The House of Favourite Newspapers

Kocha Msauz Aomba Kazi Simba, Alikuwa Msadizi wa Pitso Mosimane Al Ahly

0
Cavin Johnson

UONGOZI wa klabu ya Simba umeweka wazi bado upo katika mchakato wa kutafuta kocha mpya wa kukiongoza kikosi hiko katika michuano mbalimbali ambayo wanashiriki kwa sasa huku wakiweka wazi mmoja wa makocha wakubwa barani Afrika tayari ameshatuma CV zake kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo.

 

Simba kwa sasa ipo chini ya kocha Juma Mgunda ambapo inakabiliwa na mtihani mzito mbele ya wapinzani wao, Premeiro de Agosto kutoka Angola ambapo wanatakiwa kuhakikisha wanasonga mbele katika michuano hiyo na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Chanzo cha ndani kutoka Simba, kimeliambia Championi Jumatano kuwa, tayari baadhi ya makocha wametuma CV zao kwa ajili ya kuomba kazi ya kuifundisha timu hiyo, huku likiwemo jina la aliyekuwa msaidizi wa Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane, Cavin Johnson.

 

“Tayari kuna makocha wengi tu wameanza kutuma CV (wasifu) za kutaka kuifundisha Simba na mmoja kati ya makocha wakubwa ambao wameomba nafasi hiyo ni Cavin Johnson ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Al Ahly chini ya kocha Pitso Mosimane.

 

“Mchakato bado haujakamilika, ukikamilika nadhani uongozi watafuata taratibu zao kama wanavyofanya siku zote,” kilisema chanzo.

 

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmedy Ally aliliambia Championi Jumatano kuwa: “Kwa sasa Wanasimba wawe watulivu timu ipo chini ya kocha Juma Mgunda na matokeo ni kama yanavyoonekana timu inashinda na inafanya vizuri jambo ambalo tunashukuru kuona hivyo.

 

“Mchakato wa kocha mpya kwa sasa bado unaendelea na makocha wanaendelea kutuma CV zao kwa ajili ya kuomba nafasi za kuinoa timu kubwa hii ya Simba na kama kutakuwa na lolote juu ya upatikanaji wa kocha mpya na mchakato unavyoendelea basi kila kitu tutaweka hadharani.”

 

Calvin Johnson ni kocha mwenye uraia wa Afrika Kusini ambaye amewahi kufundisha timu kubwa kama Platinum Stars, SuperSport United, AmaZulu na Black Leopards kabla ya kuungana na Pitso Mosimane kuwa msaidizi wake ndani ya Al Ahly.

Na Marco Mzumbe

Leave A Reply