The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 42

0

Huku Mtima na Abdulrahman wakionekana kuanza kukwaruzana kutokana na tabia mpya alizoanza kuonesha Mtima, upande mwingine Destiny anashtuka usingizini baada ya saa nyingi kupita akiwa amepoteza fahamu. Baada ya kufumbua macho anahisi maumivu makali kichwani, alipotazama pembeni ya kitanda alipolala alishangaa kuona kundi la watu likiwa limemzunguka jambo lililomfanya ahoji juu ya kilichotokea mpaka akawa mahali hapo…

Teremka nayo…

HADI wakati huo hakuna hata kitu kimoja ambacho Destiny alikuwa anakikumbuka akilini mwake. Baada ya majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwadondokea yeye, Elizabeth pamoja na watu wengine waliokuwepo eneo hilo, Destiny alibahatika kuwa mmoja kati ya watu 20 pekee waliobahatika kuokolewa katika tukio hilo la kihistoria.
Elizabeth alifia palepale, lakini hata Destiny mwenyewe na watu waliookolewa walikuwa wameungua vibaya na kuharibika sura zao, urembo wote aliokuwanao mwanamke huyo haukuwepo tena, makovu ya moto yalikuwa yamejaa mwilini mwake.
Baada ya kuokolewa alibahatika kukutwa na mkoba wenye kitambulisho chake cha kazi kilichoisaidia serikali ya Tanzania kufahamu alikuwa ni nani na alikwenda nchini hapo kufanya nini, ambapo baada ya kutangaza jina lake kwenye vyombo vya habari mama yake, Bi. Lucy alijitokeza, akamchukua na kumpeleka nchini India kwa ajili ya matibabu.
Alipofikishwa huko alifanyiwa vipimo vya kina ikagundulika alikuwa na matatizo kwenye ubongo, maji yanayouzunguka ubongo wake ambayo kitaalamu huitwa Cerebrospinal Fluids yalikuwa yamemwagika nje. Akafanyiwa operesheni na kupewa matibabu, wakati huo ilishapita miezi mitatu akiwa kitandani na afya yake iliendelea kuimarika kwa mafanikio makubwa.
Siku zikazidi kusonga mbele baada ya miezi mitano Destiny akawa amekwishapona kabisa lakini kilichomuumiza sana moyo ulikuwa ni muonekano wake wa wakati huo.
Hakuwa msichana anayevutia tena, sura yake ilijikunjakunja na kutengeneza mikunyanzi kuliko kawaida kiasi kwamba msichana huyo akajikuta akiangua kilio kila alipoutazama uso wake kwenye kioo.
Lakini hakuwa na namna ya kufanya, kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele ilimbidi akubaliane na hali halisi, akarudi tena Tanzania alikosikia bado Kundi la Wab linaendelea kufanya mashambulio katika sehemu mbalimbali nchini humo, jambo lililowashangaza ndugu zake wengi.
Alipofika huko hakuwa na msaada wowote kama ilivyokuwa awali kwa Elizabeth, kutokana na hali aliyokuwa nayo watu wengi hawakuhitaji kabisa kumkaribia, kila aliyemhitaji awe karibu naye alikuwa anamkimbia na ilifikia hatua watu wengine wakawa wanamtania kwa kumfananisha na Zombi.

***
Ilikuwa siku tulivu, Destiny alikuwa kwenye chumba cha hoteli aliyofikia Tanzania akiendelea kutazama taarifa ya habari kupitia televisheni.
Akizidi kukazia macho kwa makini kutazama kilichokuwa kinaendelea mara ilitangazwa taarifa juu ya tukio ambalo Kundi la Wab walinyetisha kulifanya jijini Mwanza katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Baada ya kuitazama kwa makini taarifa hiyo, Destiny aliinuka harakaharaka kitandani kisha akakusanya baadhi ya vitu vichache muhimu na kuondoka mbio hadi mapokezi alipokabidhi funguo, bila kuongea neno lolote alitoka hadi nje alikokodi teksi iliyompeleka moja kwa moja hadi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Baada ya kufika uwanjani hapo aliulizia sehemu walikokatisha tiketi za safari ya ndani ya Tanzania, akapata iliyomruhusu kusafiri usiku wa siku hiyo hadi jijini Mwanza.
Akiwa kwenye ndege iliyozidi kupasua anga mawazo yake yote yalikuwa kwa Mtima, alitamani sana kuikamilisha azma yake, ndani ya dakika 50 tayari alikuwa jijini Mwanza, alikokwenda kufikia kwenye hoteli ya Tilapia.
Bila kupoteza muda mapema siku iliyofuata Destiny alikuwa eneo la karibu kabisa na Hospitali ya Rufaa Bugando akisubiri kushuhudia kitakachotokea.
Akizidi kusubiri, majira ya saa tisa mchana aliliona gari aina ya Landrover Discover likiingia kwa kasi hospitalini hapo, akawashuhudia watu wawili walioshika mitutu ya bunduki wakishuka kwenye gari hilo na kuanza kuua watu hovyo.
Destiny akachomoka kama mshale mahali alipokuwa akiwa amebeba kamera na vifaa vyake vya kuchukulia habari huku akitaka avuke barabara kuelekea eneo la tukio akidhamiria kufika mahali alipokuwa Mtima.
Hakuweza kutazama hata huku na kule wakati anaingia barabarani, akili yake yote ilikuwa sehemu moja, kwa Mtima, sasa ile anaingia tu barabani na kukaribia kufika katikati ya barabara hiyo, katika hali ya kushangaza lilitokea pembeni yake lori kubwa la mizigo lililomgonga Puuu!
Destiny akadondoka na kugalagala kwenye rami kisha akadumbukia kwenye mtaro uliokuwa pembeni ya barabara na kunyamaza kimya, upande mwingine risasi ziliendelea kurindima wala hakuna aliyejali kuhusu yeye, kila mmoja alikuwa akikimbia kuokoa uhai wake.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply