The House of Favourite Newspapers

Kunaumuhimu wa Kuwa ‘Vipofu’ Kwenye Uhusiano

0

 

KUNA Ni Jumatatu nyingine Mungu ametupa zawadi ya uhai. Tunakutana kwenye safu yetu hii mahususi kwa ajili ya kupeana elimu juu ya masuala mbalimbali ya uhusiano na maisha kwa ujumla.

Ni muhimu sana kujifunza kwa sababu si kila mwanadamu anajua kila kitu. Kuna mambo unaweza kuwa huyajui, lakini kupitia safu hii unaweza kupata elimu na kubadilisha mfumo mzima wa maisha yako hususan ya uhusiano.

Nimekuwa nikipata kesi nyingi za masuala ya uhusiano, halafu ukiuliza kisa unakuta ni kitu kidogo sana, mathalan mtu anakuwa bize sana na simu, uongo au ulevi. Ukimuelekeza mambo machache tu ya kufanya, ndani ya wiki kadhaa tu anakwambia tatizo lake limekwisha.

Basi moja kwa moja twende kwenye darasa letu la leo. Kwenye maisha ya uhusiano kuna kelele nyingi mno. Kila mtu anasema lake, usipipokuwa makini, unaweza kujikuta umepoteza dira nzima ya uelekeo wa maisha yako.

Kuna ambao watakwambia mume au mke mzuri ana tabia fulani. Utaambiwa pengine mwanaume au mwanamke wa aina fulani hafai. Hata mtu uliyenaye, wanaweza kukwambia hafai, tena wanakupa na ‘fact’ zao kuonesha kwamba wanachozungumza wanakimaanisha.

Kuna wengine watakwambia achana na fulani, halafu uwe na fulani kwa sababu huyo fulani mnaendana. Wanakupa vigezo vyao. Wanakupa faida za huyo mtu mpya ambazo ukilinganisha na huyo uliyenaye unaona kama kweli unapoteza muda.

Unatamani maendeleo ya haraka. Unaoneshwa maendeleo yalipo ambayo yanapatikana ndani ya muda mfupi, unajikuta umeingia kwenye laini mwenyewe. Baadaye unaweza kujikuta umeingia kwenye mikono ambayo si salama, utajuta!

Ndugu zangu, siyo wote wanaokupigia hizi kelele kwenye uhusiano wanakuwa na nia njema. Wengi wao wanafanya kutokana na utashi au fikra zao binafsi. Wanaweza kukuharibia au kukujengea. Hivyo ndiyo maana nasema, mapenzi yanahitaji upofu.

Unapojiridhisha kwamba upo sehemu salama, weka msimamo. Shikilia hapohapo mpaka kieleweke. Usiwe mtu wa kushikiliwa akili. Mwenzako naye anatakiwa kupata elimu hii. Hivyo ukisoma hapa, mueleweshe na yeye.

Kuweni ninyi kama ninyi kwenye uhusiano wenu. Msiwe watu wa kupelekwapelekwa na anasa za dunia au watu wengine. Mkishaamini kwamba kwa pamoja mnapendana, basi shikilieni pendo lenu. Mlitunze kwa gharama yoyote.

Iwe ni kwa shida au kwa raha ninyi msimame imara. Jiwekeeni mikakati yenu ya maisha ambayo mnataka kuyafikia. Mkipata mshukuru na hata mkikosa pia furahieni maisha yenu.

Hakuna kitu kizuri maishani kama kuridhika. Wanaoridhika wanasonga mbele. Wanaishi miaka mingi kwa sababu tamaa kwao ni mwiko. Wanaishi maisha yao. Huo ndiyo upofu wa kwenye uhusiano ninaouzungumzia. Nikuache na msemo huu wa Kingereza;

“Love needs to be ‘blind’ for survival. It does not seem to matter what others say to a new lover —he or she is always perfect in our eyes. This blindness is critical for us to move forward in our relationship and is usually required to move onto the ‘attachment stage’ as scientists call it so that they can stay in love long enough to have and raise children; in other words, to populate the earth!”

Kwa tafsiri isiyo rasmi; mapenzi yanahitaji upofu ili yachanue. Haijalishi watu watasema nini kuhusu mpenzi wako mpya, lakini wewe pekee ndiye unayeamini anakufaa. Upofu unasaidia kusonga mbele kwenye uhusiano, unakupeleka kwenye hatua ya kushikamana.

Mnakuwa kwenye mapenzi ya muda mrefu na kupata watoto na kwa maneno mengine, mnaijaza dunia.

Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii; Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Erick Evarist

Love

SIMU:0768 811 595

Leave A Reply