The House of Favourite Newspapers

Ladha ya Penzi Imepotezwa Kabisa na Simu

Na GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| XXLOVE

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa nafasi ya kunikutanisha nawe tena mpenzi msomaji wa safu hii murua ya XXLove. Hapa ndipo tunapopata elimu ya uhusiano wa kawaida, kimapenzi na maisha.

Bila hivyo, mambo hayaendi. Mada tajwa hapo juu inatupeleka moja kwa moja kwenye mjadala wetu. Tukubaliane kuwa mapenzi ya siku hizi yamepoteza kabisa mvuto.

Yamepoteza ladha yake halisi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Ujio wa teknolojia na huduma za simu si jambo baya lakini matumizi ya mitandao na huduma hiyo kwa jumla ndiyo inayoleta shida kwa watumiaji husika. Ladha tamu na laini ya penzi baina ya wawili kwa sasa haipo tena kama zamani na nafasi hiyo imechukuliwa na ubize wa simu.

Wakati mwingine hata muda wa ‘chakula cha usiku’, unakuta mwanamke au mwanaume yuko bize na simu yake kujibu SMS na chatting  wakati mwenzake anamuandaa mwenzi wake kwa ajili ya chakula hicho. Ukiangalia, kwa sasa katika wa watu 10 wenye simu, basi asilimia 80 muda wote watakuwa bize na simu zao. Kwenye asilimia hiyo, umo wewe msomaji wa kike au wa kiume.

Kwa ubize wa kuchati muda wote, muda gani unautumia kujumuika au kuzungumza na mwenza wako juu ya maisha yenu ya uhusiano? Au ndiyo hadi usiku wakati wa kukutana faragha? Kama ndivyo, basi si sawa, jaribu kutumia simu yako vizuri, uwe una muda wa kuchati na kujadiliana naye mambo mengine ya msingi. Kila kitu kina kiasi, inapokuwa ‘too much’, inageuka kuwa sumu mbaya.

Ubize wa simu umeua mapenzi, kila mtu yuko bize na mambo mengine, mama yuko bize na kazi na hata akirudi nyumbani yuko bize na simu yake kuliko kuonesha mapenzi ya dhati kwa mwanaye aliyembeba tumboni miezi tisa.

Utamu na ladha ya penzi kwa wapenzi imepungua sana, wapendanao siku hizi wamegeuka kuwa wapenzi wa simu zao, muda mwingi kila mtu anautumia kuchati na kupata umbeya kwenye mitandao ya kijamii. Huko ndiko mapenzi yalikozikwa. Mume akitoka kazini, akifika nyumbani yuko bize na simu kuchati kwenye ma-group ya WhatsApp, Instagram, Facebook na mitandao mingine.

Vivyo hivyo kwa mwanamke, hakumbuki majukumu yake tena kama mama na hivi mumewe amemuwekea msaidizi (dada wa kazi), basi ni full kuchati tu. Mapenzi ya dhati kati ya mama na mtoto hakuna tena, baba na mama, rafiki na rafiki au mfanyakazi na bosi wake kwa sababu ya simu.

Kila mtu yuko bize na simu yake. Simu ndiyo mpenzi, ndiyo kila kitu, hakuna muda wa kukaa na kujadili mambo muhimu ya maendeleo, kama ikitokea  mkajadili basi ni kwa uchache na kwa wepesi ili kuwahi mambo ya mitandaoni. Naliona anguko la uhusiano na ndoa nyingi kwa zama hizi na chanzo cha anguko hilo ni simu na mitandao ya kijamii.

Mapenzi ya wapendanao yamegeukiwa kwenye simu, kwenye kuchati. Kama unahitaji kuimarika na kuimarisha uhusiano wako ni vyema ukawa na kiasi katika kutumia simu yako, punguza kuchati wakati wa mambo ya muhimu ya ujenzi wa familia.

Tenga muda wa kuzungumza na familia yako. Pia kuwa mtulivu unapojiandaa kula chakula cha usiku. Mpenzi msomaji, kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Insta:@ mimi_na_uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba zilizopo hapo juu.

Comments are closed.