The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-14

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Baada ya kukataliwa na mwanaume aitwaye Edson, mwanamke bilionea, Elizabeth Marcel anapokea simu na kuambiwa aende nchini Morocco kwa ajili ya kuzindua mavazi yake. Hakatai, japokuwa aliyemuita hamfahamu, anaelekea huko.
SONGA NAYO…

Safari ikaanza, Elizabeth alikuwa na hamu kubwa ya kumfahamu huyo Rasheed, kitu kilichojijenga akilini mwake ni kwamba alikuwa mmoja wa watu wenye fedha nyingi kitu kilichomchanganya kabisa. Alimuuliza dereva kuhusu huyo Rasheed lakini hakumwambia alikuwa nani.

Alijua kwamba dereva yule alikuwa na mambo mengi ambayo angeweza kumwambia kuhusu Rasheed lakini alikuwa akimficha, alichokifanya ni kuendelea kumwambia kwamba alihitaji kumfahamu huyo Rasheed mwenyewe kwani alihisi moyo wake kuwa na kiu kubwa.

“Utamjua tu,” hilo ndilo jibu alilopewa kila wakati alipokuwa akiuliza.
Safari iliendelea mpaka walipofika katika mtaa uliokuwa na majumba mengi ya kifahari, kwa kuuangalia tu wala usingesumbuka kujiuliza juu ya watu waliokuwa wakiishi ndani ya mtaa huo, walikuwa ni watu wenye fedha kwani hata magari waliyokuwa wakipishana nayo yalikuwa ni ya kifahari mno.

Gari lile likaenda kusimama nje ya geti moja kubwa, ndani yake kulikuwa na jumba kubwa la kifahari. Alichokifanya dereva yule ni kuchukua rimoti kisha kuibonyeza kwa kuielekezea katika geti lile, hapohapo likajifungua kisha kuliingiza gari lile.

Mazingira aliyoyakuta ndani ya eneo la jumba hilo la kifahari yalimshangaza, kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, bustani kubwa ya maua, magari ya kifahari zaidi ya lile alilokuwa amepokelewa nalo, kila kitu alichokiangalia ndani ya eneo la jumba lile la kifahari, alibaki akishangaa tu.

“Tumefika!” alisema dereva yule na wote kuteremka.
Wakaingia mpaka ndani ya jumba lile, kila kitu alichokiona, Elizabeth alibaki akishangaa tu. Vyombo vingi vilivyokuwa ndani ya jumba hilo vilinakshiwa kwa dhahabu, kwa muonekano aliokuwa ameukuta, ulimwambia kwamba mwanaume aliyekuwa akiishi humo alikuwa mtu mwenye fedha nyingi mno.

“Karibu sana. Ngoja nikaendelee na majukumu,” alisema dereva yule.
“Sasa mbona unaniacha! Huyo Rasheed yupo wapi?” aliuliza Elizabeth.
“Anakuja. Wala usijali.”
“Sawa!”

Akabaki sebuleni pale peke yake, macho hayakutulia, alikuwa akiangalia huku na kule, kila kitu alichokiona kilikuwa kigeni machoni mwake. Alikuwa mwanamke bilionea, aliyeogelea sana fedha lakini kile alichokutana nacho kilimshangaza mno.

Wala hazikupita dakika nyingi, mara mwanaume fulani akatokea sebuleni hapo. Alikuwa Mwarabu, aliyevalia kanzu ndefu, usoni hakuwa kama watu wengine, hakuwa na ndevu hata moja, nywele zake alizinyoa kwa staili ya kiduku kwa mbali, alivalia miwani, alipofika mahali hapo, akavua miwani na kubaki akiangaliana na Elizabeth.

Elizabeth akashtuka, aliwahi kusikia stori nyingi kuhusu malaika kwamba vilikuwa viumbe vizuri mno huku akimuomba sana Mungu japo naye akutane na malaika hao ili kuona walikuwa wazuri namna gani.

Siku hiyo alihisi kwamba Mungu alijibu maombi yake, mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa mzuri mno. Alipomwangalia, moyo wake ukaanza kudunda kwa nguvu, hakuamini kama duniani kulikuwa na mwanaume mzuri kama alivyokuwa yule Mwarabu aliyekuja sebuleni pale, akajikuta akianza kutoa tabasamu pana.

“Karibu sana Elizabeth! Mimi ndiye niliyewasiliana nawe jana,” alisema mwanaume huyo, Elizabeth akazidi kutabasamu.

“Ni furaha yangu kukutana nawe,” alisema Elizabeth kwa sauti nzuri ambayo hakuwahi kuitumia kumwambia mwanaume yeyote yule, tayari moyo wake ukaanza kufa na kuoza, alitamani japo mwanaume yule amwambie tu kwamba alikuwa akimpenda. Hakika alimhitaji, alikuwa mzuri hata zaidi ya Edson. Mwanaume huyo alikuwa Rasheed.

Ili kuonesha heshima, Elizabeth akasimama na kumsalimia zaidi kwa kumpa mkono. Waliposhikana, Elizabeth akahisi kitu kama shoti ya umeme kikiupiga moyo wake, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, akabaki akiwa ameachia tabasamu tu. Hakika moyo wake uliburuzwa vilivyo.

“Nimetokea kukupenda Rasheed…” alijikuta akijisemea moyoni mwake, hata kukutanisha macho tena na Rasheed, akaona aibu, akajikuta akiangalia chini.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply