The House of Favourite Newspapers

KWA HAYA YAWEZEKANA KIBA ANAMCOPY DIAMOND

HAINA ubishi kwamba kwa asilimia 100 unaweza kusema kuwa Muziki wa Bongo Fleva umekuwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo kwa studio nyingi pamoja na wimbi la wasanii kuibuka na ngoma mpya na kali kila siku tofauti na mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambao muziki huu ulikuwa ukianza kupenya kwa taratibu Bongo huku wengine wakiudharau na kuuona wa kihuni.  

Lakini pia uwepo wa ushindani wa wasanii, Nasibu Abdul ‘Mondi’ na Ally Salehe Kiba ‘Kiba’ pamoja na mafanikio yao waliopata katika muziki umekuwa chachu kubwa kwa wasanii wengine kujiunga katika muziki huu.

Pamoja na kuwa chachu, wasanii hawa ndani na nje ya muziki wamekuwa wakifanya mambo yanayofanana kwa kiasi fulani na katika mambo hayo, mengi yanaonekana kuanzishwa na baada ya kipindi fulani Kiba naye anaibuka na ‘ku-copy’.

 

KOLABO ZA KIMATAIFA

Japokuwa Kiba ndiye aliyeanza kutoka kimuziki, lakini kolabo zake nyingi alizokuwa akifanya zilikuwa za ndani ya nchi, hakuwahi kumshirikisha staa wa kimataifa katika wimbo wake wowote.

Kolabo iliyokuwa ikimbeba ni ile ya One 8 alioshirikishwa na mkongwe wa R & B kutoka Marekani, Robert Sylvester ‘R Kelly’ akiwa na wasanii wengine wengi kama vile Amani, Fally Ipupa, Navio na 2 Face Idibia.

 

Baada ya Diamond kuanza kupata nafasi ya kufanya kolabo ya kwanza ya Number One Remix akiwa na msanii wa Nigeria, Davido na kumtoa kimataifa, Kiba naye akaanza kutoka hadi Kenya na kufanya kolabo ya Wimbo wa Unconditionally Bae akiwa na Kundi la Sauti Sol la Kenya na baadaye Nigeria kwa msanii M.I kupitia remix ya wimbo wake wa Aje.

VIDEO

Ukitazama asilimia kubwa ya nyimbo za Kiba, video zake zilikuwa zikifanywa na madairekta wa Kibongo wakati Mondi video zake zilikuwa zikifanyikia Afrika Kusini ‘Sauz’ au Nigeria chini ya Dairekta, Mike Ogoke ‘Godfather’. Video za Mdogo Mdogo, Kidogo, Utanipenda na Nana za Mondi ndizo zilioonesha uwezo mkubwa wa Godfather kwenye soko la video Bongo na baada ya kipindi kifupi Kiba naye akamuibukia Godfather na kutengeneza video yake ya Mwana ambayo ilitokea kukubalika.

 

KUANIKA WAPENZI

Kwa kipindi cha nyuma, Kiba alikuwa akifanya siri kuwaanika wapenzi anaotoka nao ambao ni mastaa lakini kwa Mondi kwake alikuwa akijiachia tu, mara Penny, Wema Sepetu na wengineo.

Baada ya kipindi, Kiba akaona naye isiwe kesi, akaanza kujitokeza hadharani na mtu aliyekuwa akitajwa kama mpenzi wake, Jokate Mwegelo ambao kapo yao ilikuwa ya kuongozana sehemu mbalimbali kwenye matukio, uwanja wa mpira na kwenye shoo za muziki.

MAJINA YA WANYAMA

Mondi baada ya kupata mafanikio makubwa katika Muziki wa Bongo Fleva, alianza kujiita a.k.a ya Simba akiwa na maana ya mnyama anayejulikana kama ni mfalme wa porini kwa hiyo yeye alijifananisha na mnyama huyo kutokana na kuona kuwa  hakuna msanii aliyekuwa akimshinda. Baada ya kipindi kifupi, Kiba akapata shavu la kuwa Balozi Wild Aid ambalo lilikuwa likipinga ujangili wa Tembo. Mara baada ya kuchukua ubalozi huo Kiba akaanza naye kujiita Tembo akimaanishi mnyama mwenye nguvu kuliko wote.

 

KUMILIKIWA NA LEBO

Alianza Mondi kupata shavu la kusainiwa lebo ya kimataifa inayosimamia muziki ya Universal Music Group (UMG). Katika lebo hiyo, Mondi alikuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kusainishwa na lebo hiyo na kazi ya kwanza kuitoa ilikuwa Marry You akimshirikisha mkali wa R&B kutoka Marekani, Ne-Yo.

Baada ya kipindi, Kiba naye akaingia Sauz na kusainiwa na Lebo ya Sony Music Entertainment ambayo inadili na kusimamia video zake na audio kwa kuzilipia na kuzifikisha kwenye masoko makubwa ya muziki duniani.

 

BIASHARA

Mbali na muziki, Mondi pia amekuwa mfanyabiashara ambapo alianza kwa kutengeneza mavazi yenye jina la lebo yake ya WCB na baada ya muda akaja na pafyumu aina ya Chibu kisha akazindua Diamond Karanga.

Kiba naye akaona siyo ishu, akajiingiza kwenye biashara na kuibuka na kinywaji cha Mofaya ambacho amekuwa akikitangaza sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye jezi za timu ya mpira wa miguu ya Coastal Union ya Tanga.

KUMILIKI WASANII

Alianza Mondi kwa kuanzisha Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na ndani yake akawasaini wasanii kadhaa kama vile Harmonize, Rayvanny, Queen Darleen na Mbosso. Katika lebo hiyo, Mondi amekuwa akishirikiana nao kwa ukaribu kwa kutoa nao nyimbo mbalimbali.

Wakati Mondi akiendelea na WCB, Kiba naye akaanzisha lebo yake ya King’s Music na kumiliki wasanii wake kwa mara ya kwanza ambao ni Killy, Cheed, K2ga na Abdu Kiba.

Comments are closed.