The House of Favourite Newspapers

Kocha Yanga Abadili Program Ya Mazoezi

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mserbia, Zlatko Krmpotic, ni kama vile ameshtukia kitu baada ya juzi kuongeza program katika mazoezi ya timu hiyo ili kukiimarisha kikosi chake.

 

Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya Yanga kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo juzi Jumanne aliongeza program ya mazoezi na kufanya mara mbili kwa siku badala ya moja kama ilivyokuwa awali.

 

Mtoa taarifa huyo ambaye yupo kambini Yanga maeneo ya Avic Town, Kigamboni, Dar, alisema kocha huyo amefikia hatua ya kuongeza program ya mazoezi kwa sababu mbili, kati ya hizo ni kuwaongezea fitinesi wachezaji.

 

Aliitaja sababu nyingine ni wachezaji wake akiwemo Carlos Carlinhos wazoeane ili wacheze kitimu ndani ya muda mfupi ili kuhakikisha timu yake inapata matokeo mazuri.

“Kocha ameona upungufu wa timu yake baada ya mchezo wa kwanza wa ligi na kubaini tatizo. Moja ya upungufu aliouona ni wachezaji wake kukosa fitinesi, hivyo amepanga kulifanyia kazi kwa kuwapa mazoezi ya fitinesi ili vijana wake wamudu kucheza dakika 90.

 

“Upungufu mwingine ni timu yake kushindwa kucheza kitimu wakati wachezaji wake wanapokuwa na mpira wakilishambulia goli la wapinzani na hiyo imetokana na nusu ya kikosi cha kwanza kuundwa na wachezaji wapya wengi, hivyo atatumia wiki hii moja kuwafanyisha mazoezi pamoja ili kulimaliza tatizo hilo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alithibitisha hilo kwa kusema: “Kocha aliona upungufu wa kikosi chetu, hivyo amepanga kuufanyia kazi ili kuhakikisha anakuwa timu itakayocheza kwa kuelewana.

 

“Tayari ameongeza program ya mazoezi ambayo kila siku timu itakuwa inafanya mara mbili, lengo ni kuhakikisha anakiboresha kikosi chake na kupata matokeo mazuri.

 

”Mpaka sasa wachezaji wengi wanaonekana hawana fiziki huku Carlinhos akionekana kutokuwa fiti kutokana na kutocheza kwa muda mrefu.

STORI: WILBERT MOLANDI, DAR

Leave A Reply