Kocha Mpya Simba Huyu Hapa Raia wa Kenya

TAARIFA zinasema kuwa, Klabu ya Simba, ipo kwenye mazungumzo na Kocha Abdul Idd Salim raia wa Kenya kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Muharami Mohammed aliyeondolewa hivi karibuni kikosini hapo.

 

Muharami ambaye alikuwa akiwanoa makipa wa Simba tangu Julai 2017, amesitishiwa ajira yake kwa kile kilichoelezwa kwamba ameshindwa kuwaongoza vema makipa wa timu hiyo, Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim.

 

Simba baada ya kuachana na Muharami, wameanza mazungumzo na Salim ambaye kwa sasa anawanoa makipa wa timu ya Sheikh Russel inayoshiriki Ligi Kuu ya Bangladesh.

 

Salim aliwahi kuwanoa makipa wa Simba katika vipindi viwili tofauti ambapo mara ya kwanza alitua Juni 2015 wakati Kocha Mkuu wa Simba akiwa, Dylan Kerr raia wa England, kisha akaondolewa na kurudi tena Desemba 2016, kipindi Simba ikinolewa na Mcameroon, Joseph Omog ambapo kwenye vipindi vyote alifanya kazi nzuri sana.

 

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, uamuzi wa kumrudisha kocha huyo ni baada ya kuona ndiye kocha atakayewafaa kwa wakati huu ili kurudisha viwango vya makipa wao lakini anaweza kuwasaidia sana kwenye michuano ya kimataifa.

 

“Baada ya kuachana na Muharami, haraka uongozi umeanza mazungumzo na yule kocha wetu wa zamani wa makipa, Abdul Salim kuja kuchukua nafasi yake.

 

“Mazungumzo yameanza vizuri, tunaamini yatakamilika haraka na kuja kusaini mkataba wa kuwanoa makipa wetu haraka sana,” kilisema chanzo.

 

Spoti Xtra lilipomtafuta Salim kwa njia ya simu akiwa Bangladesh ambaye ana leseni A ya kuwanoa makipa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Uefa, alisema: “Mimi bado nina mkataba wa miaka mitano na timu yangu huku lakini kuna uwezekano wa kuondoka endapo itatokea dili sehemu nyingine.

 

“Unajua kwa muda wa miaka miwili sijafundisha soka Afrika, nilipoondoka Simba nikaja huku kufundisha ambapo nipo hadi sasa.“Taarifa za mimi kutakiwa na Simba ni mpya na ninazisikia kutoka kwako.

 

Tusubiri nini kitatokea, lakini nipo tayari kurudi kufundisha Tanzania.”Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’, imeamua kuchukua uamuzi huo wa haraka ili kurudisha heshima yao na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

STORI NA MWANDISHI WETU | SPOTI XTRA

Toa comment