The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Unataka kusema mchungaji wangu anayetumia damu ya Bwana Yesu kuokoa, maono yake si ya kweli?”

Niliwaona wale wanawake wakipepesuka, mikono wakaikinga kama wanaokwepa joto la moto uliokokwa.ENDELEA MWENYEWE SASA…

“Si ya kweli mke wangu. Nadhani tuachie hapo,” nilimwambia kwa sauti iliyojaa amri na ukali kidogo.
Mke wangu alitulia, wale wanawake walipotea ghafla kisha wakarudi tena.
“Mkeo anataka kutufanya nini sisi? Hajui kwamba tunaweza kumtoa roho kabisa?” walisema kwa pamoja.

Mke wangu akaangalia juu tena na kusema:
“Jamani huu upepo huu sasa. Si unaweza kuezua paa la nyumba!”
Mimi ndiyo nilikuwa najua kwamba, sauti za wale wanawake ndizo zilisababisha kutikisika kwa paa la nyumba.

“Jamani msameheni ni mke wangu,” nilisema.
“He! Mume wangu yaani paa linayumba kwa upepo mkali hivi halafu wewe unaimba,” aliniambia mke wangu.

Ina maana kwamba, wakati mimi nawaambia wale wanawake hivyo, mke wangu aliona mimi naimba.
Basi, wale wanawake waliniaga wakapotea machoni pangu huku wakiahidi kurudi usiku kwa ajili ya kazi maalum.
***
Ilikuwa usiku wa saa sita, nilichelewa kulala siku hiyo lakini nilikuwa nimejilaza tu kitandani nikiangalia paa, nikahisi joto kali sana na ukichukulia Mkoa wa Iringa ni wenye baridi kali, kumbe ni wale wanawake wanakuja, wakaonekana ghafla chumbani kwangu.

Walisimama ukutani wakinitazama kwa macho makavu. Mmoja wao akaniita kwa ishara ya mkono. Niliinuka kitandani, nikashusha miguu na kutembea hadi walipo.

Mmoja wao akaniwekea mkono kichwani, akaugandisha kwa muda wa kama dakika tano nzima bila kusema lolote. Niliusikia mwili ukiwa wa baridi sana, kuanzia utosini hadi miguuni.

“Utatoka hapa sasa hivi, utatembea hadi nje, ukifika huko utapewa maelekezo mengine, sawa?”
“Sawa,” nilijibu bila kuuliza, wakapotea.
Nilirudi kitandani nikakaa. Nikaanza kujiuliza kama lile tukio nilikuwa naota au ni kweli.

“Unapoteza muda kufikiri, toka ukafanye kazi,” sauti ilisikika ndani ya chumba bila kumwona msemaji.

Nilisimama kama niliyepigwa shoti ya umeme, nikiwa kwenye mavazi ya kulalia tu, nikatoka hadi nje. Wakati nafungua milango, yaani wa chumbani kwenda sebuleni na wa sebuleni kutoka nje, nilikuwa natumia nguvu kubwa sana na kuibamiza.
Nje, nilikuta kundi la watu wamesimama kwa mbele kama waliokuwa wakinisubiri mimi.

Walinifuata, wakanishika mkono na kugeuka, tukatembea kuelekea barabara kuu. Kule, tukakutana na wengine kama wao.

Nao wakanishika mkono. Cha ajabu ni kwamba, wakati wananishika, mwili wangu ulikuwa ukiingia baridi sana. halafu sijui walitumia maarifa gani kunishika kwani waliweza kunishika wote japokuwa walikuwa wengi.

Tulikwenda mpaka kwenye ofisi za posta ambazo zipo eneo la bustani ya halmashauri ya mji. Tukasimama hapo. Mmoja wao akaniambia natakiwa kwenda hospitali ya mkoa ambako si mbali na ofisi hizo za posta.

Kule nilitakiwa kwenda kuchukua vivuli vya wagonjwa ambao bado wana nguvunguvu, yaani afya zao hazijatetereka sana.
“Una swali?” yule mmoja wao aliniuliza.
“Vivuli navichukuaje?” nilimuuliza.

“Kila mgonjwa unamshika kwa mkono wa kushoto. Kwa kufanya hivyo ndiyo maana ya kuchukua vivuli vyao. Wakati unaingia hakikisha unapofika tu mlangoni geuka na kuingia kinyumenyume huku unatembea kwa hatua ndefu. Una swali jingine?”
“Vina kazi gani hivyo vivuli?”

“Sisi huwa tunatengenezea dawa ya kujichubulia. Wanawake wengine wanapenda kujichubua, lakini asili ya zile dawa ni sisi na ndiyo tuliyoleta ufundi huu kwenu duniani.”
“Sawa.”

Niligeuka, nikatembea nikiwaacha wamesimama pale. Lakini wakati nakwenda moyoni nikawa najiuliza ni kwa nini nikachukue vivuli vya wagonjwa? Je, wagonjwa hao baada ya kuwachukua vivuli watakuwa katika hali gani wenyewe?

Nikakumbuka kwamba, swali hilo sikuwauliza, nikageuka ili kurudi kwanza pale ili nikawaulize, lakini ile nageuka tu, nikawaona wamesimama mbele yangu. Ina maana walitembea nyuma yangu.

“Kuna tatizo gani tena?” waliniuliza.
“Je, nikiishachukua hivyo vivuli, hao wenye vivuli au niseme wagonjwa, watakuwa katika hali gani kiafya?”

Walicheka sana, wakacheka wee na waliponyamaza walinyamaza wote. Wakaniangalia japokuwa ilikuwa usiku lakini niliwaona walivyonikazia macho.
“Hiyo sasa si kazi yako kujua. Baada ya kuchukua vivuli kazi yako itakuwa imeisha mara moja. Wewe nenda.”

Niligeuka na kutembea kwa masikitiko sana. nilijua nikishachukua vivuli, wahusika watakata roho palepale na ndiyo maana pia hawakutaka kuniambia.
Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.

Leave A Reply