Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani -08

ILIPOISHIA:
“Ina maana Bantu kitendo changu cha kumdanganya kimemuuma sana na kuona kila siku nilikuwa namdanganya? Mmh! Ni nani aliyemwambia mimi nipo kule lazima kuna wachawi wanao niwangia kila siku na kutaka kujua maisha yagu yanavyokwenda ili waharibu.
SASA ENDELEA…

Nilijikuta nimepoteza watu wawili muhimu kwa wakati mmoja, lilikuwa pigo kubwa moyoni mwangu. Niliamua kupiga moyo konde kwa kujua maji yamekwisha mwagika siwezi kuyazoa japo kumpoteza Abdul ni hasara kwa maisha yangu mwanaume aliyenijali kama mkewe wa kumuoa.
Tukio lile japo lilinishtua halikunichanganya sana akili kwa kujua nitapata mtu wa kuziba nafasi zao.
Siku zote nilijifananisha na ulezi chakula cha ndege kila njiwa akionaye lazima atue.
Niliyaanza maisha yangu ambayo hayakuwa na upungufu mkubwa, naweza kusema Bantu lilikuwa ni pengo nililolifananisha na mchungwa wa uani uliong’olewa, ambao sikupata tabu kuchuma matunda yake kila ninapo kuwa na hamu ya machungwa.
Nilijua itanigharimu kumpata mwanaume shababi kama yeye awezae kunikata kiu ya mapenzi. Hakuchukua muda nilipata bwana mmoja afisa wa jeshi ambaye aliingia kichwa kichwa. Mmh! Nilishangaa uwezo wake wa pesa, alinipa kila nilichokitaka. Mapenzi yetu yalikuwa kukutana naye kwa wiki mara mbili.
Lakini alijikuta akinogewa na kuongeza siku zilikuwa mbili zikaja tatu mara nne, ooh, kila siku. Kukutana kila siku siyo tatizo kilichoniudhi ni wivu wa kijinga hapo ndipo nilipoamua kuvunja mapenzi na yeye hakuwa tayari kuvunja mapenzi. Alinipiga mkwala asinione na mwanaume yeyote atamuua.
Mbona makubwa yaani mapenzi siku hizi yamekuwa lazima, nilimwambia mapenzi siyo lazima masharti aliyonipa yanachekesha pale aliponiambia kama simtaki yeye basi niwakatae wanaume wote.
Nilijua ni maneno ya kuchanganyikiwa si mchezo mwanaume akiingia kichwa huniganda kama luba. Tatizo kubwa upande wangu ni kuwekewa wivu wa kijinga wakati hujanioa.
Baada ya kuachwa na mwanajeshi nilijikuta nachagua mabwana wastaarabu, nilipenda waume za watu ambao hawafanyi mapenzi kama chakula wao mapenzi ni starehe. Nilijikuta napata bwana mmoja ambaye alikuwa ni afisa katika kampuni ya mafuta kwa kweli pamoja na kuwa na pesa nyingi lakini alikuwa mstaarabu sana.
Siku za kukutana huniuliza kama nina nafasi na ninapokuwa sina huwa hakasiriki, lakini nilijitahidi kutokumuudhi. Nilipanga mipango yangu ambayo haikuingiliana na mtu. Nilipata wanaume wa watu wanne ambao wote hawakujuana.
Niliweza kuwahudumia wote bila kujuana na kila mmoja alifurahia huduma niliyompa kwa moyo wote. Nilipata kila nilichokitaka kwa kweli ulikuwa mradi mzuri ambao ulikuwa haunigharimu nguvu nyingi zaidi ya kujitoa kimwili pia kuonesha najali.
Kila mwanaume aliyepata huduma yangu alitamani kunioa kwa vile niliwashinda mbali wake zao. Nilikuwa na heshima msikivu sijui kukasirika mwelewa, vitu ambavyo waolewaji wengi hawana. Kama nilivyokueleza baada ya kuacha na wanaume zangu na kuona adha yake, sikuwa tayari tena kuolewa kutokana na kujijua siwezi kukaa na mwanaume mmoja.
***
Siku moja nikiwa katika ukumbi wa hoteli ambayo nilipenda kwenda na mmoja wa mabuzi yangu. Nikiwa nimemuacha chumbani baada ya kustareheshana, nilitoka nje kufuata nyama ya kuchoma ambayo ilicheleweshwa na mhudumu kuletwa niliamua kuifuata jikoni.
Baada ya kutoka nje nikielekea jikoni, nikiwa sina hili wala lile nilisikia nikishikwa mkono na mtu. Nilipogeuka nilikuta ni yule bwana yangu wa zamani mwanajeshi.
“Hebu niachie we vipi?” nilipiga kelele huku nikijitahidi kujitoa mkononi mwake.
“Konso nilikuambia nini?” aliniuliza kwa sauti kuonesha amelewa huku harufu kali ya pombe ikiniingia puani mwangu.
“Kuhusu nini?”
“Ulifikiri nakutania basi leo ndiyo nitakuonesha mimi ni mwanajeshi, kuua kwangu ni jambo la kawaida kama kupiga mswaki.”
“Kwani mapenzi lazima?”
“Yaani umenifilisi ndiyo umeniacha siyo?”
“Nilikuita?”
“Sasa nasema nipeleke alipo huyo mwanaume ili ushuhudie nammwaga ubongo,” alisema huku akinikunja kwa nguvu.
“Siende popote.”
Aliponishika kwa nguvu niligoma kwenda, yule bwana alinizaba makofi mawili yaliyofanya masikio yazibe na kuona kizunguzungu. Alinishika kama kibaka aliyemtoroka askari, hivyo alimshika makini ili asimkimbie. Alitoa bastola kiunoni ili nimpeleke kwa yule bwana aliyekuwa chumbani akinisubiri nipeleke nyama choma.
Nilijua lazima bwana yule atafanya kweli kutokana na taarifa za matukio ya wanajeshi, niliwahi kusikia mwanajeshi amemuua mke wake na yeye kujilipua. Ilibidi niwe mpole ili nitunge uongo wa kumuokoa yule bwana. Lakini kibaya zaidi yule mwanajeshi alikuwa amelewa lazima angefanya alichokidhamiria.
“Basi mpenzi taratibu,” nilisema kwa sauti ya kubembeleza.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.


Loading...

Toa comment