyoyaelewa sebuleni wakati mwingine nje ya nyumba yetu, akawa anapenda kuniita chumbani kwake.

Awali nilikuwa nahofu lakini kwa vile nilimchukulia kama kaka yangu wa damu, sikuwa na wasiwasi nikawa naingia ambapo alikuwa akinifundisha kusoma na namna ya kutumia kompyuta yake mpakato ‘laptop’.

Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga akawa anaonesha dalili za mapenzi ndipo kengele ya tahadhari ililia kichwani mwangu nikaanza kumkwepa, kila aliponiambia nikajisomee chumbani kwake nikawa najifanya nipo bize au kumwambia tukae sebuleni.

Niliendelea na msimamo wangu hadi aliporudi chuoni, nami nikaendelea na masomo lakini mara kwa mara alipokuwa akimpigia simu mama aliomba anipatie simu ili aweze kuongea nami.

Maisha yaliendelea hadi tulipofunga tena shule kwa ajili ya likizo ya Desemba ambapo kaka Evance alikuja Shinyanga kwa ajili ya Sikukuu ya Krisamsi na Mwaka Mpya, wakati huo mama alikuwa anaendelea na biashara zake za kusafiri.

Nakumbuka wakati wa likizo hiyo, pale nyumbani watu walisafiri kwenda kijijini nilibaki mimi, Emmy, mama na Evance.

Kama ilivyokuwa kawaida yake, Evance mara kwa mara alikuwa akipenda kuwa na mimi na hata marafiki zake waligundua hilo wakaanza kumsema vibaya lakini hakujali.
Kaka aliendelea kuwa karibu nami kunifundisha masomo na namna ya kutumia laptop yake ambapo alisema ilikuwa muhimu sana kujua kuitumia.

Mara kwa mara alikuwa akiniita chumbani kwake akawa ananifundisha baadhi ya masomo, kuna siku alifanya kitu kilichonishangaza sana.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply