Kocha Simba: Bocco Atakwenda Kuwavaa Gendarmarie Nationale

John Bocco

SIMBA kupitia kwa Kocha wao Msaidizi, Masoud Djuma wamesisitiza kwamba hata kama John Bocco anaumwa enka lazima awepo kwenye msafara utakaoondoka leo Jumapili jioni kwenda Djibouti kuwavaa Gendarmarie Nationale.

 

Bocco aliumia enka katika mchezo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga, uliochezwa katikati ya wiki na kutolewa kabla ya mchezo kumalizika huku Simba ikitoa sare ya bao 1-1.

 

Djuma aliiambia Spoti Xtra kwamba ; “Bocco anaendelea vizuri na hana tatizo na mtu yeyote, hata kama ni majeruhi ni nahodha wetu lazima aende atakiongoza kikosi katika safari na pia tutaangalia kutokana na vipimo atakayofanyiwa, iwapo atakuwa vizuri ataweza kucheza na kama atakuwa bado basi hatutamtumia.”

 

“Tutaangalia jinsi afya yake ilivyo kwani tunaweza kumtumia mchezaji kisha ikawa shida kwenye mechi zinazofuata za ligi, tunahitaji kuwa na kikosi imara cha ushindani kwa kuhakikisha kila mchezaji anakuwa fiti,” alisema Djuma.

 

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha unamlinda vilivyo Bocco.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Omog ambaye kwa sasa yupo jijini Yaounde nchini Cameroon alisema kuwa Bocco ndiye muhimili wa timu hiyo kwa hiyo uongozi wa timu hiyo unapaswa kuwa makini naye.

 

“Tangu niondoke bado nimeendelea kufuatilia mechi za Simba na niliumia sana baada ya Bocco kuumizwa katika mechi dhidi ya Mwadui FC.

 

‘’Niuombe uongozi wa Simba kuhakikisha unamlinda sana Bocco kwani yeye ndiye muhimili wa timu huu, ikitokea akawa nje ya uwanja kwa muda mrefu, litakuwa ni pigo kubwa kwao katika kipindi hiki ambacho wanapambana kuhakikisha wananyakua ubingwa wa ligi kuu msimu huu,’’ alisema Omog.

 

Hata hivyo, Daktari wa Simba, Yasin Gembe alisema kuwa jitihada za kumlinda mchezaji huyo tayari zimeishafanyika hivyo wanaamini ataitumikia timu hiyo kama kawaida.

 

Wachezaji wengine wa Simba watakaoondoka na kikosi hicho leo ni pamoja na Aishi Manula, Emmanuel Mseja, Erasto Nyoni, Ally Shomari, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Asante Kwasi, Shomari Kapombe, Yusuf Mlipili, Paul Bukaba, Juuko Murshid na James Kotei.

 

Wengine ni Jonas Mkude, Muzamiru Yasini, Shiza Kichuya, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Moses Kitandu, pamoja na Emmanuel Okwi.

STORI: KHADIJA MNGWAI | SPOTI XTRA

Loading...

Toa comment