The House of Favourite Newspapers

kudaaaadeki

0

Omary Mdose
Dar es Salaam
KUNA msemo wa raha ya ngoma uingie ucheze, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mashabiki wa Simba ambao jana jioni waliondoka Uwanja wa Taifa wakiimba na kushangilia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo imeifanya timu hiyo kushika usukani wa ligi kuu, lakini ni neno moja tu ndilo linaloweza kutumika kuonyesha Wekundu walivyonoga: Kudaaaadeki.
Raha ya ushindi wa jana, ilitokana na ukweli kwamba Simba imeipiku Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi huku ikionyesha kiwango bora dakika za mwisho, baadhi ya mashabiki wa Simba waliisikika wakiikebehi Yanga kwa kuimba: “Pisha njia, pisha njia.”
Inawezekana ikaonekana ni ushindi wa kawaida lakini soka la ushindani lililoonyeshwa na timu zote katika mchezo huo lilisababisha mchezo huo uwe mzuri, lakini bao la pili lililofungwa na Ibrahim Ajib lilichangia kuongeza furaha hiyo ya Wanamsimbazi.

Ajib alifunga bao hilo baada ya kuwakokota mabeki wa Mbeya City kisha kuwahadaa kama anapiga na kuwapangua kisha kupiga mpira katika ‘engo’ ya pembeni ambao ulimpita kipa wa Mbeya City, Hannington Kalyesebula na mabeki wake na kujaa wavuni.
Kuingia kwa bao hilo ndiyo hasa kulikonogesha ushindi huo kwa kuwa ilikuwa ni katika dakika ya 90, hivyo mashabiki kulipuka kwa furaha huku Ajib akishindwa kukimbia kushangilia na kuamua kubaki ndani ya nyavu za lango la wapinzani wake akishangilia.
Ajib pia alifanya kazi nzuri katika bao la kwanza ambapo alimpiga chenga beki wa Mbeya City, Hassan Mwasapili kisha akatoa pasi kwa Awadh Juma ambaye alipiga shuti kali likapanguliwa na Hannington Kalyesebula hapo ndipo Danny Lyanga katumia fursa kuutupia mpira wavuni kiulaini dakika ya 75.

Mabao hayo yalikuwa baada ya matokeo kuwa 0-0 hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika ambapo kulikuwa na upinzani mkali huku Mbeya City wakionekana kuwa sawa kifiziki lakini walishindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata.
Kutokana na matokeo hayo, Simba sasa imeshika usukani wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 48 katika michezo 21 ikiziacha Yanga na Azam zinafuatia zote zikiwa na pointi 47 kila moja, lakini Simba ipo mbele kwa michezo ambapo imecheza mechi 21 huku Yanga na Azam zikiwa zimeshuka dimbani mara 20 kila moja.
Mbeya City ambayo inanolewa na Kocha Kinnah Phiri imeendelea kubaki na pointi 21 katika michezo 21 iliyocheza ikiwa imebaki katika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo.

Kikosi cha Simba kilichoanza katika mchezo wa jana: Vincent Angban, Emiry Nimubona, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajib na Brian Majwega.
Simba ilifanya mabadiliko katika mchezo huo kwa kuwatoa Brian Majwega, Nimubona na Hamis Kiiza kisha nafasi zao kuchukuliwa na Danny Lyanga, Awadhi Juma na Hassan Kessy ambaye aliongeza uhai katika kuamsha mashambulizi ya timu yake.
Hii ni mara ya kwanza Simba kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, baada ya mchezo, kocha Jackson Mayanja alisema: “Ninachojivunia ni kuiongoza Simba kuifunga timu hii kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huu.” Kocha Wa City, Kinnah Phiri, alisema kwa ufupi: “Hatukuwa na bahati.”

Leave A Reply