The House of Favourite Newspapers

Kurejea kwa Lissu TZ, Polisi Yatoa Neno

JESHI la polisi nchini limetoa neno la kumuondolea hofu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kuwa anaweza kurejea nyumbani wakati wowote kwa kuwa nchi ina amani, utulivu na usalama kwa watu wote waliomo ndani na wanaoingia nchini.

 

Aidha, limemtaka mwanasheria huyo kutoa taarifa kwa kile alichodai kuwa kuna taarifa amezipata katika mitandao ya kijamii kuwa usalama wake pindi atakaporejea nchini bado unatia shaka.

 

Kauli hiyo ya Jeshi la polisi imekuja wiki moja baada ya Lissu ambaye alinusurika kuuawa miaka miwili iliyopita na kwenda Ubelgiji kwa matibabu, kusema amesitisha mpango wake wa kurudi nchini kwa sababu za kiusalama.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Msemaji wa Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), David Misime alisema hakuna hofu yoyote ya kiusalama kwa mtu yeyote.

 

“Ninachoweza kusema ni kwamba nchi yetu ni ya amani, utulivu na usalama kwa watu wote, waliomo ndani na wanaoingia. Hatuna hofu yoyote ya kiusalama kwa mtu yeyote yule. Mtu akisema ana hofu na maisha yake aje polisi atuambia ana hofu gani na kitu gani.

 

“Sisi tutachunguza… atupatie hiyo taarifa atuambie anaona hiyo hofu dhidi yake; kuna kitu kinachomtishia maisha yake, sisi tunajua watu wote. Kwa mujibu wa sheria nchi yetu iko salama ni ya amani, utulivu na usalama kwa wananchi waliopo ndani ya Tanzania na wanaoingia,’ alisisitiza Misime.

 

Lissu ambaye pia alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki, kabla ya nafasi yake kutenguliwa na Spika Job Ndugai na baadaye Tume ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza Miraji Mtaturu kuwa mshindi katika jimbo hilo, alitarajiwa kurejea nchini Septemba 7, mwaka huu.

 

Akihojiwa na Kituo cha VOA Swahili huko Washington Marekani, Lissu alisema kuna matamshi ambayo yamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumtishia, hivyo kilichobaki kwa sasa ni viongozi wenzake waliopo Tanzania wamuhakikishie kuwa Tanzania ni salama.

 

“Mazingira ya kiusalama si mazuri, wale walionipiga risasi 16 mchana kweupe katika nyumba za Serikali bado wanaitwa wasiojulikana. Pia kuna maneno yanajitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuwa ngoja aje safari hii hatutakosea shabaha. Mfano Musiba ametamka hadharani,” alisema Lissu

Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa silaha na watu wasiojulikana nje ya makazi yake Dodoma.

STORI: Gabriel Mushi, Risasi Jumamosi

Comments are closed.