The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo

ILIPOISHIA:
Nilikubaliana na mzee Sionjwi kuwa hashindwi na kitu kilicho nje ya kudra za Mungu. Nilishika mikono kifuani huku machozi yakinitoka kwa furaha, mkurugenzi alizunguka meza yake na kuja kuninyanyua na kunipigapiga mgongoni kunipongeza.
“Hongera kwa kuipata nafasi adhimu kama hii, nakuamini katika kazi yako na nidhamu yako nina imani utafanikiwa na Mungu akutangulie kwa kila jambo.”
“Amen, asante bosi.”

SASA ENDELEA…

“Basi nikuache ukaendelee na kazi, kesho utamkabidhi msaidizi wako aendelee na kazi zako zote, ili kuanzia kesho kutwa uwe na mapumziko na kujiandaa na safari.”
“Asante sana bosi,” nilijibu huku nikifuta machozi ya furaha.
“Basi kamalizie kazi.”
“Sawa bosi,” nilitoka ofisini kwa bosi nikiwa nimechanganyikiwa kwa furaha.
Nilijikuta nikimpita Safia bila kujua mpaka aliponishtua.
“He! Shoga kulikoni kunipita kama gogo kuna nini tena?”
Niligeuka kumtazama Safia aliyekutana na machozi kitu kilichozidi kumshtua na kutoka kwenye kiti chake na kuja haraka kunikumbatia akiamini nina matatizo.
“Jamani shoga yangu kuna nini tena?” Safia aliniuliza kwa sauti ya huruma.
“Hamna kitu.”
“Hapana niambie mpenzi.”
“Kweli, haya ni machozi ya furaha.”
“He! Furaha ya nini mpenzi?” aliniuliza huku akinishika mabegani na kunitazama usoni. Nilikutana na michirizi ya machozi mashavuni kwake kuonesha jinsi gani matatizo yangu yanavyougusa moyo wake.
“Ile nafasi nimeipata.”
“Nafasi! Nafasi ipi?”
“Nakwenda kusoma.”
“Wewee! Kweli?”
“Kweli kabisa, nashukuru shoga Mungu amesikia maombi yetu.”
Tulijikuta tukikumbatiana tena kwa furaha, Safia aliacha ofisi yake na kunisindikiza mpaka ofisini kwangu. Niliamini naye alikuwa na furaha kama yangu, nilimuomba akaendelee na kazi ili jioni tupate muda wa kuzungumza kwa kirefu.
Siku ile nilifanya kazi kwa furaha huku nikiufikiria uwezo wa babu Sionjwi, kwangu ulikuwa muujiza ambao kwa akili yangu ya kawaida ilikuwa vigumu kuamini. Nilijiuliza babu Sionjwi nimpatie zawadi gani itakayolingana na kazi nzito aliyonifanyia.
Kwa vile nilijua nikiondoka sitarudi tena pale nilimalizia kazi zangu zote na kuandaa mambo ya kumkabidhi msaidizi wangu ambaye niliamini ndiye atakayeshika nafasi yangu. Kutokana na ubize na furaha ya safari hata muda ulivyokwenda sikujua.
Safia aliponipitia twende tukale nilimweleza siwezi kutoka kwa vile nilitaka kumaliza kazi zote. Nilimuomba aninunulie soda na keki, huwezi amini kwa furaha ya safari hata njaa sikuisikia kabisa.
“Shoga soda na keki tu kwa nini nisikuletee chipsi kuku.”
“Shoga hata hiyo soda keki nakunywa tu basi kwa vile mchana usipite.”
“Mmh! Au umeshiba safari?”
“Shoga wee acha tu kwangu naona muujiza.”
“Shoga ilikuwa riziki yako na siku zote riziki ya mtu haipotei.”
“Basi shoga baada ya kupata ujumbe ule furaha niliyoipata hata njaa nasikia?”
“Basi nitakuletea keki na soda.”
“Hapo umecheza hata hivyo naweza kuvibakiza.”
“Mmh! Sasa hiyo sifa hata soda na keki ubakize?”
“Safia we wahi acha nikimbizane na kazi leo siondoki mpaka nimalize kila kitu ili kesho nikifika nakabidhi kazi kwa muda mfupi na kwenda kupumzika kujiandaa na safari.”
“Sasa shoga siyo uende ukirudi unisahau.”
“Safia wewe ni zaidi ya kila kitu, hata kabla ya kuondoka kuna zawadi nitakupatia.”
“Usiniambie!”
“Tena itakufurahisha sana, basi wahi,” nilimuharakisha aondoke maana Safia porojo zilikuwa haziishi.
Safia aliondoka na kunipa nafasi ya kuchakarika kumalizia viporo vyote pia kuandaa mipango mipya ambayo nilikubaliana na mkurugenzi niifanye siku inayofuata. Mtoto wa kike nilichakarika kama sina akili nzuri huku nikihakikisha mahesabu yote yanakaa vizuri ili nikiondoka pasiwepo na maswali.
Kutokana na wingi wa kazi muda wa kutoka ulipofika ilibidi nimwambie Safia atangulie, aliondoka na kuniacha. Siku ile nilitoka kazini majira ya saa nne usiku nikiwa nimechoka sana. Lakini kutokana na furaha ya safari uchovu haukuwa mkubwa sana.
Kama kazi ile ningepewa na kampuni lazima siku ya pili ningelala nyumbani au kuingia kazini mchana. Baada ya kumaliza mambo yote muhimu niliondoka huku mlinzi akifunga mlango na mimi kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani nilioga na kupata chakula na kupanda kitandani. Kwa vile siku ya pili sikutakiwa kuwahi sana kutokana na sikuwa na kazi kubwa zaidi ya kukabidhi majukumu. Lakini kwa upande wangu nilitaka kumaliza mambo yangu mapema ilinilazimu kuwahi asubuhi.
Kwa vile nilimjulisha msaidizi wangu awahi ili tukabidhiane na kuelekezana mambo muhimu. Nashukuru nilimkuta kama tulivyokubaliana, kwa vile kazi kubwa nilimaliza jana yake hakukuwa na kazi kubwa kumwelewesha ilichukua saa tatu kumaliza kila kitu.
Baada ya kukamilisha kila kitu, nilipeleka paspoti kwa mkurugenzi kwa ajili ya viza, nilirudi kwa Safia ili kumpatia zawadi ya mkufu ambao niliununua kwa gharama bila kuuvaa. Kwa thamani ya ule mkufu nilijua angeupenda sana. Nilipofika mbele ya meza yake alisimama kabla hajasema neno nilimuomba afumbe macho naye alifanya hivyo.
Kwa vile nilikuwa nimeshaufungua mkufu nilimvisha na kumfunga kisha nilimweleza afumbue macho. Safia hakuamini alipouona mkufu wa thamani shingoni mwake. Alinikumbatia kwa furaha.

Je, kilifuatia nini? Usikose kufuatilia katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Comments are closed.