The House of Favourite Newspapers

Kukosana Mkosanie Chumbani Mitandaoni Inahuu?

Tausi Mdegela mwandishi wa makala hii.

Na TAUSI MDEGELA| GAZETI LA AMANI| SINDANO ZA MASTAA

PENZI msomaji wa Sindano za Mastaa, wiki iliyopita ulikuwa na staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper. Wiki hii tunakukutanisha na mwigizaji wa Bongo Muvi hasa kwenye upande wa vichekesho, Tausi Mdegela, ungana naye.

Hakuna sababu ya kukuchelewesha sana maana najua u mzima wa afya. Moja kwa moja nachomoa sindano yangu na ninakudunga wewe na mpenzi, mchumba au wanandoa ambao mmekuwa mkikorofishana chumbani halafu mnaenda kubwaga mambo yenu kwenye mitandao ya kijamii.

Kugombana, kukosana, mkosanie chumbani, leo hii unaenda kumwaga kila kitu mitandaoni. Hivi hii inahusu jamani? Au ni ushamba? Au ni mapokeo mabaya ya hii mitandao ya kijamii? Kila kunapokucha na kuchwa ni muhimu mno kama utapata nafasi ya kumshukuru Mungu kwa kila hatua anayokupitisha.

Yapo mengi sana mabaya ambayo hukuepusha bila wewe kujua. Kuna ajali. Kuna magonjwa, shida na changamoto nyingine nyingi ambazo wewe kwa macho ya nyama huwezi kuziona.

Japokuwa nimeanza bila kutambulisha mada yangu lakini ni mada inayohusu baadhi ya wapenzi, wachumba au wanandoa ambao wamekuwa wakikosania chumbani lakini cha ajabu matatizo yao wanayatoa sebuleni na kama hiyo haitoshi, wanaamua kuyaanika hata mitandaoni.

Hivi kweli inaingia akilini, mmekosania chumbani, mitandaoni kunahuu? Huu ni ujinga, hufai kuwa mwanamke au mwanaume wa mwanamke mwerevu, hufai kuitwa baba bora au mama bora wa mfano wa kuigwa.

Wazazi wako waliweza kudumu kwenye uhusiano wao kwa sababu ya kuwa na simile, uvumilivu, moyo wa jiwe, kifua kipana cha kutunza na kuficha mambo ambayo waliamini kama kila mtu atayajua, basi yatapunguza ladha na heshima ya penzi au ndoa yao. Lakini kwako, wewe uliye katika zama za kizazi cha Facebook, WhatsApp, Instagram, Twitter na mitandao mingine, huna cha siri, huna cha simile, huna uvumilivu, huna subira, huna hekima, unapozinguana na mwenza wako chumbani, basi shemeji na wifi zako sebuleni watajua tu.

Kama hiyo haitoshi, baada ya saa kadhaa hata watu uliosoma nao watafahamu kwa sababu uliamua kuposti kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo halikusaidii. Hukatazwi kuposti mitandaoni lakini ni vyema ukaposti kitu kwa lengo la kukusaidia au kupata mbadala, siyo kuposti kwa kuhisi unamkomoa au kumuaibisha mwenza wako, hii si sawa, unakosea, kama ulihisi ukiposti kwenye Instagram basi utakuwa umemdhalilisha au umemkomoa mpenzi, mchumba, mkeo au mumeo, basi huna akili. Huna akili kwa sababu umejidhalilisha mwenyewe.

Tumia vyema mitandao ya kijamii kwa kujifunza namna ya kuepuka mambo maovu yanayoizunguka dunia, kwa maana kuna jambo hulifahamu ila kupitia kundi au mtandao uliopo unapata elimu.

Kuna vitu vidogo unaweza kuposti lakini mwisho wa siku vitakuletea madhara kwenye familia au penzi lako. Yapo mambo mengi ya maana ya kuposti lakini si mambo ya faragha, huo ni ulimbukeni wa mitandao ni matumizi mabaya ya teknolojia. Bila shaka kwa mwenye tabia hiyo, utakuwa umepata jambo.

Kama ni wa kujifunza utaacha. Kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Amani, Insta:@mimi_na_ uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba: 0679979785.

Comments are closed.