The House of Favourite Newspapers

Kisa Dola za Kimarekani, JPM Acharuka, Atoa Agizo BoT (Video)

RAIS John Magufuli amemwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, kuhakikisha malipo kwa kutumia fedha za kigeni  nchini yanadhibitiwa ili kulinda thamani ya pesa ya Tanzania isiporomoke.

Magufuli ametoa agizo hilo leo, Desemba 13, 2017 wakati akitoa hotuba alipokuwa akizindua Tawi la CRDB Bank mjini Dodoma.

“Nilizuia mkataba ulioandaliwa na Benki Kuu uliopanga kulipa kwa Dola za Kimarekani. Nasema jambo hili likiendelea wasinilaumu. Benki Kuu, kuna watu 17 wenye PhD lakini waliruhusu benki moja kufanya biashara hapa nchini bila kutambua kuwa ni ya kibababishaji, mpaka ilipozuiwa Marekani ndipo wakashtuka,” alisema Magufuli.

 

Aidha Rais Magufuli ameitaka BoT kuzifuta benki zaote ambazo hazifanyi vizuri.

“Niwaombe BoT, mabenki ambayo hayafanyi vizuri msisite kuyafungia na kuacha mambo ya kubebanabebana, heri kubaki na benki tano zinazofanya vizuri kuliko kuwa na benki nyingi zisizo na tija kwa uchumi wa taifa letu.

“Kwa mujibu wa ripoti za BoT, mwaka 2015 ukwasi wa benki ulikuwa trilioni 20.5 kiasi ambacho ni kidogo sana, kulinganisha na benki tulizo nazo nchini.  Tatizo la riba katika mabenki hapa nchini bado liko juu, tatizo hili linasababishwa na watu kutolipa na hivyo kuongeza gharama za ufuatiliaji.

 

“Nikuagize Waziri wa Fedha, BoT na benki zote uzisimamie kikamilifu, nchi nyingine ukienda na Dola huwezi kununua kitu chochote, hapa kwetu Tanzania unaweza kufanya chochote.  Tutaendelea kutoa vitambulisho vya taifa, benki zianze kupunguza viwango vya kodi ili benki ziwe na sera zinazowiana na zenye tija.”

Rais pia amependekeza CRDB Bank kujenga makao yao makuu Dodoma kwani serikali kuu yote inahamia huko na ndiyo makao makuu ya nchi sambamba na kuboresha huduma zao.

 

“Naomba mtambue kuwa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi na hivi karibuni tumefanya maamuzi makubwa ya kuhakikisha Serikali yote inahamia hapa, na mimi nitahamia hivi karibuni, sasa tutaona nani anabaki huko Dar.

“Natoa wito kwenu CRDB, msambaze huduma zenu hadi vijijini ambapo Watanzania walio wengi wanaishi. Mfikiri njia mbalimbali na kuanzisha matawi mengi ikiwemo benki kwa njia ya mtandao.

“Najua Makao Makuu yenu yapo Dar lakini nitoe wito kwenu CRDB muangalie utaratibu wa kujenga makao makuu hapa Dodoma. Itasaidia kutangaza benki yenu na hata mkiwa na jambo mtasaidiwa haraka kwa sababu hata makao makuu ya Serikali yatakuwa hapa.

 

“Napenda kutoa wito kwa wananchi wa Dodoma wawe na utamaduni wa kujiwekea fedha benki kwani itawasaidia kwa kiasi kikubwa sana. Tutaendelea kutoa vitambulisho vya taifa benki zianze kupunguza viwango vya kodi ili benki ziwe na sera zinazowiana.

“Hii hundi ya shilingi milioni 100 mliyonipatia namkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ikajenge wodi ya wagonjwa katika hospitali ya Dodoma na nitafuatilia. Sasa ole wake iliwe! Kwa heshima ya Benki ya CRDB wodi hiyo itaitwa Wodi ya CRDB.

“Niziombe mahakama ziharakishe kesi zinazohusiana na mikopo, kama mtu anatakiwa kufilisiwa hakimu anachelewesha nini?

 

“Sambamba na hayo, lazima tuangalie, tuweke utaratibu unaoeleweka, zaidi ya Dola bilioni moja zimeshikwa uwanja wa ndege ni kwa sababu Tazania imeonekana ni kichaka cha fedha za kigeni.

“Tuliwahi kufungua benki moja, fedha zikaonekana ziko Tanzania lakini zilikuwapo asilimia 15 tu.  Benki inataka kufilisika mnaomba fedha kutoka hazina ziende kusaidia, hiyo hapana; nataka fedha ziende kusaidia wananchi siyo ziende kuokoa jahazi.

“Mabenki na kampuni zote za simu zihahikikishe zinajiunga na utaratibu mpya, kampuni zitakazoshindwa utaratibu ufanyike la sivyo ifungiwe kufanya kazi nchini,” alisema Rais Magufuli.

LIVE: Hotuba ya JPM Kwenye Ufunguzi wa Tawi la CRDB BANK, Dodoma

Comments are closed.