The House of Favourite Newspapers

Kizizi cha Bocco balaa Simba

SIKIA hii. Nahodha wa Simba, John Bocco akikufunga tu, ujue siku hiyo tatu zinakuhusu. Ameweka rekodi ya aina yake katika michezo aliyopata nafasi ya kuifungia timu yake kwani mechi zote alizofunga Simba ilishinda mabao matatu.

 

Bocco ambaye msimu uliopita alitupia mabao 14 na msimu huu aliliambia Spoti Xtra kuwa atafunga mabao mengi zaidi ya hayo alianza kwa kusuasua kutokana na kusumbuliwa na majeruhi na alifungulia bao lake la kwanza kwenye mchezo wake dhidi ya Mwadui.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mwadui Complex Bocco alifunga mabao mawili na bao la tatu likafungwa na Meddie Kagere na kufanya Simba ishinde mabao 3-1. Pia katika mchezo wake dhidi ya Singida Bocco aliifungia timu yake na ilishinda mabao 3-0, pia kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Mwadui Bocco alifunga bao moja na kuiongoza Simba kushinda mabao 3-0.

 

Hakuishia hapo mchezo wake dhidi ya African Lyon alitupia mabao mawili na mchezo ulikamilika kwa mabao 3-0, juzi aliendeleza rekodi hiyo baada ya kuwatungua mabosi wake wa zamani Azam FC Simba ilishinda mabao 3-1, rekodi hii haijawekwa na nahodha yeyote Bongo kwa sasa.

 

Bocco mpaka sasa ana mabao saba huku timu yeke ikiwa imefunga mabao 38 ikiwa nafasi ya tatu na pointi 45 huku Azam wakiwa nafasi ya pili na pointi 50, wakiachwa nyuma na wapinzani wao Yanga ambao ni vinara wenye pointi 61.

 

“Kila mchezo ambao uko mbele yetu ni kupambana na kuondoka na pointi tatu muhimu na hilo ndiyo jambo la msingi wanaosema tuna viporo kazi kwao sisi ni kucheza tu. “Hilo ndiyo jambo la msingi na tunapokwenda kucheza na timu hatuangalii historia ya nyuma ilikuwaje zaidi ni jinsi gani sisi tunaweza kufanikiwa kupata pointi.

Comments are closed.