The House of Favourite Newspapers

Kwa Pamoja Tunaweza Kuzuia Ukatili Wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake

Beatrice Mkenda.

HII ni kampeni ya miaka mitano ya kuhamasisha umma ili kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake nchini Tanzania. Kampeni inalenga kujenga/ kuleta vuguvugu la watu katika jamii wanaopinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake. Watekelezaji wakuu wa kampeni hii ni watu wanaojulikana kama wanamabadiliko pamoja na asasi rafiki. Kampeni hii ambayo watu wanaweza kubadili tabia na mienendo yao ya ukatili dhidi ya wanawake.

MWANAMABADILIKO NI NANI?

Mwanamabadiliko ni mtu jinsi yeyote ile awe mwanaume au mwanamke, mvulana au msichana ambaye ameweka dhamira kubadili tabia na mienendo yake juu ya ukatili dhidi ya wanawake na watu wengine. Dhamira hiyo ni lazima awashawishi na watu wengine kumi (10) au zaidi kwa hiyari yake ili wabadili mienendo na tabia zao dhidi ya ukatili. Watu hawa (Wanamabadiliko) wanaweza kufanya kazi kama kikundi au kila mmoja peke

Janeth Mawinza

 

Mwanamabadiliko:

  • Kutambua aina kuu nne (4) za ukatili dhidi ya wanawake (Kihisia, Kiuchumi, Kijinsia na Kimwili)
  • Kuhamasisha watu walio karibu yake kubadili mienendo na tabia zao dhidi

 

  • Kutafakari pamoja na jamii juu ya mila na tamaduni inazonyanyasa wanawake na jinsi ya kuchukua hatua pindi tabia hizo zinapojitokeza.
  • Kama shule, mikutano mbalimbali ya kijamii, vituo vya afya pamoja na uongozi katika ngazi ya mtaa.
  • Awe jasiri na mwenye msimamo katika kutetea na kupinga ukatili dhidi ya wanawake.

 

Beatrice Mkenda ni mwanafunzi wa shule ya Ilemela mkoani Mwanza. Anatueleza namna anavyopinga ukatili wa kijinsia kutokana na mafunzo aliyopata kupitia kampeni ya Tunaweza.

“Kuna aina nne za ukatili wa kijinsia; kuna ukatili wa kingono, wa kiuchumi, wa kisaikolojia na wa kimwili.” Anasema Beatrice.

George Mtambalike.

Beatrice anasema mafunzo ya kampeni ya Tunaweza yamemsaidia yeye kama mwanafunzi kujua namna ya kujitetea na kupata haki yake. Anasema mafunzo hayo yamemsaidia kujua namna ya kuishi na wenzake kwa amani na upendo. “Kuna wakati mwingine sisi wenyewe kama vijana tulikua tunafanyiana vitendo vya ukatili bila kujua.”

 

Beatrice anashukuru kupata elimu juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia na ameahidi kuisambaza elimu hiyo kwa jamii yake. “Kuna jamii nyingi ambazo akina mama bado wanakandamizwa, elimu hii itanisaidia kusimama na kuwatetea.”

 

Beatrice anasema atafanya utetezi wa haki za wanawake kadiri ya uwezo wake na atakaposhindwa atawashauri waliofanyiwa ukatili kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia na watoto ya polisi kwa msaada zaidi.

 

“Pale ambapo tunapewa mafunzo na kuyatendea kazi ipasavyo ile ndio hali ya kusema kwamba mtu ana busara na hekima.” Anasema Beatrice na kuongeza kwamba maendeleo huletwa na jamii inayoishi kwa amani na upendo bila kufanyiana vitendo vya ukatili.

 

“Kampeni ya (Tunaweza) imeweza kunibadilisha kwa kiasi kikubwa sana.” Anasimulia Janeth Mawinza mkazi wa Dar es salaam. “Mpaka watoto wangu na wajukuu zangu pamoja na jamii inayonizunguka wanaishi kwa amani.”

Betinisimbo Shija

Janeth ambaye ni mama wa familia anasema kupitia mafunzo ya ukatili aliyoyapata ameweza kuona mabadiliko makubwa sana yeye binafsi, familia yake na jamii kwa ujumla. “Pale ninapoona vitendo vya ukatili, ninachukua hatua.”

 

“Watu wa familia yangu pia wamekuwa wanamabadiliko wakiendesha kampeni hii kila kona baada ya mimi kuwa mwanamabadiliko.”

 

Janeth anasisitiza kwamba ili kufanikiwa kutokomeza aina zote za ukatili ni lazima jamii nzima iwajibike. “Kila mtu ana nafasi na ana wajibu wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake.” Anasema.

“Wanawake ni watu muhimu sana ndani ya jamii kwa sababu jamii imewategemea zaidi wanawake katika masuala mbalimbali.” Anasema Janeth na kuongeza kwamba ili taifa lipige hatua ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika jamii.

Janeth anasema kutetea haki za wanawake sio jambo rahisi na kwamba linahitaji umakini na uchambuzi ili kuona ukatili ambao mwanamke anaupitia.

“Kila mtu atumie nafasi yake alipo, atumie mamlaka yake aliyonayo, atumie umri wake alionao katika kulinda na kumtetea mwanamke.”

 

George Mtambalike

George Mtambalike ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mogu, Kipawa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

George anasema baada ya watu kupewa mafunzo ya kampeni ya Tunaweza wengi wanabadilika na kuahidi kuacha tabia za unyanyasaji dhidi ya wanawake. “Jamii imekuwa na uelewa mpana na wanawake wengi wametambua haki zao.”

 

Anaendelea kufafanua kwamba katika jamii yake sasa wanawake wamekuwa wakishirikishwa kwenye kufanya maamuzi hasa kwenye masuala ya dhamana wakati wa kuchukua mikopo. “Kutokana na mabadiliko haya ya kifikra, sasa mwanamke anathaminika kabisa na anapewa haki zake.”

Faraja Komba.

George anashauri masuala ya haki za wanawake zikiwemo haki za kumiliki ardhi, unyanyasaji wa kijinsia yaongezwe kwenye mitaala ya elimu kuanzia ngazi za shule ya msingi hadi vyuo vikuu. “Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaiingizia jamii uelewa wa pamoja.”

Dawati la Jinsia na Watoto

Betinisimbo Shija anasema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo kama dawati la jinsia na watoto ni pamoja na wananchi kuchelewa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na kukosa ushirikiano kutoka kwa jamii, “unapoenda eneo la tukio unakosa ushahidi na vielelezo ambavyo vinasaidia katika ufuatiliaji wa kesi.”

 

Faraja Komba kutoka kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Polisi Mwanza anasema kitengo hicho kinashughulikia kesi zote zinazohusiana na ukatili kwa haraka na faragha. Aidha anasema, kitengo chao hutumia daftari maalum kurekodi na kupata kumbukumbu ya makosa ya ukatili wa kijinsia yanayojitokeza kwa mwaka.

 

Prisca Komba kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Dar es salaam ametaja changamoto kubwa wanazokutana nazo katika kitengo chao kuwa ni pamoja na watu kukubaliana baada ya kufungua kesi na kutokomea. “Unafungua kesi vizuri, unaiandaa kupeleka mahakamani, unapomtafuta mlalamikaji ambaye alikua amefanyiwa kitendo, humpati kabisa.”

 

Aidha Inspekta Komba anasema, kesi zingine wanakubaliana na kulipana pesa hivyo kuitaka jamii kufikiria endapo kiasi chochote cha pesa kinatosha kuondoa ugonjwa mkubwa ambao mtoto anaweza kuupata kwa kufanyiwa ukatili au kupoteza kizazi na kuwaharibia kabisa maisha yao.

Inspekta Komba ametoa wito kwa watu wanaofungua kesi polisi wasirudi nyuma waache haki itendeke.

Rehema Mayuya

“Kabla sijaifahamu kampeni ya Tunaweza kuna vitu nilikuwa nafanyiwa ndivyo sivyo lakini sikujua kama nafanyiwa ukatili.” Anasema Rehema Mayuya mwanamabadiliko kutoka Dar es salaam.

Rehema anasimulia kwamba hapo awali aliwahi kufanyiwa ukatili wa kupigwa na kuporwa viwanja na mumewe. “Alichukua vile viwanja akaninyang’anya hati zote.”

 

Rehema anasema tangu ajiunge na Kampeni ya Tunaweza mwaka 2013 imemsaidia kujitambua yeye binafsi, kutambua haki ya mwanamke, haki ya yeye kama raia wa Tanzania. “Kampeni hii imenibadilisha kutoka kule nilikokuwa na hapa nilipo ni vitu viwili tofauti.”

“Ukatili basi, sasa nahitaji mimi kama mwanamke nisimame, nipambane, nitetee haki yangu, nitetee na haki za wanawake wengine ambao wanafanyiwa vitendo vya ukatili.” Anasema.

Elizabeth Frank

Elizabeth Frank ni mwanamabadiliko anayesoma katika Shule ya Sekondari Lumala iliyopo mkoani Mwanza.

Elizabeth anasema ukatili majumbani mara nyingi hufanywa na wazazi hasa wa kambo kwa kuwanyima watoto chakula au kuwapiga bila kosa, “huo ni ukatili.” Anasema.

“Mashuleni napo kuna wakati unakuta mwalimu anamtaka mwanafunzi kimapenzi. Mwanafunzi anakosa sehemu ya kwenda kushtaki.” Anasema Elizabeth.

“Wavulana pia wanatutendea vitendo vya ukatili kwa sababu wao wanajua wana nguvu zaidi kuliko wasichana.”

 

Elizabeth anafafanua kwamba kuna wakati wanafunzi wa kike wanapewa vitisho na wavulana ili wasiripoti kwa walimu wanapowatendea vitendo vya ukatili, “ukienda kushitaki kweli anakuijia nyumbani au anakuvizia njiani na vikundi vyake anakupiga.”

Baada ya kupata elimu ya ukatili kupitia Kampeni ya Tunaweza Elizabeth anasema ameweza kubadilika na kuzitambua haki zake pamoja na kufahamu umuhimu wa kutoa taarifa za ukatili katika vyombo husika.

Neofita Kunambi

“Nachukia sana vitendo vya ukatili.” Anasema Neofita Kunambi mfanyabiashara ndogondogo, mkazi wa Dar es Salaam.

Neofita ni mwanamabadiliko katika jamii yake hivyo hujishughulisha na kutetea haki za wanawake na watoto.

Anasimulia namna ambavyo ameshiriki katika kesi mbalimbali za ukatili ikiwemo kumpeleka polisi mama aliyemchanja mwanae katika unyayo na wembe. “Nilimchukua yule mama nikampeleka katika dawati la jinsia kisha tukaenda ustawi wa jamii mahakamani Sinza, akapewa onyo.”

“Kampeni imenibadilisha vizuri sana kiasi kwamba sahivi sikubali hata kitendo kimoja cha ukatili wa kunyanyasika mtoto au mwanamke kinipite.”

Neofita anatoa wito kwa jamii kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili kupinga ukatili.

Pamela Kijazi

“Matukio mengi ambayo yanatokea yanayohusiana na ukatili mara nyingi hayaripotiwi. Watu katika jamii wanayaacha, wanayaficha.” Anasema Pamela Kijazi, Afisa Ustawi wa Jamii Tarafa ya Ilemela Mkoani Mwanza.

Pamela anasema matukio mengi ya ukatili yanayotokea katika jamii huishia kujadiliwa ngazi ya familia na kuyamaliza wao wenyewe. “Mfano binti anaweza akapewa mimba lakini familia ikakaa ikajadili lisifike popote.” Anasema.

Pamela anasema Kampeni ya Tunaweza imesaidia jamii kupata uelewa juu ya aina mbalimbali za ukatili na kwamba, “watu wameanza kuripoti vitendo vya ukatili.”

Pamela anasema halmashauri inafanya kazi kwa mujibu wa sera na sheria zilizopo ikiwemo sheria ya mtoto ya mwaka 2009, sera ya elimu n.k. “Tunashirikiana na wadau wengine kama polisi kuhakikisha kwamba matukio yote yanayohusiana na ukatili yanaripotiwa.”

Pamela ametoa wito kwa vyombo vinavyohusiana na masuala ya ukatili kushirikiana kwa pamoja ili kuwa na matokeo chanya ya kupinga ukatili. Amevitaja vyombo hivyo kuwa ni pamoja na Idara ya Ustawi wa Jamii.

Aidha ameiomba jamii kutoa taarifa za ukatili kwa vyombo vya sheria na kwamba hiyo ni njia muhimu katika jitihada za kutokomeza vitendo vyote vya ukatili. “Naomba watu wasikae kimya wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.”

Fatma Hussein

Fatma Hussein ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru iliyoko Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, yeye ni miongoni mwa wanamabadiliko aliyepata elimu kuhusu ukatili kupitia kampeni ya Tunaweza.

Fatma anasema kampeni ya Tunaweza imemsaidia kutambua aina mbalimbali za ukatili ikiwemo ukatili wa kimwili hasa fimbo zisizo na idadi zinazotolewa kama adhabu mashuleni.“Adhabu ya viboko kupitiliza ni moja kati ya aina ya ukatili wa kimwili inayopelekea wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri mashuleni.” Anasema.

Akifafanua kuhusu ukatili Fatma anasema, ni vitendo wanavyofanyiwa watu kinyume na sheria na kwamba madhara yake ni makubwa sana. Aidha Fatma anatufahamaisha kuwa zipo aina mbali mbali za ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili, ukatili wa kisaikolojia pamoja na ukatili wa kiuchumi.

“Kampeni ya Tunaweza imenisaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kubadilika na kuamua kupinga aina zote za ukatili.”

Fatma anasema kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake walizungumza na walimu wao na kufanikiwa kupunguza adhabu ya viboko shuleni kwao hali ambayo imesababisha wanafunzi wengi kufanya vizuri darasani. “Kwa kipindi kirefu wanafunzi tumekuwa tukifanyiwa ukatili wa kimwili katika mashule bila ya sisi wenyewe kujua kwamba tunafanyiwa ukatili.” Anaongeza.

Fatma anawashauri watu wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kutoa taarifa katika vyombo husika.

Metrida Shija

“Wanafunzi walikuwa hawaelewi nini maana ya ukatili kwa hiyo kuna baadhi ya mambo walikuwa wanafanyiana wao kwa wao bila kujua kwamba ni kitendo kinachowaumiza wengine.” Anasema Metrida Shija, Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Bwiru iliyopo wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Metrida anasema wanafunzi wengi wamekuwa wakitendewa vitendo vya ukatili na wanavipokea kwa kuelewa kwamba ni mambo ya kawaida bila kujua kama ni ukatili. “Yapo masuala mengine walikua wanashiriki bila ya wao kujua kwa mfano tulikua na tatizo la wanafunzi kutoroka shuleni kwa kurubuniwa na vijana.” Anasema.

Metrida anasema Kampeni ya Tunaweza imewasaidia walimu na wanafunzi kuelewa mambo mengi kuhusiana na ukatili wa kijinsia ambayo walikuwa hawayajui. Anasema, “hapo awali mwanafunzi alikuwa akirubuniwa kwa fedha anaona ni jambo jema lakini baada ya kupata mafunzo kutoka Kampeni ya Tunaweza imewasaidia kufunguka na kujua kwamba kumbe jambo kama hili halina faida kwao zaidi ya kujipotezea nafasi katika kutafuta maisha binafsi.”

“Ninatoa wito kwamba serikali iweke pia mkono wake katika kuhakikisha elimu ya ukatili inatolewa kila sehemu. Jamii nzima ielewe nini maana ya ukatili.”

Mwl. Metrida anasisitiza juu ya umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii, kuanzia ngazi ya familia “kuna baadhi ya familia binti anaelezwa kabisa kwamba kuna umri wa kuolewa na ukiacha kuchangamka katika umri huo maana yake umepitwa na wakati.”

Comments are closed.