The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa-45

0

Destiny anafanikiwa kupona baada ya muda mrefu kupita akiwa hospitalini mahututi kutokana na ajali mbaya aliyoipata, mzee Boti aliyemsaidia anamchukua na kwenda kuishi naye kwake lakini baada ya siku kadhaa majira ya jioni msichana huyo alimwambia mzee Boti alihitaji kuondoka nyumbani hapo kwenda kutimiza lengo lake la kumtafuta Mtima pia alimsimulia juu ya ukaribu aliokuwa nao na kijana huyo ambao ndiyo uliomfanya kuhangaika wakati huo kumtafuta.

Teremka nayo…

USIKU wa siku hiyo ulipotea, siku iliyofuata Destiny aliamka alfajiri akapanga mizigo yake vizuri kwa ajili ya safari ambapo wakati wa kuondoka ulipowadia alimshukuru mzee Boti na familia yake kwa wema wote waliomfanyia tangu mzee huyo alipomuokota baada ya kupata ajali mbaya ya kugongwa na gari.

“Kuwa mwangalifu huko unakokwenda na kama tulivyozungumza jana usiku, ukihitaji msaada wangu wowote usisite kunitafuta.”

“Nashukuru sana mzee.”

“Usijali, wewe ni sawa na mwanangu.”

“Kweli kabisa.”

Msichana huyo aliondoka nyumbani hapo kwa mzee Boti huku wanafamilia wote wa mzee huyo wakiisindikiza kwa macho teksi aliyoikodi kwa ajili ya kumpeleka hadi maeneo ya Kapripointi kwenye Hoteli ya Lion Bay alikochukua chumba namba 124.

Dhumuni kubwa la kuchukua chumba hotelini hapo ilikuwa ni kupata sehemu tulivu kwa ajili ya kufikiria zaidi ni namna gani angeianza tena safari ya kumtafuta Mtima na kumbadilisha kuwa binadamu mwenye moyo wa huruma ikiwezekana warudishe ukaribu waliokuwa nao siku za nyuma. Siku hiyo yote ilikatika Destiny akiwa amejifungia ndani ya chumba chake akitafakari juu ya suala hilo.

 *   *   *

“PUUU!” Ulisikika mlipuko mkubwa wa kitu mfano wa bomu.

“Mamaaa…mamaaa…mamaaa,” mara kelele za watoto zikaanza kusikika.

Ghafla hali ya hewa ilibadilika, watu waliokuwa wamefurika katika kanisa hilo la Isamilo Assemblies Of God (IAG) walianza kukanyagana wakijaribu kuyaokoa maisha yao lakini moto ulikuwa mkubwa mno, ulizidi kuwaka kiasi kwamba baada ya dakika kumi eneo zima lilipokuwa kanisa hilo kulikuwa kumefunikwa kwa moto.

Watu zaidi ya 130, wakiwemo wanakwaya, wachungaji, watoto na waumini wa kawaida waliteketea bila huruma, hata wasamaria wema waliojitokeza kwa ajili ya kutoa msaada hawakuweza kufanya jambo lolote.

Swali la nani aliyesababisha kutokea kwa mlipuko huo lilitawala anga zima la eneo hilo, lakini hakuna hata mtu mmoja aliyeweza kutola jibu.

Wakiwa wanaendelea kuelea kwenye dimbwi la maswali, ghafla mbele ya umati huo kulipokuwa na mti mkubwa wa Mkaribea alitokea mwanaume wa Kiarabu aliyevaa kiremba cheusi kichwani huku mkononi akiwa ameshika bunduki kubwa na kuanza kuua watu ovyo.

Vilio, vifo na kelele vikatapakaa mahali hapo kutokana na spidi aliyokuwa nayo muuaji, watu wengi waliendelea kuteketea lakini katika hali ya kushangaza alionekana mwanamke mwenye makovu mengi katika mwili wake akitambaa kuelekea kule alikokuwa muuaji na wakati huo ving’ora vya polisi vilianza kusikika vikielekea mahali hapo.

Sauti hizo za ving’ora ndizo zilizoifanya kengele ya hatari kulia kwenye kichwa cha Abdulrahman, alichoamua kukifanya ili kujihami na kutoweka eneo hilo, alimteka mwanamke yule aliyekuwa anatambaa kuelekea mahali alipokuwa na kutokomea naye kusikojulikana baada ya mapambano ya muda mrefu na polisi.

*   *   *

Siku iliyofuata akiwa ndani ya mgahawa wa hoteli hiyo ya Lion Bay akiendelea kupata kinywaji baridi, Destiny aliweza kushuhudia kupitia televisheni taarifa iliyotolewa punde juu ya kanisa lililolipuka maeneo ya Isamilo.

Moyo ulianza kumdunda kwa kasi, akafahamu tayari akina Mtima walikuwa wanafanya yao, bila kupoteza muda aliunuka na kukitelekeza chakula alichokuwa anakula, akaanza kukimbia hadi nje alikokodi bodaboda iliyomkimbiza hadi eneo la tukio.

Alipofika alikuta watu wakiwa katika hamaki kubwa, lakini kabla hata hajafanya lolote lile alitokea mtu aliyemfahamu kuwa ni Abdulrahman aliyeanza kuua watu kwa fujo.

Akili ya Destiny ilifanya kazi zaidi ya uwezo wake wa kawaida, akaamua kufanya jaribio la kumsogelea kijana huyo ambalo aliamini kabisa lingeweza kusababisha hata kifo chake, lakini hakujali, alijisemea moyoni liwalo na liwe lakini ilikuwa ni lazima amkaribie akiamini kupitia kwake angemfikia Mtima, akalala chini na kuanza kutambaa kuelekea kule alikokuwa Abdulrahman.

Kwa Abdulrahman msichana huyo aligeuka kuwa ngao yake baada ya kusikia ving’ora vya polisi, alimteka na kutokomea naye hadi yalipokuwa maficho yake kwenye Mawe ya Kuchungu, huko Ibanda.

“Mtima yuko wapi?” Destiny alimuuliza Abdulrahman huku kijana huyo akimfungia kwenye mti kwa kutumia kamba za katani.

Swali hilo lilimshitua Abdulrahman haraka akauinua uso wake na kumtazama msichana huyo mara mbilimbili.

“Mtima unamfahamu?” Abdulrahman aliuliza.

“Ndiyo, ninawafahamu nyie wote.”

“Sisi wote! Umetufahamu vipi?

 “Tumesoma pamoja”

“Wapi na wewe ni nani?”

“Mimi naitwa Destiny, tumesoma pamoja Uholanzi!”

“Mungu wangu, wewe ni Destiny?”

Je, nini kitaendelea? Usikose Simulizi hii ya kusisimua Jumamosi ijayo ujue kilichojiri.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply