The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-12

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Jamani nina swali muhimu sana kwenu ambalo limenijia baada ya kunisamehe.”
Yule msemaji wao wa tangu awali akaniambia kwa sauti yenye amri.
“Si unataka kuuliza kuhusu utakachopata kwa mambo yote haya?”
ENDELEA MWENYEWE…

“Ni kweli,” nilikiri huku nikianza kuogopa kwa maana kwamba kama wamejua bila kusema nini kitaendelea?
“Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unatenda sawasawa na matakwa yetu, hilo tu, basi.”

Nilikubali kwa kutumia ishara ya kichwa na shingo. Wakasema nikalale ila kwa usiku wa kesho yake nitatakiwa kufanya kazi moja ngumu sana lakini sitakuwa peke yangu, nitashirikiana na majini.

Niliwauliza ni kazi gani hiyo, wakasema kuna sherehe ya kuzaliwa kwa mtoto wa mmoja wao. Huyo mtoto ni wa mwanamke jini aliyezaa na mwanaume mtu. Lakini mtoto anaishi ujinini.

Hapa naomba niseme kidogo mwamba, wapo wanaume wengi tu wa duniani wamezaa na wanawake wa ujinini. Lakini pia kuna wanawake wa duniani wamezaa na wanaume wa ujinini.

Kinachotokea ni kwamba, unakuta mwanaume anatokea kumpenda msichana jini bila mwenyewe kujua kuwa yule ni jini. Anatembea naye kwa tendo la ndoa kisha hawaendelei na uhusiano.

Yule msichana kumbe ni jini na alijitokeza duniani kwa kutaka kuzaa na binadamu tu. Baada ya hapo anarudi ujinini kulea mimba yake mpaka anajifungua.
Na kwa msichana wa duniani vivyohivyo, anatongozwa na mwanaume, kumbe jini, wanakwenda hotelini na kukutana kwa tendo la ndoa. Baada ya hapo, mwanaume anarudi ujinini na msichana huku duniani anapata mimba, baba hajui aliko.

Basi, tuliachana hapo, nikarudi nyumbani kulala. Kesho yake niliamka nikiwa nina nguvu za ajabu. Mwili ulikuwa kama umepumzika kwa siku saba, kumbe wapi! Mwenyewe nilishangaa sana.

Siku ya pili, nilipotoka kazini jioni ya saa kumi na mbili, nilisikia sauti ikiniambia nisitoke kwenda popote baada ya kufika nyumbani kwangu na nilitakiwa kuoga na kujipaka mafuta ya mgando, maelekezo mengine ningepewa.

Nilifanya hivyo, baada ya kuoga nilijipaka mafuta ya mgando na kukaa sebuleni. Baada ya saa kadhaa, kwenye saa mbili usiku, upepo mkali sana ukavuma, nikajua wenyewe wanakuja.

“Hivi saa ni saa mbili na nusu, simama uondoke. Unasubiriwa nje kwa ajili ya kwenda kwenye sherehe,” sauti iliniambia, nikafikicha macho, hakukuwa na mtu.

Nilikuwa nimevaa, nikatoka nje na kuwakuta wanawake wawili ambao walinishika mikono, kila mmoja wa kwake. Kufumba na kufumbua tulikuwa tumekaa kwenye ukumbi mmoja maarufu sana hapa Iringa.

Wateja walikuwepo wakiendelea na mambo yao lakini baadhi ya meza hazikuwa na wateja. Pembeni kulikuwa na meza, walikaa watu kama kumi na kuendelea. Wale wanawake wakanipeleka kule na mimi nikajua ndiko kwenye sherehe.
Kweli, palikuwa na wanawake mchanganyiko na wanaume. Mwanamke mmoja alikuwa na mtoto kama wa miaka miwili hivi.

Meza ilipambwa na keki, mishumaa, vitambaa vyekundu, mabakuli, vikombe vya kuwaka kama almasi, mahotpoti na kadhalika. Lakini kwa pembeni yake chini palikuwa na seti ya muziki na DJ alisimama hapo.

Kwa haraka nilichobaini ni kwamba, wateja wengine ndani ya ukumbi ule walikuwa hawawaoni wale watu. Pia, kuna mtu katika wale watu alikuwa akitoka mara kwa mara na kwenda kusimama mbele ya meza na kunyoosha kidole mlango mkuu.

Awali sikujua ni kwa nini, baadaye nilibaini kwamba, mtu yule alikuwa maalum kwa kuwazuia wateja waliokuwa wakiingia na kuonesha dalili ya kuja kukaa tulipokuwepo sisi.

Nililigundua hilo baada ya wakati fulani kuwaona watu wawili, nadhani ni mke na mume wakiingia mlango mkubwa na kuja uelekeo wetu ambapo yule mtu alitoka kwenye meza na kwenda kusimama mbele halafu aliwanyooshea kidole kisha akawa anakipeleka kidole hicho usawa wa meza nyingine kabisa na wale watu nao walielekea huko mpaka kwenye meza nyingine, wakakaa. Yaani ilikuwa kama anawaelekeza.

Hapa kabla sijaendelea, nataka kuwapa wasomaji somo moja. Ni kwamba, kwenye mabaa na maeneo mengine wanayokutanika watu kuna mambo mengi ya ajabu ambayo hayaonekani.

Maandiko yanasema Mungu aliumba viumbe vinavyoonekana na visivyoonekana. Sasa ni mara nyingi tu, visivyoonekana vinapenda kukaa sehemu ambayo vinavyoonekana vipo.

Mfano kwenye baa, dalili kubwa kwamba viumbe vinavyoonekana navyo vipo vimekaa kwenye viti ni wateja kukauka au kuingia na kupenda kukaa upande mmoja tu wa viti vya baa hiyo.

Utakuta baa nzuri sana, lakini viti vitupu muda mwingi. Lakini ukweli ni kwamba, hapo si kwamba wateja hawataki kuingia bali kuna majini nayo yanapenda kukaa kwenye baa hiyo wakifanya mambo yao.

Je, nini kiliendelea? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo katika gazeti hilihili.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply