The House of Favourite Newspapers

Kondakta Mshindi wa Nyumba Ageuka Mcharo Dom

0
George Majaba akiwa na familia yake.

KONDAKTA wa basi aliyeshinda zawadi ya nyumba katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba, ambaye ni mkazi wa Makole, Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, hivi sasa anajiandaa kukabidhiwa mjengo huo uliojengwa Bunju B, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Majaba, mwenye umri wa miaka 42 akiwa na familia yake, waliyapokea matokeo ya droo kubwa iliyochezeshwa Septemba 27 mwaka huu katika Viwanja vya Las Vegas, Mabibo jijini Dar es Salaam kwa shangwe kubwa.

Kutokana na ushindi huo, habari kutoka Dodoma zinasema hivi sasa Majaba amekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa mji huo pamoja na vijiji ambavyo magari anayoyafanyia kazi yanapita.

 

George Majaba na familia yake.

“Aaah bwana Majaba sasa hivi amekuwa mcharo aisee, yaani kila mtu amekuwa akitaka kumuona na kushangaa kama kweli ndiye mshindi halisi wa nyumba, kila anapopita anapata shangwe za kufa mtu,” alisema Idrianiseri Nasoroni, mmoja wa vijana wapiga debe katika stendi ya Dodoma.

Majaba mwenyewe akizungumza na Ijumaa alisema; “Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti ya Global, nimekuwa nikisoma kwa zaidi ya miaka 15, mara nyingi huwa sikosi magazeti yenu, hasa ya michezo kwa kuwa mimi ni mdau mzuri wa michezo.

“Shindano hili lilipoanza nikawa nakusanya magazeti na kujaza kuponi, nilikuwa nakusanya huku naendelea kufanya kazi zangu.

“Mimi ni kondakta wa mabasi yanayotoka hapa Dodoma yanaelekea vijijini maeneo kama Dabalo.

“Mara ya kwanza nilikusanya kuponi 73 nikazituma huko Dar, mara ya pili nikakusanya kuponi 46, sasa siku ya kuzituma kuna baadhi nilikuwa sijazijaza, nikaenda nazo Posta kwa ajili ya kuzituma, kufi ka nikawa nazijaza nikiwa hapohapo Posta, sasa wakati naendelea wakaniambia wanataka kufunga na kuzisafi risha, nikawa nazijaza harakaharaka.”

“Kuponi zote nilikuwa najaza namba ya simu, nadhani haraka ya kujaza siku hiyo ndiyo nikasahau kujaza namba katika hiyo kuponi niliyoshinda.

“Sasa Jumatano iliyopita nilirudi nyumbani mapema, nikawa nasikiliza michezo kwenye simu nikiwa nje ya pale Makole ninapokaa, hiyo nyumba nimepanga.

George Majaba na mkewe na mtoto wao.

“Watoto wakanifuata na kuniambia wamepigiwa simu kuwa nimeonekana Channel Ten, natafutwa Dar nimeshinda nyumba, nikashangaa sana na kujiuliza mbona sijapigiwa simu, baadaye simu zikaanza kupigwa nyingi kwangu kwa watu wanaonifahamu hadi ikazima chaji,” alisema Majaba.

Nakala ya gazeti moja la Championi linauzwa kwa shilingi mia tano, sawa na magazeti mengine ya Global Publishers ambayo ni Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi na Amani.

Kwa maana hiyo, nakala 119 ambazo msomaji huyo alitumia kununua magazeti hayo, ni sawa na shilingi 59, 500 tu, ambazo zimemuwezesha kujipatia nyumba hiyo yenye thamani ya mamilioni ya shilingi, ambayo ina samani zote za kisasa ndani.

Nyumba hiyo iliyojengwa eneo la Bunju B nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ina vyumba vitatu, ikiwemo Master Bed Room, jiko, chumba cha chakula, maongezi, choo na bafu.

Kana kwamba haitoshi, mmiliki huyo mpya, atakabidhiwa nyumba ikiwa tayari imeshaunganishwa nishati ya umeme.

Katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Kwanza, Nelly Mwangosi, Mkazi wa Iringa Mjini, aliibuka mshindi wa nyumba iliyojengwa Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar.

Na Mwandishi Wetu

Hii Kali! Kulala na Kuamka Umejishindia Nyumba! Majaba Aelezea Furaha Yake

Leave A Reply