The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 33

ILIPOISHIA

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo Destiny kwa Mtima, anaamua kuiuza supamaketi yake ili aanze kazi ya kumtafuta kijana huyo hatimaye kumshawishi aachane na vitendo vya kuua watu ovyo.
Ili kulikamilisha jambo hilo, Destiny aliwaza njia mbili ambazo alifikiri zingemuwezesha mapema kukutana na Mtima, moja ilikuwa kuwa mwanajeshi nyingine mwandishi wa habari, lakini baada ya kufikiria kwa kina mawazo ya kuwa mwandishi wa habari ndiyo yalishinda.

TAMBAA NAYO…

BAADA ya kuyapitisha mawazo hayo Destiny alitakiwa kutafuta chuo ambacho kilikuwa kinatoa kozi nzuri za masomo ya habari huku akipanga baada ya kumaliza masomo yake awe mwandishi wa habari wa kujitegemea ambaye angezunguka duniani kote hasa kwenye viwanja vya mapambano ya waasi kumtafuta Mtima.
Akiwa na malengo ya kuhakikisha anamrudisha kuwa binadamu mwenye moyo wa kawaida ikiwezekana wawe marafiki kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Ukweli ni kwamba hiyo ilikuwa kazi ngumu sana kwa Destiny kuifanya jambo ambalo alilifahamu wazi, lakini wakati huo hakujali matokeo mabaya ambayo yangemtokea, alikuwa amepania kwa dhati kuhakikisha siku moja Mtima anaachana na vitendo vya mauaji kwa watu wasio na hatia alivyokuwa anavifanya.
Bila kupoteza muda aliamua kumweleza mama yake Bi Lucy Okelo juu ya mawazo hayo huku akimtaka kumsaidia kuanzia kumtafutia shule na hata kumuwezesha kujikimu katika kipindi chote atakachokuwa katika masomo yake.
“Kwa nini umeamua kuwa mwandishi wa habari?” Mama yake alimuuliza.
“Ni taaluma sahihi kwangu.”
“Sawa, lakini kumbuka msimamo ni jambo muhimu katika maisha mwanangu, umri ulionao ni mzuri kuandaa mustakabali mzima wa maisha yako ya baadaye!”
“Hilo mbona nalifahamu mama.”
Bi Lucy Okelo hakuhitaji kabisa kumkatisha tamaa Destiny kwa kile alichokuwa anawaza kukifanya, aliamua kuwasiliana na rafiki yake wa muda mrefu Profesa Christopher Aoun, Rais wa Chuo Kikuu cha Habari cha Notheastern kilichopo huko Boston, Massachusetts, Marekani.
“Anategemea kuanza masomo lini?”
“Muda wowote kuanzia sasa.”
“Sawa, kwa heshima yako nafasi itakuwepo kikubwa nipate uhakika wa siku atakayokuja ili kuweka sawa mazingira atakayofikia.”
“Usijali.”
Mipango ya safari na taratibu za masomo vilifuatwa mara moja, baada ya wiki mbili tayari zilikuwa zimekamilika kwa kutumia Shirika la Ndege la Emirates, Destiny alisafiri hadi Dubai huko akaunga na ndege ya Kermo Line A380 hadi Amsterdam, Uholanzi alikopata usafiri mwingine wa ndege iliyompeleka hadi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kenned, jijini New York, Marekani.
Hadi anafika marekani tayari yalikuwa ni majira ya saa 6 usiku, masaa 48 tangu atoke Kenya, alilala jijini hapo, siku iliyofuata kwa kutumia ndege ndogo zilizokuwa zinafanya safari ndani ya Marekani alisafiri hadi jijini Boston, akaihitimisha safari yake kwa upande wa anga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan.
Hali ya hewa jijini hapo ilikuwa ya baridi sana siku hiyo, ambapo baada ya kushuka kwenye ndege na kukaguliwa, Destiny aliyekuwa amevalia mavazi ya baridi kama walivyokuwa abiria wengine aliendelea kusogea hadi alipokutana na mwanamme mwenye asili ya Kizungu aliyebeba karatasi yenye maandishi makubwa yaliyoandikwa; DESTINY WELCOM IN BOSTON.
Msichana huyo aliachia tabasamu pana kisha akasogea hadi alipokuwa huyo Mzungu, wakaongea mawili matatu, kisha akapelekwa hadi alipokuwa Profesa Christopher Aoun, siku mbili baadaye Destiny aliuanza mwaka wa masomo katika Chuo Kikuu cha Habari cha Northeastern, kwake hiyo ilikuwa safari moja kwenda katika azma yake ya kumbadilisha Mtima.

Je, nini kitaendelea? Destiny atafanikiwa azma yake hiyo? Vipi mwisho wa Abdulrahman na Mtima? Usikose wiki ijayo.

Comments are closed.