The House of Favourite Newspapers

Matola Atumia Mbinu za Zahera

Kocha Mkuu wa Lipuli FC ya mkoani Iringa, Selemani Matola.

KOCHA Mkuu wa Lipuli FC ya mkoani Iringa, Selemani Matola amepanga kuingia na mbinu za Kocha Mkuu Mkongomani wa Yanga, Mwinyi Zahera kuhakikisha anaizuia Simba. Timu hizo zinavaana Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Samora, Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara msimu huu unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.

 

Lipuli ina rekodi nzuri kwenye wake huo wa nyumbani ya kutokufungwa na Simba tangu timu hiyo imepanda kucheza ligi msimu wa 2017/2018.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Matola alisema Simba wazuri sehemu ya katikati, hivyo ili afanikiwe hataki kuwapa nafasi ya kucheza viungo wa timu hiyo wanaoongozwa na Mzambia, Clatous Chama, Jonas Mkude, James Kotei, Hassani Dilunga na Haruna Niyonzima.

Matola alisema, mbinu hiyo ilitumika na Zahera ambayo alifanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha kwanza wakati timu hizo zilipokutana kabla ya kipindi cha pili kufanya mabadiliko ambayo yalimgharimu kufungwa bao 1-0. “Nilifurahishwa na mbinu za Zahera alizoingia nazo kwenye mchezo alioingia nao katika kipindi cha kwanza kwa kutowapa nafasi viungo wa Simba kumiliki safu ya kiungo ambayo ipo vizuri.

 

“Viungo wa Yanga wakiongozwa na Tshishimbi (Papy), Fei Toto (Feisal Salim) na Ajibu (Ibrahim) ambao wenyewe walifanikiwa kuwamudu viungo wa Simba kwa kutowapa nafasi ya kupiga pasi kwa washambuliaji wao ambao hatari Okwi (Emmanuel), Kagere (Meddie) na Bocco (John).

 

“Na hilo lipo wazi utaona katika kipindi cha kwanza Simba hawakufanikiwa kupiga shuti kabla ya kipindi cha pili kufanya mabadiliko, hivyo nitakavyoingia katika mchezo huo na kikubwa ninataka kupata pointi kwenye kila mechi nitakayocheza nyumbani,” alisema Matola.

WILBERT MOLANDI, DAR ES SALAAM

Comments are closed.