The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-38

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mjomba wa akina Bite, Barton na Monica alipofika nyumbani kwao ambapo walimchangamkia. Mjomba huyo alipomuuliza Dorcas kama alianza shule akamwambia bado na alipomuuliza dada yake akasema mumewe alikuwa akishughulikia suala hilo. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Baada ya kuambiwa hivyo, mjomba alifurahi sana ndipo alimuuliza dada yake za tangu walipoachana siku ile tuliyotoka Shinyanga, akamwambia zilikuwa nzuri.
Mjomba aliyeonekana kuwa na haraka, kabla ya kuondoka alitoa pochi yake akachomoa noti mbili za shilingi elfu kumi na kumpatia mama kisha akaaga na kuondoka.

Ingawa tangu nilipofika sikumsikia mama akizungumzia suala langu la shule, nilifurahishwa na upendo aliouonesha mjomba kwa kumuuliza mama jambo hilo.
“Huyu mjomba inaonekana anapenda sana mambo ya shule, maana alipofika tu hapa suala la kwanza kutaka kujua ni kama nimeanza kusoma,” niliwaza.

Nikiwa chumbani na Tabu baada ya mjomba kuondoka, mama ambaye tangu nilipofika sikuwahi kumuona akiwa bize kwa kazi yoyote alituita.
Tulipokwenda kuitikia wito alituambia tuchukue mahindi, ulezi na karanga tuchambue kisha twende tukasage unga kwa ajili ya uji ambao ulipendwa sana na familia ile.
Wakati anatuambia hivyo, akina Bite na Monica walikuwa sebuleni wamewasha runinga wanaangalia muziki, kitendo hicho kilinikwaza, nilipomuuliza Tabu kuhusu tabia hiyo akaniambia niachane nao.
“Dorcas usipende kuishi kwa kushindana, mimi hao nimewazoea kikubwa omba Mungu uanze kusoma kama mama alivyokuahidi,” Tabu aliniambia.

Nilimshukuru Tabu kwa ushauri wake, tulipomaliza kuchambua mahindi, karanga na ulezi mama alitupatia hela tukashika njia kwenda mashineni.
Tukiwa njiani Tabu alinisimulia historia ya maisha yake kwamba kwenye familia yao walizaliwa wawili na kaka yake ambaye wakati huo alikuwa akitumikia kifungo kwa kesi ya kusingiziwa.
Alinifahamisha kwamba kiasili kwao ni Kigoma vijijini na kwamba wazazi wake walikufa kwa Ukimwi na kuwaacha wakiwa wadogo, akasimama na kuanza kulia.

Kufuatia hali hiyo nilibaini alikumbuka jambo lililomuumiza nikamsihi anyamaze, akatulia na kusema;
“Hata hii kazi naifanya kwa sababu ya matatizo tu kwani naamini kama baba na mama wangekuwa hai licha ya kwamba walikuwa ni wakulima maskini, nisingeifanya zaidi ningesoma kwa bidii ili elimu inikomboe,” Tabu aliniambia.

Tabu alinifahamisha kwamba kaka yake aliyeitwa Samweli alikuwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka miwili baada ya kusingiziwa aliiba baiskeli.
Alisema tukio hilo lilimuumiza sana kwani kabla ya kufungwa alikuwa msaada sana kwake kwani fedha alizopata baada ya kufanya vibarua ziliwawezesha kupata mahitaji yao na walikuwa wanapendana sana.
“Kila nikimkumbuka kaka naumia kwani yupo gerezani anatumikia kifungo kisicho halali, kama kweli angekuwa ameiba ningesema alijitakia, kweli hii dunia wakati mwingine haina huruma,” Tabu aliniambia na kuanza kulia tena.

Kitendo cha Tabu kulia, kilinikumbusha mateso niliyopitia likiwemo tukio la kubakwa na Evance, nikajikuta nami nalia kitendo kilichowafanya akina mama wawili waliotuona tukiwa tunalia huku tumetua mfuko wa mahindi kutufuata na kutuuliza tulipatwa na masaibu gani.
Kwa kuwa sikupenda kuwaambia ukweli niliwadanganya kwamba tulipata taarifa ya msiba wa mdogo wetu huko Mbeya, walitupa pole na kutuambia tusilie turudi nyumbani.

Mama mmoja alipotueleza hivyo tulitulia, walipoendelea na mambo yao nasi tulibeba mfuko wetu na kuelekea mashineni, bahati mbaya tulipofika huko tulikuta umeme umekatika.
Tukiwa tunasubiri Tabu aliniambia baada ya kaka yake kufungwa na maisha ya kijijini kuwa magumu alichukuliwa na dada mmoja na kumleta Dar kwa ajili ya kufanya kazi za ndani.
Aliongeza kuwa, alipokaa na dada huyo miezi sita alianza kumfanyia visa ndipo msichana mmoja rafiki yake alimshauri aache kazi na kumtafutia kazi kwa mama Bite.

Tabu aliniambia hata kwa mama huyo alikuwa anavumilia mengi kwa sababu alikuwa mkali hata kwa mambo yasiyostahili na kuna wakati alipokosea jambo alikuwa akimchapa na kumtukana.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa mkasa huu wiki ijayo. Maoni tumia namba iliyopo hapo juu.

Leave A Reply