The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa 28

0

Abikanile anafariki wakati akijifungua, mtoto wake aliyepewa jina la Mtima kama yalivyokuwa maelekezo ya Abikanile kupitia barua aliyoiacha anachukuliwa na Mzee Johannes aliyekwenda kumlea kama mtoto wake wa kumzaa.

Siku zikasonga mbele hatimaye Mtima akaendelea kukua lakini akiwa na umri wa miaka 14 kuna jambo lilianza kuisumbua akili yake kiasi kwamba akajikuta anashuka kabisa kimasomo na kilichowashangaza zaidi wengi kila mara alihitaji kukaa peke yake tu!

SONGA NAYO…

“Mtima,”  Destiny alimuita wakiwa mapumziko.

“Nambie.”

“Una tatizo gani?”

“Sina tatizo lolote.”

“Mbona unaonekana mwenye mawazo mengi?”

“Ni kweli, nawaza hapo baadaye nitakuja kuwa nani!”

“Mh! Si kweli…”

“Niamini.”

Mtima hakupenda kabisa kuwa muwazi kwa kilichokuwa kinamsibu, kila aliyejaribu kumdadisi aliambulia majibu yasiyoridhisha.

Siku zikaendelea kukatika lakini pale uzalendo ulipomshinda kijana huyo aliamua kumueleza mama yake mdogo, Alile kile kilichokuwa kinamsibu.

“Nahitaji kuufahamu ukweli,” Mtima aliongea akionekana hana masihara.

“Ukweli upi?”

“Kuhusu wazazi na asili yangu.”

 “Babu yako si ameshakwambia?”

“Ndiyo, ila aliniambia uongo unaofanana na ukweli.”

Kauli ya Mtima ilimuumiza sana moyoni Alile, ni kweli alifahamu ilikuwa ni haki ya kijana huyo kuelezwa ukweli mzima kuhusu maisha ya wazazi wake, asili yao na hata kuonyeshwa barua iliyoachwa na Abikanile, lakini swali lililokuwa linamtatiza mwanamke huyo ni jinsi ambavyo Mtima angeupokea ukweli atakaoelezwa.

Alichoamua kufanya alimtaka Mtima kuwa mvumilivu, akamwambia ilikuwa ni lazima kumshirikisha babu yake juu ya jambo hilo, Mtima aliomba hilo lifanyike haraka sana kabla hajafanya maamuzi ambayo yangemshangaza kila mmoja.

****

Maisha katika familia ya Alile yalikuwa yamebadilika kwa kiasi kikubwa, tofauti na miaka kumi na tano iliyopita wakati ambao mama yake Chotsani alikuwa anajishughulisha na uuzaji wa samaki huku mzee Thambo, baba wa msichana huyo akikomaa na uvuvi huko Malawi,  maisha yalikuwa yamebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na mafanikio ya msichana huyo .

Alile alikuwa amewajengea nyumba kubwa wazazi wake ikiwa ni pamoja na kuwafungulia miradi tofautitofauti iliyocheua pesa nyingi huku jambo la muhimu alilolifanya aliajiri wasomi wenye elimu kubwa waliyoisimamia miradi hiyo kukua kila kukicha.

Akawa anaelekea kuzitimiza ndoto zake lakini kutokana na jeuri ya fedha alizokuwa nazo aliamua kushirikiana na Max Dean rafiki yake wa siku za nyuma ambaye alikuwa ni mumewe wakati huo, kuasisi taasisi nchini Malawi ya kusaidia na kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi iliyoitwa DICOPE Foundation (Different Colour One People).

Suala la Mtima kuhitaji kuufahamu ukweli lilizidi kuichanganya akili yake, akaamua kuwaeleza wazazi wake walezi bwana na bibi Johannes ambao pia walionekana kuchanganywa na jambo hilo, kwa kuwa Mtima alisisitiza juu ya kuhitaji kuufahamu ukweli wakapanga siku ya kumueleza.

“Inakubidi kuwa na roho ya kiume kukabiliana na ukweli.” Mzee Johanes alimwambia Mtima.

 “Sawa!”

Johannes aliamua kuitumia fursa hiyo kumuomba msamaha Mtima kwa niaba ya familia kutokana na kitendo chao cha kumficha ukweli aliotakiwa kuufahamu juu ya asili yake pamoja na wazazi wake kwa miaka mingi.

Alimhadithia kila kitu kuanzia maisha ya mateso aliyoishi mama yake Abikanile kwa kiasi alivyokuwa anayafahamu  pia alimpa barua iliyoachwa na mama yake huyo.

Hadi Johannes anamaliza kusimulia mkasa huo machozi mengi yalikuwa yanambubujika Mtima. Alimsikitikia sana mama yake kutokana na stori ya kuumiza aliyopewa, akajikuta anawachukia walimwengu kwa roho zao mbaya za kuwanyanyasa na kuwatesa watu walioishi na ulemavu wa ngozi.

“Binadamu wana roho mbaya sana,” alijikuta akitamka huku akiangua kilio.

“Usiseme hivyo mwanangu,” Alile alimwambia naye akifuta machozi.

“Ndivyo ilivyo mama, nitahakikisha napambana nao.”

“Vitabu vitakatifu haviruhusu kulipa kisasi.”

“Kwa hili Mungu atanisamehe.”

Kila mmoja sebuleni hapo alionekana kuyashangaa maneno aliyokuwa anayatamka Mtima, walishindwa kuelewa ni nini alipania kufanya kijana huyo dhidi ya binadamu, lakini kilichowashangaza zaidi, Mtima aliinuka huku ameishika mkononi barua iliyoachwa na mama yake Abikanile kisha akaondoka sebuleni hapo. Wote walibaki midomo wazi.

***

Urafiki kati ya Mtima, Abdulrahman na Destiny uliendelea kukomaa kadiri walivyozidi kukua kiumri, walikwishamaliza elimu yao ya msingi, wakasoma sekondari hatimaye wakaingia pamoja ngazi ya chuo walikotakiwa kujikita zaidi kwenye fani zao.

Mtima na Destiny wao walizidi kukomaa na masomo ya uchoraji huku ndoto zao zikiwa ni kuanzisha kampuni la ubunifu wa michoro mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa katuni jongefu (Animation).

Abdulrahman yeye alikuwa tofauti nao kabisa, aliendelea kujifua na michezo ya sarakasi huku mawazo yake yakiwa baada ya kumaliza masomo arejee Somalia kujiunga na jeshi la nchi hiyo, siku zikaendelea kusonga mbele lakini bila yeyote yule kutegemea miongoni mwa rafiki hao ni kumuona rafiki yao Mtima akibadilika kitabia .

JE, NINI KITAENDELEA? USIKOSE WIKI IJAYO.

Leave A Reply