The House of Favourite Newspapers

Kisa Uchaguzi: Majengo ya Serikali, Magari Yachomwa Moto

0

BAADHI ya wananchi wenye hasira mkoani Lindi, wanadaiwa kufanya uharibifu wa mali za umma ikiwamo kuchoma majengo ya serikali, binafsi na vyombo vya usafiri kama magari, pikipiki na kusababisha hasara kubwa.

 

Hasara na uharibifu huo, vinadaiwa kusababishwa na mambo ya kisiasa.

 

Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi, ameyaeleza hayo mjini Lindi, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na uharibifu uliofanywa wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

 

Watu hao wanadaiwa kufanya fujo kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi ulivyokwenda, kutokana na kile kinachodaiwa kuhujumiwa, ikiwamo madai ya kuzuiliwa mawakala kuingia vituoni, ongezeko la vituo hewa vilivyo nje ya mfumo na vitambulisho vya kupigia kura.

 

Madai mengine ni kubadilishiwa matokeo ya ushindi ya mgombea aliyeshinda kupewa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Zambi alisema katika fujo hizo, magari zaidi ya saba kati ya hayo mawili ya polisi, majengo ya serikali pamoja na binafsi tisa na pikipiki moja, yaliharibiwa kwa kuchomwa moto.

 

Zambi alizitaja wilaya zilizoathirika kutokana na uharibifu huo kuwa ni Liwale, Nachingwea, Kilwa na Lindi katika Halmashauri ya Mtama. Amesema huko Liwale magari zaidi ya saba, likiwamo la polisi na binafsi yaliyokodiwa kusaidia uchaguzi huo, yaliharibiwa, na kwamba nyumba mbili na magari matatu ya Mbunge mteule, Mohamed Kuchauka yalihusika katika hujuma hizo.

 

Imo pia zahanati ya Diwani mteule Kata ya Liwale Mjini, Omari Mkoyage na nyumba moja ya askari polisi. Zambi alisema wilayani Nachingwea, magari matatu na nyumba, mali za Diwani mteule Ahamadi Makoroganya, gari moja la polisi na nyumba zimechomwa moto, huku jengo la Mahakama Wilaya limenusurika licha ya kuwamo kwenye orodha ya kutaka kuichomwa.

 

Kwa mujibu wa Zambi, Halmashauri ya Mtama, watu hao walichoma moto majengo mawili, ikiwamo ofisi ya muda anayoitumia Mkurugenzi Mtendaji, Samuel Waryoba, Ofisi ya Serikali ya Kata ya Mtene na jengo la saluni la mtendaji wa kata hiyo. Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa kwa ajili ya mahojiano, kwa lengo la kuwabaini waliohusika.

Leave A Reply