The House of Favourite Newspapers

Kimenuka Bukoba… Madereva Wagoma, Sababu Hizi Hapa!

MADEREVA wa daladala wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamegoma kusafirisha abiria baada ya kupandishiwa gharama za maegesho leo Jumanne, Novemba 27, 2018 asubuhi huku wasafiri kwenda maeneo mbalimbali mkoani humo wakishindwa kusafiri kutoka stendi ya mabasi Bukoba baada ya kutokea kwa mgomo huo.

 

Inadaiwa kuwa madereva hao wamepinga ongezeko la ushuru kotoka Tsh. 1,000 hadi Tsh. 2,000 kwa magari madogo (Hiace) na Tsh. 2,000 hadi Tsh. 4,000 kwa Coster huku kukiwa hakuna maboresho yaliyofanyika kituoni hapo.

Aidha, Mwenyekiti Chama cha Kutetea Abiria Kagera (CHAKUA), Samidu Bashiru amepinga ongezeko hilo na kuongeza stendi hiyo haina choo wala jengo la kupumzikia abiria.

 

Kamanda wa Polisi Bukoba, Revocatus Malimi amesema jeshi hilo linafuatilia ili kubaini waliogoma ni madereva au ni wamiliki wa magari, na kwamba  jeshi hilo litatoa taarifa juu ya mgomo huo.

 

 

“Taarifa ni za kweli ila jeshi letu linafuatilia lijue madai yao ni nini, pia tunahitaji kujua waliogoma ni wasafirishaji au ni abiria, na tumeambiwa ni mgomo baridi wa kutokutoa huduma,” amesema Kamanda Malimi.

 

Mapema leo majira ya saa 3 asubuhi zilianza kusambaa taarifa juu ya kutokea kwa mgomo wa madereva wa daladala kutokutoa huduma za usafiri wakielekeza malalamiko yao kwa manispaa ya Bukoba. Mbali na madai hayo pia inaelezwa kuwa madereva hao pia wanagomea juu ya ubovu wa miundombinu kwenye eneo ambalo wamekuwa wakiegesha magari yao.

MAGUFULI: LOWASSA Wambie Wenzako, Wataishia Gerezani

Comments are closed.