The House of Favourite Newspapers

MAGUFULI: LOWASSA Waambie Wenzako, “Wataishia Gerezani” – Video

RAIS Dkt. John Magufuli amempa ujumbe Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowasa awaambie viongozi wengine wa vyama vya upinzani kuwa watulie “la sivyo wataishia magerezani”.

 

Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Novemba 27, katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mara baada ya kumsifia Lowassa, kuwa ni mwanasiasa mstaarabu ambaye alionyesha utulivu hata baada ya kushindwa kweny uchaguzi wa urais mwaka 2015.

 

“Ninakupongeza sana Lowassa, hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka, vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo, nimeona hili nilizungumze kwa dhati na kwa kabisa ili wale unaowaongoza ukawashauri watulie, la sivyo wataishia kwenye magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za nchi,” alisema Magufuli.

 

Hadi sasa, viongozi kadhaa wa upinzani, hasa Chadema wana kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali nchini; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

 

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walifutiwa dhamana mahakamani Kisutu kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria, uchochezi na uasi.

 

Wengine wanaoshtakiwa katika kesi hiyo, ni Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji, Naibu Katibu MKuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mch. Peter Msigwa, John Heche, Halima Mdee, Esther Bulaya.

 

Jana pia Mahakama ya Kisutu ilielezwa kuwa upelelezi wa kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe umekamilika na sasa itaanza kusikilizwa mahakamani hapo.

 

Akizindua maktaba hiyo ya kisasa yenye uwezo wakuchukua wanafunzi 2,100 na kutunza vitabu 800,000, Rais Magufuli amesema heshima iliyojengwa na UDSM inatakiwa iendelee kuwepo na wanafunzi wapate yanayostahili kwa wakati.

MAGUFULI: LOWASSA Wambie Wenzako, Wataishia Gerezani

Comments are closed.