The House of Favourite Newspapers

Kisa rambirambi… Mwanamke akodiwa matarumbeta

0

Fedheha ilioje! Mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Maria ameonja joto ya jiwe baada ya kudaiwa ‘kuchikichia’ fedha za rambirambi kiasi cha shilingi laki mbili na elfu themanini (280,000) kisha kukodiwa matarumbeta na ngoma maarufu kwa jina la Kigoma cha Uruguay.

Mwanamama huyo ambaye ni mmoja wa wasusi wa Mwenge jijini Dar alikumbwa na kisanga hicho hivi karibuni maeneo hayo ya Mwenge-Sokoni ambapo ilibidi akimbilie polisi kujinusuru huku akisindikizwa na matarumbeta na ngoma iliyokodishwa na wasusi wenzake katika zoezi la utoaji wa fedha hizo.

Shuhuda wa kuaminika alilitonya gazeti hili kuwa, kisa cha yote hayo ni kufuatia kifo cha msusi mwenzao ambaye alifariki dunia hivyo siku ya mazishi walishauriana wamkabidhi padri fedha hizo za rambirambi ili atangaze kuwa kuna wenzake wamemchangia.

Mpashaji wetu alisema kuwa wakati wakishauriana, Maria alisema ana mtazamo tofauti kuwa kuliko wamkabidhi padri fedha hizo ni bora wampe yeye (Maria) akae nazo ili amkabidhi mtoto wa marehemu zimsaidie kulipa ada ya shule, jambo ambalo walikubaliana naye.

Shuhuda huyo aliendelea kumwaga ‘ubuyu’ kwamba, baada ya kumkabidhi fedha hizo Maria, alimwambia mtoto huyo wa marehemu kuwa baada ya siku mbili, aende maeneo ya Mwenge  kuzichukua lakini cha ajabu ni kwamba kila alipokuwa akimfuata alikuwa akimzungusha na kumwambia kwa nini anamfuata bila taarifa.

Ilidaiwa kwamba, kitendo cha Maria kumrudisha mtoto huyo kila wakati, kiliwauma wenzake hivyo ikabidi wamfungie kazi na kwenda kudai fedha na kama haitoshi wakakodi hadi ngoma ili kusindikiza utoaji wa fedha hizo.

Wakati sekeseke hilo likifunga mtaa wa Mwenge-Sokoni, gazeti hili lilitia nanga eneo la tukio ambapo liliwashuhudia wasusi hao wakiwa kwenye hekaheka na wengine kucheza ngoma wakitaka fedha hizo zitolewe.

Katika hali ya aibu, Maria alikimbilia kwenye Kituo Kidogo cha Polisi cha Mwenge na kuzitoa fedha hizo.

Amani lilipomfuata Maria na kumuuliza kwa nini alikubali fedheha hiyo impate badala ya kulipa fedha hizo za rambirambi mapema, alisema kuwa anachoamini ni kwamba waliomfanyia hivyo siyo wote walikuwa na nia na ile fedha bali kumfedhehesha na kumshusha kwani yeye hakuwa na nia mbaya hata kidogo kuhusiana na fedha hizo.

Leave A Reply