The House of Favourite Newspapers

KWA DAWA HIZI, DIAMOND ‘HATARINI KUFA’!

DAR ES SALAAM: Kama ni kweli Staa wa Muziki wa kizazi kipya, Nasibu Abdul ‘Diamond’ anatumia vidonge vya kusisimua misuli kama inavyodaiwa na vyanzo vilivyo karibu naye basi yu hatari kufa, Amani linakupa habari kamili.

Chanzo makini kililiambia Amani kuwa, mwanamuziki huyo amekuwa akitumia dawa hizo za kutunisha misuli zinazojulikana kwa jina la ‘Doping’ kwa muda mrefu.

Kiliendelea kueleza kuwa, Diamond kutumia kwake dawa hizo ndiyo maana mwili wake unaonekana kujengeka na kuwa na misuli iliyotanuka licha ya kwamba wakati mwingine huwa anakondeana na kuwa na muonekano wa tofauti.

 

“Diamond anatumia dawa za kutanua misuli na akiacha kutumia ndiyo anaonekana kama mtu anayetumia madawa ya kulevya ‘teja.’

“Yaani ameshazizoea hizo dawa kwa kiwango ambacho akizikosa hata kwa wiki moja tu zinamfanya kupungua mwili,” chanzo cha karibu kilidai bila ya kuwa na uthibitisho wa uwepo wa matumizi hayo ya dawa hizo kwa Diamond.

 

MENEJA WAKE AFUNGUKA

Baada ya kupata habari hizo, Amani lilimtafuta meneja wa Diamond aitwaye Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambapo alifunguka kwamba siyo kweli msanii wake anatumia dawa bali anafanya mazoezi ya nguvu.

“Hahaha, leo naona umekuja na hili, Diamond asili yake ni mwembamba, asipofanya mazoezi ndiyo anakuwa mwembamba zaidi lakini akifanya anatanuka kama anavyoonekanaga.

 

“Siyo kweli kwamba akionekana kutanuka anakuwa ametumia dawa, kwa mfano mwaka huu toka mwezi wa kwanza hadi wa sita hakufanya mazoezi kabisa.

“Ndiyo maana alionekana kapungua, unakumbuka tulipokwenda Marekani huko alikula vizuri na kufanya mazoezi ya kutosha na muonekano wake ukawa ndiyo huo wa kutanuka,” alisema Babu Tale.

DAKTARI ANASEMAJE?

Akizungumza na gazeti hili daktari wa Hospitali ya Temeke, Godfrey Chale ‘Dk. Chale’ alieleza kuwa dawa hizo za kutunisha misuli siyo nzuri kwani zina madhara makubwa kwa mtumiaji japokuwa vijana wengi siku hizi wamekuwa wakizitumia.

“Vidonge vya kutunisha misuli na kuongeza nguvu ni hatari sana kwani zinasababisha magonjwa mengi hatari kwa mtumiaji ambayo yanaweza kumsababishia kifo cha haraka kabla ya muda wake,” alisema Dk. Chale.

 

MADHARA YAKE

Daktari huyo alieleza kwamba madhara yatokanayo na utumiaji wa vidonge hivyo ni pamoja na maradhi ya moyo, ini na figo kuharibika, wanaume kuwa na matiti kama wanawake, shinikizo la damu, saratani na magonjwa mengine mengi.

 

Hata hivyo daktari huyo aliwataka vijana kuachana na matumizi ya vidonge na kama wanataka kuwa na mwili na misuli iliyotanuka basi wafanye mazoezi ya kawaida ambayo hayana madhara kwenye maisha yao.

 

DIAMOND ASHAURIWA

“Kama ni kweli atakuwa anatumia dawa hizo atakuwa anajihatarishia maisha yake hasa kutokana na kazi yake, anaweza kufa ghafla hata jukwaani.

“Namshauri asitumie hizo dawa afanye mazoezi, pumzi anayoitaka na kutanuka mwili ataipata bila matumizi ya dawa hizo,” alisema Dk Chale.

 

NINI HASA SABABU YA KUTUMIA?

Wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa wanaume au vijana wengi wamekuwa wakitumia vidonge hivi kwa ajili ya kuwa na muonekano wa kitanashati kwani inadaiwa wanawake wengi wanapenda wanaume wenye muonekano huo.

Licha ya hilo pia wapo vijana wengine wanatumia kwa ajili ya kazi wanazofanya kama ubaunsa, uwanamichezo, uwanamuziki ili kuwasaidia wasiishiwe pumzi.

Comments are closed.