The House of Favourite Newspapers

KUKAA NUSU UTUPU WAACHIE KINA GIGY

Makala: Sifael Paul KIPINDI cha miaka ya nyuma uliibuka mtindo fulani wa baadhi ya wanamuziki wa kike waliokuwa wanachipukia nchini Marekani. Wasanii hao walipenda kuwatoa udenda wanaume kwa kuacha wazi matiti yao ili kupata watu wa kuwafuatilia.

 

Miaka kadhaa baadaye, mtindo huo uliigwa na baadhi ya mabinti wasanii wanaochipukia wa Bongo ambao nao walianza ‘kubusti’ na kuyaacha matiti yao wazi.

 

Namna walivyokuwa wanayaacha matiti yao nje huku yakiwa yametuna kama machungwa au maembe bolibo ilionekana ni fasheni mpya, lakini wao wakaongezea na kukaa nusu utupu.

 

Wao kuonesha nguo ya ndani wala hawaoni aibu kabisa, bila kujali kwamba nguo ya ndani ni siri ya mtu. Nguo ya ndani hasa ya mwanamke ni jambo nyeti na halipaswi kufanywa maonesho. Ndiyo maana wengine huita kufuli au mfuniko wa asali.

 

Kizazi hiki kilipewa jina la wasanii wanaochipukia wasiokuwa na maadili. Waliofyatuka! Naomba nitumie neno wasiojielewa. Hawa waliamini kukaa utupu kunatosha kuwapa umaarufu bila kujali ubora wa kazi zao za sanaa.

 

Hawa wapo wengi kutoka Bongo Muvi hadi Bongo Fleva kama Gigy Money, Amber Lulu, Sanchi na wenzao wengi.

 

Kuna baadhi ya watu huamini kuwa usupastaa wa hapa duniani, kuna uwezekano mkubwa wa shetani kuhusika. Weka kituo hapo!

 

Judith Wambura Mbibo almaarufu Lady Jaydee au Jide ni mmoja wa mwanamuziki walioiweka Bongo Fleva kwenye ramani kwa kuijengea njia na sasa inaajiri watu wengi wa kada mbalimbali. Hongera zake.

 

Kwa asiyemfahamu vizuri, Jide ni mzaliwa wa mkoani Shinyanga nchini Tanzania. Amezaliwa Juni 15, 1979. Mwaka huu anatimiza umri wa miaka 40. Amekula chumvi!

Jide amejitanabaisha kama mwimbaji wa R&B, Zouk na Afro- Pop. Ana takriban albam saba na mwaka huu nimemsikia akisema yupo kwenye maandalizi ya albam ya nane. Amewahi kushinda tuzo kibao za Msanii Bora wa Kike wa Bongo Fleva za ndani na nje ya nchi. Huyu ndiye Malkia wa Bongo Fleva.

 

Niseme wazi kwamba nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa kazi ambazo zinazofanywa na Jide ambaye amejijengea heshima kubwa tangu miaka ya 2000 alipoanza kusikika redioni na kuonekana runingani. Niseme kweli, Jide si malaika, lakini sikuwahi kumuona akifanya mambo ya ajabuajabu.

 

Ndiyo maana nilipata mshtuko nilipoona picha zake zilizomuonesha maungo yake nyeti alizoziachia mtandaoni.

 

Majibu ya watazamaji yalikuwa mepesimepesi na hata mimi nilifi kiria kiwepesi kuwa alikuwa anaandaa kazi mpya kwani umekuwa ni utamaduni wa wasanii wa kizazi hiki!

 

Lakini nilijiuliza, hivi hata Jide anaweza kutafuta kiki kwa staili hii ya kukaa nusu utupu akionesha maumbile yake nyeti?

Ili iweje?

Kwa nini asiwaachie kina Gigy Money staili yao hiyo?

Wapo mashabiki wanaoeleza hisia zao waziwazi kuwa amewasikitisha mno kwani hawakutarajia kuona jambo kama hilo likifanywa na mtu kama yeye. Wanaamini kwamba kuna levo ambayo ukishavuka na ukawa na heshima mbele ya jamii ni vizuri kujitafakari mno unapotaka kufanya kitu chochote.

 

Jide kama hajui kuna wazazi waliowakataza watoto wao kuingia kwenye muziki kwa kuona ni uhuni, lakini walipomtazama yeye na heshima aliyoiweka, waliamua kuwaruhusu kujiingiza kwenye muziki. Mfano gani anawapa wadogo zake? Tutawakanya wadogo zake kwa mfano upi tena? Inasikitisha!

 

Jide anapaswa kujua ana heshima kubwa mbele ya jamii kama mwanamuziki mkongwe. Anapaswa kutunza heshima hii kama walivyofanya wenzake, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Joseph Haule Profesa Jay.

Mwili wa Aliyegundua Tanzanite Ukiswaliwa Msikitini

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.