The House of Favourite Newspapers

Kiongozi Huyu Aliyedaiwa Kulewa Pombe Mbele ya JPM, Siri Nzito Yafichuka

0
Isihaka Juma Karanda alipowasili kwenye ofisi za Global Publishers hivi karibuni.

 

DAR ES SALAAM: Wakati Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani, Mrisho Swagara akitoa shutuma nzito kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Humprey Polepole kwa kumtaka aache propaganda dhidi ya chama chake kwa kumpokea Isihaka Juma Karanda aliyedai siyo kiongozi wao, jamaa huyo amejitokeza na kufichua siri nzito.

 

Isihaka Juma Karanda alivyopata ajali.

 

Akijibu shutuma dhidi yake, Karanda aliyefika katika ofisi za gazeti hili Jumamosi iliyopita alisema amesikitishwa na kitendo cha Swagara kumkana kwamba hajawahi kuwa kiongozi wa chama hicho wakati anajua alikifanyia makubwa chama cha ACT Wazalendo akiwa ni katibu mwenezi wa mkoa.

“Nashangaa kuona wananikana huku nikizushiwa kwamba mimi ni mlevi eti kwa sababu sizungumzi vizuri.

 

Isihaka Juma Karanda akionesha jeraha

 

Viongozi wote wa mkoa, wilaya na wanachama wa chama hicho wanajua kwamba hali ya kushindwa kuzungumza vizuri imenitokea baada ya kupata ajali mbaya ya kugongwa na gari mwaka 2012 iliyonifanya nilale kitandani kwa miaka miwili,” alisema Karanda huku akitoa nyaraka mbalimbali za Hospitali ya Tumbi Kibaha na picha kuthibitidha kauli yake.

Alifafanua kuwa baada ya ajali hiyo ambayo ilikuwa mbaya yalifunguliwa majalada polisi Kibaha moja namba KIN/TR/ AR/4632 /2012 la Novemba 19, 2012 na KIN/TR/RB/4649/2012 la Novemba 19, 2012 na baadaye ikafunguliwa kesi ya trafiki namba 1342 ya 2012 akishitakiwa dereva Carlo Francesco Soglia aliyesababisha ajali hiyo kwa uendeshaji mbaya.

 

Isihaka baada ya kutoka hospitali

 

Akikigeukia Chama cha ACT Wazalendo, Karanda alisema kuwa amefanya mambo mengi akiwa katibu mwenezi katika chama hicho hasa wakati wa kampeni za mwaka 2015 kwani alitumia gari lake aina ya Toyota Noah bure bila kudai fedha za mafuta na jitihada hizo zikafanikiwa kumpata diwani wa Kata ya Mbwawa.

“Nilikua nazunguka na gari langu Kisarawe, Bagamoyo na kuna kiasi kikubwa cha fedha nilitumia katika kampeni zile na nyingine nilikiazima chama huku wenzangu katika chama wakidai nyingine atapelekewa Zitto Kabwe Kigoma kwenye kampeni, sijui kama walipeleka kwa sababu nilifanya bidii kuonana naye ikashindikana,” alidai Karanda. Alisema amesikitika kuona anapakaziwa kwamba yeye alikuwa amelewa alipokutana na rais wakati wanachama wengi na baadhi ya wananchi wa Kibaha wanajua kwa nini amekuwa na kasoro wakati anazungumza na Swagara anajua hilo.

 

Isihaka akifanya mahojiano na Mhariri wa Uwazi, Elvan Stambuli

 

“Mwenyekiti wa Swagara unajua nilivyougua hakika nisingekuwa na fedha ningeweza kufariki dunia katika ajali ile, nilikuwa natumia zaidi ya shilingi laki mbili kwa kununua dawa,” alisema.

Aliongeza kuwa Mgombea Ubunge wa Kibaha Mjini kwa tiketi ya ACT, Habib Machange alishirikiana naye wakati wote wa kampeni akiwa na mwanachama maarufu, Warda Hafidhi Ramadhani aliyekuwepo wakati wa mahojiano haya.

 

Akisimulia jinsi alivyorejea CCM, Karanda alisema aliomba CCM mkoa na wakamjibu siku ileile.

“Mimi Polepole sijawahi kuongea naye kabla. Viongozi wa mkoa nilizungumza nao siku ileile ya mkutano, waliniambia niende nimekubaliwa, hivyo, nikaenda kukabidhiwa kadi,” alisema.

 

Aliongeza kuwa anawaomba wote wale wenye nia mbaya kuhusu kujiunga kwake CCM, wamuache rais afanye kazi yake nzuri na asiingiliwe na mtu mwingine yeyote.

 

“Wanaosema nililewa anawaona na ndiye aliyetaka niwe hivi, yeye Mola atawajibu kwa sababu sikuomba niwe hivi.

“Nashukuru nina akili timamu kabisa, licha ya kunusurika kifo.

 

“Lakini pia vyombo vya habari vilivyosema nilikuwa nimelewa mbele ya rais wanatakiwa kunisafisha, wamenidhalilisha sana, kwa nini hawakunihoji?” alisema.

 

Naye mwanachama wa ACT Warda Ramadhani aliyefuatana na Karanda alisema ni kweli kiongozi huyo alikuwa katibu mwenezi wa ACT na alikuwa msaada mkubwa kwa chama.

 

“Nimeamua kufuatana naye kuja hapa ofisini kwa sababu wamemfanyia kitu kibaya sana. Huwezi kumzushia mtu kashfa mbaya wakati ukweli unajulikana. Kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama akitakacho,” alisema Warda.

 

Juni 21, 2017 akihutubia wananchi kwenye Viwanja vya Bwawani, Kibaha Mjini, Mwenyekiti wa CCM, Magufuli alitumia fursa hiyo kumruhusu Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole kumwingiza Karanda CCM.

 

Hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Mkoa wa Pwani, kudai kwamba Karanda hakuwa na nafasi yoyote katika Kamati ya Uongozi ya Mkoa wa Pwani wala wilaya yoyote ya mkoa huo.

 

Stori: Elvan Stambuli | DAR ES SALAAM

 

Rais Magufuli Akumbana na Kada wa Upinzani Akiwa Ziarani Pwani, Tazama Kilichotokea

Leave A Reply