The House of Favourite Newspapers

Kumbuka Matatizo Huzalisha Mapenzi Mapya

GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| XXLOVE

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kunifikisha Mwezi Februari ambao ni kumbukumbu yangu ya kuzaliwa. Pia niwatakie heri ya siku ya kuzaliwa wasomaji wote ambao wamezaliwa mwezi mmoja na mimi.

Mungu awatangulie katika maisha yenu ya kila siku, hekima, busara na utii akujalie ili kufikia ndoto zako.

Niwashukuru wote walioguswa na mada ya wiki iliyopita na leo mada yangu inakuonya na kukufundisha kuwa matatizo ndani ya uhusiano wako ya mara kwa mara husababisha kuzaliwa penzi jipya kwa mweza wako kama hatakuwa mvumilivu na mwenye hekima.

Ni kweli matatizo hayakwepeki katika maisha ya kila siku ya binadamu ila matatizo yakiwa ni yaleyale ya mara kwa mara na mhusika ni yuleyule, hii sasa ni kero, ni karaha, kama ni mwenza wako basi unamfanya ajue kuwa hiyo ndiyo tabia yako halisi.

Huyo mwenye hilo au hayo matatizo ndiyo wewe. Watu wengi wamekuwa wakizua matatizo kila kukicha kwenye uhusiano wao wa kimapenzi na kusahau kuwa matatizo hayo yanaweza kusababisha mwenza wake akazalisha penzi lingine jipya nje ya uhusiano wao. Jambo hili unaweza kuliona ni la kawaida, lakini huo ndiyo ukweli, kama wewe umekuwa kwenye matatizo na mpenzi, mchumba, mkeo au mumeo unaweza kusababisha mpenzi wako kuhamishia mapenzi kwa mtu mwingine. Ikitokea mwenza wako akapata nafasi ya kupetiwapetiwa na mchepuko au kuhisi tu kuwa anaweza kupata faraja badala ya zile dhoruba anazozipata kwako basi ujue kuwa hapo umetengeneza usaliti wewe mwenyewe.

Simaanishi sasa wale wapenzi au wanandoa wenye matatizo basi ndiyo msalitiane ila hii nawapa kama tahadhari kuwa matatizo ya kila siku na ya mara kwa mara si mazuri kwenye uhusiano wenu. Haiwezekani kila siku uhusiano wenu unakuwa umetawaliwa na matatizo ya kulumbana, kukwaruzana, kupigana na aina nyingine ya matatizo ambayo ni hatari kwa afya ya ustawi wa maisha yenu.

Jaribu kujichunguza na kubadilisha mwenendo mzima wa maisha ya kila siku ya uhusiano wako na mpenzi, mchumba, mkeo au mumeo kwani unaweza kujikuta unatoa nafasi kwa mtu mwingine kuliingilia penzi lako. Bila shaka hakuna mtu anayependa penzi au utamu wake ugawanywe kwa mwingine kama wewe ni mmoja wa wale ambao hawapendi utamu wako aupate mtu mwingine, basi badilika, tengeneza mazingira ya amani, upendo, uelewano na mazungumzo ya mara kwa mara ya namna ya kusahihisha inapotokea kukosana na mpenzi wako, jitahidi kuepuka migongano isiyokuwa na maana. Kuwa mtu wa tahadhari ili usisababishe kukwazika au kumkwaza umpendaye, ukifanya hivyo mtaishi kwa amani na upendo kwenye uhusiano wenu.

Pamoja na kuwa makwazo, gubu na changamoto za mapenzi ni ngumu kuziepuka lakini jitahidi kuziepuka kwa kukwepa migongano ya kusababisha, kuhisi na kufikiria. Hii itakusaidia kuendelea kudumu kwenye uhusiano wako.

Mara nyingine kama utakuwa ni mtu wa kumkwaza mwenzi wako basi unatengeneza wigo mpana wa kukaribisha maadui au michepuko kwenye himaya yenu na hii ni kwa mwanaume au mwanamke, maana mwenzi wako alitegemea anapokuwa na msongo umfariji lakini imekuwa ngumu kila akionana uso kwa uso na wewe ni matusi, maneno makali, ngumi, mateke na mitama, hilo ni tatizo, atakuja kukutoroka au kuchukuliwa na jamaa mwingine au mrembo ambaye hutaamini kwa muonekano wake na wako, hapo ndipo utakaposhangaa mpenzi wako alikosa nini kwako na kuhamia kwingine ilihali alipata kila kitu isipokuwa amani, upendo na furaha ndani ya nyumba.

Fanya marejeo kwenye uhusiano wako ili kudumisha na kuboresha uhusiano wako, kuepuka kunyang’anywa tonge mdomoni.

Comments are closed.