The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-8

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Aliposema hivyo tu nikalikumbuka hilo tukio. Niliwahi kupanda basi Kihesa kwenda Miyomboni. Ni kweli, kuna mama mmoja nilikaa naye akapiga chafya mara nyingi sana mpaka nikasikia kero, kidogo nimwambie.

Nikamjibu: Ni kweli, naikumbuka siku hiyo. Wewe umejuaje lakini?”
“Kwani unataka nikwambie mambo zaidi ya hapa?” aliniuliza huku akiwa amenitumbulia macho mpaka nikaanza kuogopa.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

“Ndiyo,” nilimjibu waziwazi.
“Nimejua kwa sababu yule mwanamke ni mimi.”
Nilishtuka, nikasimama na kuuendea mlango lakini cha ajabu, mkono wake pale alipokaa ukarefuka mpaka mlangoni ukafunga mlango kwa funguo kisha akasema:
“Sisi huwa hatukimbiwi hata siku moja. Tena usije ukajaribu kufanya hivyo siku nyingine hata kwa jini ambaye ni tofauti na mimi. Utapoteza maisha yako bure.”

Nilirudi kukaa pale kwenye kiti kama mwanzo. Nikamwona akibadilika sura laivu. Masikio yake yalianza kurefuka mpaka kufikia usawa wa masikio kama ya sungura.

Halafu macho yakaanza kuwa makubwa mpaka kufikia ukubwa wa kama ngumi ya binadamu mtu mzima. Juu, yaani kwenye paji la uso, kukachomoza mapembe mawili yakawa marefu kama ya ng’ombe. Nilikuwa katika kipindi kigumu na cha ajabu sana.

Nikiwa katika hofu hiyo, mara nikaanza kuona meno yake yanatoka kwenye kinywa kuja nje na kurefuka kiasi cha kuzidi urefu wa kidole cha katikati cha binadamu. Uso wake wote ulibadilika rangi, weupe uliisha, akawa mweusi au kama rangi ya kahawia.

Mpaka hapo alikuwa hajaanza kusema lolote zaidi ya kuwepo kwa mabadiliko hayo. Na alikuwa akibadilika huku akiniangalia na macho yake makali na ya kutisha sana.
“Hii ndiyo sura ya duniani, unabisha?” aliniuliza kwa sauti nzito sana.

“Sijakuelewa,” nilimwambia.
“Hivi nilivyo si ndivyo duniani mnavyojua sisi tupo hivi?”
“Ni kweli.”

Alicheka kwa sauti ya kama mtu mnene sana anapocheka kwa shidashida.
Kufumba na kufumbua akarejea katika hali yake ya kawaida kwamba akawa yuleyule msichana niliyekuwa naye awali. Akaachia tabasamu na kusema:
“Sisi hatuko vile. Kwanza kati ya sisi na nyie sisi ni wazuri sana. Uliwaona wale akina dada uliokaa nao sebuleni, kuna mbaya wa sura?”
Nilikataa kwa kutingisha kichwa. Akaniambia:

“Mnatukosea sana, kila kibaya mnakifananisha na majini. Ndiyo maana wakati mwingine tunaamua kuja kuishi hukohuko na majirani wanadamu na tunafanya nao kazi maofisini ili watujue kwamba hakuna jini mbaya.”

Ghafla mlango ulifunguliwa, akaingia mmoja kati ya wale wanawake wa awali, akanishika na kunitaka niondoke naye. Nilimfuata kwa nyuma, alipofunga mlango akasimama na kuniambia:

“Ulichokiona huku kitabaki kuwa cha huku hasahasa kama utarudi nyumbani kwako ukiwa hai.”

Niligunia moyoni na kubaini kwamba, kumbe kuna uwezekano wa kurudi nyumbani nikiwa siko hai kwa mujibu wa maneno yake.
Nilipobaini hilo tu, moyoni nikajiambia natakiwa kufanya juu chini kuhakikisha natoroka la sivyo hawa wataniua kweli.

Yule mwanamke akaendelea kusema: “Kuwa makini na kila agizo la huku, usitake kubisha wala usitake kutoroka. Sisi huwa hatutoroki kwa sababu tunaweza kujua hata mawazo yako hapo ulipo. Tunaweza kukuonesha hata familia yako ilivyo kwa sasa kule duniani kama utataka.”

Sikumjibu kitu, nikamfuata nyuma hadi kwenye mlango mwingine mkubwa sana kuliko yote kwa maana ya upana.
Mlango huo ulifunguka wenyewe, tukaingia.

Ndani ni ukumbi mkubwa sana lakini ukiwa umepambwa. Mbele kabisa palikuwa na meza kubwa kuna watu wamekaa kwa safu. Walikuwa watu kama kumi na zaidi.

Mimi na yule mwanamke tulisimama katikati ya ukumbi. Yule mwanamke akiwa mbele yangu akainama kwa ishara ya kusujudia au kama vile mtu anayetii kwa kiongozi au kwa mamlaka iliyo kuu zaidi yake, kisha akageuka kuniangalia. Kuona hivyo na mimi nikainama kidogo halafu nikasimama kawaida mikono nikiwa nimeifumbatia kwa chini mbele usawa wa fraizi ya suruali.

“Huyo kutoka wapi?” sauti nene na iliyojaa kitetemeshi ilisikika ikiuliza.
“Mkoa wa Iringa kiongozi,” alijibu yule mwanamke. Tena alijibu kwa sauti ye kunyenyekea sana.

“Kuna wilaya lakini,” ilisikika ile sauti. Kifupi sauti ile ilikuwa ikitoka kwa mmoja wa wale waliokaa kwenye meza kubwa mbele kabisa.
“Kuna wilaya kiongozi. Huyu ametokea Iringa Mjini.”

“Makazi?”
“Makazi yake ni Mlandege.”
“Haya! Ana taarifa na kazi?”
“Nimemwambia.”
“Akaonekanaje?”

“Kama anakubali, kama anabisha. Lakini nimeshamwambia madhara ya kukataa na faida za kukubali kwake.”

“Nenda kampangie kazi haraka sana na umjulishe na maeneo yake. Atakubali tu.”
“Nilishampangia kazi na maeneo yake kiongozi.”
“Kampe maji anywe na umwachie akaanze kazi mara moja. Lakini mpangie siku ya kuleta ripoti yake huku.”

Je, nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo.

Leave A Reply