The House of Favourite Newspapers

Kisa Balinya, Kalengo… Zahera Awahisha Fasta Kambi Yanga

UONGOZI wa Yanga umetaja sababu ya kuwahi kuanza maandalizi ya kikosi chao kuwa ni idadi kubwa ya wachezaji wapya waliowasajili katika kuisuka timu hiyo ili iwe tishio msimu ujao.

 

Yanga hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kuwasajili wachezaji kumi ambao ni Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Ally Ally, Issa Bigirimana ‘Walcott’, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Lamine Moro na Suleyman Mustapha.

 

Pia, Yanga inatarajiwa kukamilisha usajili wa wachezaji wanne wanaoshiriki Afcon nchini Misri ambao ni kipa Mkenya Farouk Shikhalo, Metacha Mnata, Ally Sonzo na Gadiel Michael.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ni kuwa idadi kubwa ya wachezaji wapya waliowasajili ndiyo imesababisha kuanza haraka maandalizi ya kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mwakalebela alisema kuwa kikubwa kocha anataka kuona wachezaji wapya wanashika kwa haraka mifumo na mbinu anazozitumia ili kabla ya ligi kuanza, basi wawe wameshashika mbinu zake zote.

 

Aliongeza kuwa, kingine anataka kuona timu inaungana kwa haraka kwa wachezaji kucheza kwa kuelewana kati ya wa zamani na wapya ili kuhakikisha wanacheza kitimu na kwa kuelewana.

 

“Kambi yetu ya pamoja ya timu inatarajiwa kuanza Julai 7, mwaka huu na wachezaji kutoka nje ya nchi wataanza kutua nchini kuanzia Julai 4 kabla ya kuingia kambini na kuanza mazoezi.

“Tumeanza mapema maandalizi kwa ajili ya kuiunga timu iliyo na wachezaji kumi ambao tayari tumewasajili achana na hao watatu tuliokwenda kuwasajili nchini Misri kwenye kikosi cha Stars ukitoa Gadiel ambaye yeye tumemuongezea mkataba mpya.

“Usajili wetu umekamilika kwa asilimia 80 kwa maana ya kufanikiwa kusajili wachezaji wote tuliokuwa kwenye mipango ambao kocha wetu Zahera aliwapendekeza.

“Bado tunaendelea kuangalia baadhi ya sehemu zenye upungufu ambazo kocha alizitolea mapendekezo na kama mambo yakikamilika, basi haraka tutafanikisha usajili huo.

 

“Kambi tumepanga kuianza mapema kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha ambayo ameyatoa kama unavyofahamu nusu ya wachezaji wetu ni wapya, ni lazima kocha akae nao pamoja muda mrefu kwa ajili ya kuwapa mbinu na mifumo mbalimbali ya uchezaji anayoitumia, pia timu iunge kati ya wachezaji wapya na wa zamani ili icheze kitimu,” alisema Mwakalebela.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

TUNDAMAN AAPA – “SIWEZI Kuimba Nyimbo za YANGA Mimi SIMBA”

Comments are closed.