The House of Favourite Newspapers

Kocha Mpya Abadili Mifumo Ya Aussems

0

  JUZI jioni wachezaji wa Simba sura zilibadilika na kuonekana wakijitafakari baada ya Kocha Mkuu mpya, Mbelgiji Sven Vanderbroeck kutangaza kuanzia jana Ijumaa wataanza kufanya program mbili za mazoezi asubuhi na jioni.

 

Kocha huyo alitoa kauli hiyo mara baada ya mazoezi ya timu hiyo kumalizika yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja Simba Mo Arena uliopo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Mbelgiji huyo aliyemrithi Patrick Aussems jana Ijumaa alitarajiwa kuanza rasmi kibarua cha kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na michezo yake ya Ligi Kuu Bara.

 

Kocha wa viungo wa timu hiyo, Adel Zrane ndiye aliyetumwa kutoa tangazo hilo la kuongeza program ya mazoezi ya kufanya mara mbili kwa siku ambayo awali wakiwa na Aussems walikuwa wakifanya mara moja pekee jioni.

Lakini ujio wa kocha huyo mpya umeonekana kubadili mifumo kadhaa ambayo alikuwa akiitumia Aussems wakati akiinoa Simba.

Baadhi ya mifumo ambayo Aussems alikuwa nayo Simba ni kufanya mazoezi mara moja kwa siku pia wachezaji walikuwa hawakai kambini lakini sasa vitu hivyo vimebadilika.

Adel akitoa tangazo hilo la kuongeza program ya mazoezi, mastaa wa timu hiyo walionekana kukunja nyuso zao wakionekana kutotaka kufanya program hizo mbili za mazoezi na badala ya moja.

 

“Kuanzia kesho (jana) program ya mazoezi itabadilika, tutakuwa tunafanya program mbili za mazoezi asubuhi na jioni na siyo mara moja kama ilivyokuwa awali.

 

“Hivyo wachezaji wote nendeni kambini mkiwa mnafahamu kuwa kesho tutakuwa na program mbili za mazoezi asubuhi na jioni,” alisikika Adel akiwatangazia wachezaji hao uwanjani hapo na baadhi vichwa vikawa chini.

Aidha, katika hatua nyingine Vanderbroeck alifanya mahojiano na mtandao wa timu hiyo na kuahidi kuifanyia makubwa akisema kuwa: “Lengo langu la kwanza ni kushinda ubingwa wa ligi kuu. Nataka kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, nataka kucheza mashindano ya Caf. Nataka Simba iwe kwenye hatua kubwa na kupata matokeo mazuri.

 

“Kilichonivutia Simba cha kwanza ni wingi wa mashabiki. Ni jambo la kufurahisha kuona mashabiki 60,000 wakikushangilia inakupa hisia za kipekee.”

Naye kocha msaidizi, Matola alisema kuwa juzi usiku alifanya kikao kizito na Vanderbroeck na kikubwa ni kuandaa program nzuri ya mazoezi na kuweka mikakati thabiti ya ushindi katika michezo ya ligi ili kuhakikisha wanauchukua ubingwa wa ligi.

 

“Juzi usiku mara baada ya chakula cha usiku nilikutana na kocha kwa ajili ya kuandaa program ya mazoezi, pia kuhusu mechi ya kirafiki kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji ili kabla ya mchezo wa ligi dhidi ya Lipuli awe ashawajua wachezaji,” alisema Matola.

STORI NA Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply