The House of Favourite Newspapers

Kisa Wawa, Pluijm abadili mbinu

0

Pluijm

Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.

Said Ally,Dar es Salaam
UWEPO wa beki kisiki wa Azam, Pascal Serge Wawa katika eneo la ulinzi la timu hiyo, umemfanya Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm kuja na mbinu mpya ambayo ataitumia kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi katika mechi baina ya timu hizo.

Yanga na Azam zinatarajiwa kukutana kesho Jumamosi katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ambapo presha ni kubwa kwa kila upande.
Pluijm amefikia maamuzi hayo kutokana na kuwa safu ya ulinzi ya Azam inayoongozwa na Wawa imekuwa ngumu kufungika.

Mbinu hizo za mabadiliko aliamua kuzifanya katika mazoezi ya timu hiyo Jumanne ya wiki hii kwenye Uwanja wa Boko Veteran, Boko jijini Dar ambapo alitoa mazoezi ya krosi na mashuti nje ya eneo la 18 huku Donald Ngoma akiongoza zoezi hilo.

“Natambua kuwa wapinzani wetu wapo vizuri katika eneo la ulinzi, lazima tutafute mbinu nyingi zaidi za kuweza kupata mabao kama tukishindwa kuweza kuwapita na kuingia katika boksi lao,” alisema Pluijm na kuongeza:

“Katika wiki hii yote, program kubwa nimeifanya kwenye umaliziaji pekee, kikubwa ninataka mabao mengi yatokee pembeni kwa njia ya krosi.”

Wakati huohuo, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mchezo huo ambapo kiingilio cha chini ni shilingi 5,000 kwa viti vyenye rangi ya bluu, kijani na machungwa.

Kingilio cha juu kitakuwa shilingi 30,000 kwa VIP A na shilingi 20,000 kwa VIP B & C, ambapo tiketi zitauzwa siku ya mchezo katika eneo la Uwanja wa Taifa.

Mwamuzi wa kati anatarajiwa kuwa Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga, akisaidiwa na Makame Mdogo (Shinyanga), Robert Luhemeja (Mara), mwamuzi wa akiba Frank Komba (Dar) huku Kamisaa wa mchezo akiwa Joseph Mapunda kutoka Ruvuma.

Leave A Reply